SIASA
Jumuiya ziwe na mwelekeo wa kimapinduzi
 

KIMSINGI jukumu la kila Muislamu ni lile la kusimamisha ukhalifa duniani, au kwa tafsiri nyepesi, kuweka utawala wa sheria za Mwenyezi Mungu katika sayari hii. Hii ni kwa mujibu wa maelezo ya Mwenyezi Mungu pale alipowataarifu malaika kuhusu azma yake ya kuumba viumbe wengine, yaani Adamu, Hawa na watoto wao.

Na Batuli Hussein

Ili kufanikisha jukumu hilo, ni lazima uwepo ushirikiano na mshikamano madhubuti kati ya wanaharakati. Kwa ajili hiyo, imebidi ziundwe jumuiya, taasisi na halikadhalika mashirika, mabaraza na hata vikundi.

Madhumuni ya vyombo hivi ni kurahisisha harakati kwa kukusanya pamoja, nguvu, vipaji, vipawa na mawazo ya wanaharakati. Hii ikiwa na maana kwamba vyombo hivi vinalenga kuwawezesha wanaharakati kuwa na umoja na ushirikiano katika kuratibu na kuendesha programu mbalimbali za Da'awa.

Lakini yawezekana kwamba, baadhi ya au vingi kati ya vyombo hivi haviko hadhiri na dhana ya ukhalifa hasa kutokana na ukweli kwamba hapajawahi kuwepo mkutano wa pamoja kati yao, kujadili muelekeo wa harakati zao. Hata hivyo, kwa kuwa dira yao ni moja, yaani Qur'an, wajibu wa kusimaisha ukhalifa haukwepeki.

Hivyo basi, utitiri wa vyombo hivi haumaanishi utengano au tofauti ya muelekeo kati ya wanaharakati, bali, kwa kuzingatia maana ya ukhalifa, vyombo hivi vyaelekea kumoja mithili ya mito ambayo licha ya wingi wake, yote inatiririsha maji kuelekea baharini.

Kwa mantiki hiyo, lengo la vyombo hivi linavuka ile seng'enge ya kiroho iliyowekwa na matapeli wa kisiasa. Kwani ni muhali kuzungumzia ukhalifa bila kuigusa siasa.

Kusimamisha utawala wa kikhalifa ni jukumu linalohitaji muda mrefu na maandalizi ya kutosha kwa watawala na watawaliwa. Hata hivyo, katika kipindi hicho cha maandalizi, isimaaanishe kwamba, uongozi wa serikali za mpito uachwe mikononi mwa madhalimu eti kwa sababu mfumo wake ni wa kitwaghuti.

Badala yake wanaharakati ndio wapaswao kuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanapatikana na viongozi waadilifu wa kuiongoza jamii. Kwa kuzingatia mfano wa Dhulqarnain kuinusuru jamii na udhalimu ni miongoni mwa mambo mema.

Isitoshe, kupatikana kwa serikali inayojali haki za raia ni moja ya sehemu muhimu mno za maandalizi ya utawala wa kikhalifa. Sio tu serikali hiyo itatuepushia madhila bali pia itaweka rutuba kwa ustawi wa haraka wa serikali ya kikhalifa.

Kwa hiyo, pamoja na programu nyingine, vyombo vya harakati havina budi kuwa na programu ya kuandaa watu wa kushika nyadhifa mbalimbali katika serikali za mpito, sambamba na kuuhamasisha umma kuchagua viongozi hao wanaofaa. Kwa ajili hii yawepo mawasiliano bora kati ya vyombo vyote ili upatikane msimamo mmoja.

Kwa mujibu wa Dk. Sivalon, taasisi za dini nyingine zimekuwa zikifanya hivyo, ndio maana zimekuwa na nguvu na sauti serikalini. Kufanikiwa kwao kuwa na mawakala serikalini si suala la bahati nasibu, bali ni matunda ya programu zao.

Hata kitendo cha kina Omari kushindwa kuwajali watu wa imani yao si cha bahati mbaya bali ni matokeo ya ajenda. Kina Yusufu wanajikuta tu wamo katika mtandao. Kwa hali hii, sio siri tena kuwa chama chenye mtandao huo hakiwafai kabisa wavaa kanzu.

Hivyo mtu au chombo chochote kitakachojitoa katika muelekeo wa kikhalifa na kusimama upande wa mafisadi basi hapo kitakuwa kimejivua jukumu alilotupa Allah, na kwa hali hiyo waumini wajiepushe na mtu au chombo hicho.
 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook