HOJA
Pasaka ya Misri ni kivuli cha Pasaka ya Yesu Kristo
 

Na Elia Batendi

NAOMBA nafasi kwenye gazeti lako niweze kuchangia hoja katika makala ya Bw. Muhibu Said kuhusu Pasaka ni mnyama aliyechinjwa kukumbuka kukombolewa kwa wana Israili kutoka utumwani Misri, na kwamba Pasaka haina uhusiano na kifo cha Yesu kwani ilikuwepo kabla ya Yesu kuzaliwa na kwamba Wakristo wanaadhamimisha sikukuu iliyobuniwa na watu.

Kwanza kabla ya kuanza kuchangia hoja zake ambazo ni nyingi, Bw. Muhibu tayari anakubaliana kuwa kule Misri, Mwenyezi Mungu aliwaagiza wana wa Israili wachinje mnyama wa Pasaka. Kama Bw. Muhibu anakubaliana kuwa Waisraili waliagizwa kuchinja mnyama wa Pasaka, basi pia hana budi kukubali kuwa palikuwepo na tukio la Yesu kuchinja pale msalabani kwani Pasaka ya Misri ilikuwa ni kivuli tu cha Pasaka halisi (Kol. 2:17) na mwana kondoo halisi ndiye Yesu. (Yoh 1:29). Kama Bw. Muhibu hatambui tukio la kifo cha Yesu msalabani, basi pia hana budi kutotambua tukio la Pasaka kule Misri kama ambavyo Qur'an haitambui yote mawili.

Qur'an 17:101 inasema; "Na yakini tulimpa Musa hoja tisa zilizo wazi (za kuonyesha ukweli wa Utume wake). Waulize wana wa Israili alipowajia na Firauni akamwambia: "Hakika nakuona wewe Musa umerogwa (umeharibika akili)". Pia Qur'an 4:157; "Na kwa (ajili ya) kusema kwao " Sisi tumemuua Masihi Isa mwana wa Maryamu Mtume wa Mungu, hali hawakumuua wala kumsulubu..." Aya hizi mbili za Qur'an zinaonyesha wazi kuwa hapakuwepo na tukio la kuchinja Pasaka kule Misri na pia tukio la kifo cha Yesu Msalabani.

Ishara tisa zinazotajwa katika Qur'an 17:101 ni ishara ambazo hazikuwaletea wana Israili ukombozi kwani baada ya ishara hizo tisa, Firauni aliendelea kukaidi. Tunasoma katika Biblia Kut. 10:27 kuwa Firauni alikataa kuwaruhusu wana Israili ruhusa waende zao hata baada ya ishara ya tisa ambayo ilikuwa ni giza nene kwa muda wa siku tatu. Baada ya Firauni kukaidi hata baada ya hizo ishara tisa, Mwenyezi Mungu alimwambia Musa kuwa 'bado liko' pigo moja ambalo ndilo litamlazimisha Firauni awaruhusu wana Israili waende zao (Kut. 11:1). Pigo hili la kumi ndilo lililoleta ukombozi kwa wana wa Israil, pigo hili linaambatana na agizo la kuchinja mnyama wa Pasaka na damu yake kupakwa kwenye kila mlango wa wana Israili na damu hiyo iwe ishara kwao kuwa ndio wanaohitaji kukombolewa (Kut. 12:13).

Tukio hili la kumi ambalo ndilo la ukombozi wa wana Israili halitajwi ndani ya Qur'an, vivyo hivyo, tukio la ukombozi wa Yesu halitajwi ndani ya Qur'an. Nikirudi sasa kwenye hoja za Bw. Muhibu kuwa Pasaka ya Misri ina uhusiano na kifo cha Yesu?

Jibu ni ndiyo. Kama Biblia inavyosema kuwa Pasaka ya Misri ilikuwa ni kivuli tu cha Pasaka ijayo (Kol. 2:17). Mwana kondoo aliyechinjwa Misri ni kivuli cha mwana kondoo (Yesu) atakayechinjwa msalabani. Damu waliyoagizwa Waisraili (Kut. 12:7-13) waipake kwenye vizingiti vya milango yao iwe ishara kwao wanaokombolewa ni kivuli tu cha damu ya Yesu ambayo mtu akipakwa (akioshwa) atakuwa amekombolewa kutoka katika utumwa wa dhambi.

Wana Israili pia waliagizwa wamle Pasaka bila kumvunja mifupa ni kivuli tu tu kwamba Yesu hakuvunjwa mifupa. Twasoma kuwa 'basi' askari wakaenda wakamvunja miguu wa kwanza na wa pili aliyesulubiwa pamoja naye. Lakini walipomjia Yesu na kuona kuwa amekwisha kufa hawakumvunja miguu", ndivyo wana wa Israili walitakiwa kutomvunja mifupa mnyama wa Pasaka (Kut. 12:46).

Kama ilivyokuwa muhimu kwa wana Israili kupaka damu ya mnyama wa Pasaka kwenye milango yao ili waweze kutambulika, na kwamba ambaye hakupaka damu aliweza kukumbwa na pigo (Kut. 12:13) ndivyo ilivyo muhimu kwa kila mtu leo kupakwa damu ya Yesu ili mtu asihukumiwe. Yesu mwenyewe anasema "Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu nami ndani yake (Yoh. 6:56) hivyo Yesu ndiye Pasaka 91 Kor. 5:7)

Bw. Muhibu anaandika kuwa Pasaka iliagizwa kuliwa na wana Israili peke yao (Hesabu 9:9), pengine hakuelewa vyema. Mungu aliagiza mgeni anayetaka kula Pasaka afuate tu sheria, hapo kutakuwa hakuna mgeni na huyo aliyezaliwa katika nchi (Hisabu 9:14). Maneno haya ni kivuli tu cha tendo halisi kuwa wote waliompokea Yesu wamefanyika kuwa wana wa Mungu (Yoh. 1:12) Sasa hakuna tofauti ya Myahudi na Myunani, mtumwa wala huru, mume wala mke (Gal. 3:28) kwa hivyo, Pasaka ni ya wote.

Bw. Muhibu anaandika kuwa Mungu hapandezwi na tendo la mtu kusulubiwa kwani aliyetundikwa amelaaniwa (Kumb. 21:23). Lakini aliyetundikwa amelaaniwa kwa nini? Biblia inajibu kuwa amelaaniwa kwa sababu ametenda dhambi impasayo kufa (Kumb. 21:23) Yesu hakutenda dhambi yoyote (Yoh. 8:46) wenye dhambi ni sisi ambao ndio tunaostahili kutundikwa msalabani na kupata laana hiyo. Lakini Mwenyezi Mungu kupitia kinywa cha Nabii Isaya 53:4-5 anasema Yesu alijitwisha huzuni yetu, na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.

Hivyo, Yesu alifanywa laana badala yetu (Gal. 3:13) na Mwenyezi Mungu anaposema amelaaniwa aliyetundikwa ana maana amelaaniwa mwenye dhambi ambaye ndiyo sisi.

Bw. Muhibu anaandika kuwa hakuna mafundisho ya Mungu yanayothibitisha kufa na kufufuka kwa Yesu. Kwa hakika Mwenyezi Mungu amezungumzia sana tukio la Yesu kufa na kufufuka kupitia vinywa vya Manabii. Daniel 9:26 Wakati wa mwisho, mtumishi wa Mungu atauawa kikatili. Isaya 13:7 Watamtazama yeye waliyemchoma (Yesu alichomwa mkuki ubavuni Yoh 19:34). Zab. 31:5 Najiweka mikononi mwako (Yesu akalia akisema mikononi mwako naiweka roho yangu Lk. 23:46).

Pia kufufuka kwa Yesu kulisemwa kabla Zab. 16:10 Mungu hakumwacha kuzimu. Dan. 7:14 akapewa mamlaka, heshima na utukufu (baada ya kufufuka Yesu alipewa mamlaka mbinguni na duniani Mathayo 28:18).

Kwa kumalizia hoja ya Bw. Muhibu kuwa Yuda Iskariote alitakiwa kupewa sifa kwa kuwa aliharakisha ukombozi, na kwamba mchezaji anayeingia timu yake goli anastahili sifa kwa hakika Yuda hakuifungia timu yake goli bali alijifunga mwenyewe. Beki hatakiwi ajifunge kazi ya kufunga ilitakiwa ifanywe na maadui. Beki anayejifunga mwenyewe ni msaliti na ndivyo alivyokuwa Yuda. Maneno ya Yesu kuwa heri mtu huyo asingelizaliwa ni sawa na maneno ya kocha kumlaumu beki aliyejifunga kuwa 'heri asingesajiliwa'.

Kwa kifupi Pasaka iliyofanyika Misri ilikuwa kivuli cha Pasaka ya kweli ambayo ni Yesu Kristo (1 Kor. 5:7, Kut. 12:21).
 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook