Uchambuzi/hoja binafsi
 
Je, Yehova na Allah ni miungu tofauti ? - 2
 

Na Muhibu Said

KATIKA siku za hivi karibuni kumezuka madai kutoka kwa mtaalamu mmoja wa magonjwa ya akina mama wa Hospitali kubwa jijini kwamba Yehova siyo Allah (s.w.). Msingi mkuu wa dai lake hilo ni kwamba Yehova na Allah wamekuwa ni miungu tofauti eti kwa sababu Allah hana mwana, lakini Yehova ana mwana! Hata hivyo, katika uchambuzi wa awali katika toleo lililopita, tuliona jinsi Mwenyezi Mungu alivyokuwa akijitambulisha kwa majina tofauti kwa Manabii wake mbalimbali hadi Nabii wake wa mwisho Mtume Muhammad (s.a.w.). Kwa muktadha huo, tukaona pia kuwa Mwenyezi Mungu hakuwahi kujitambulisha kwa jina lake la Yehova kwa Manabii wake (kama Nabii Ibrahimu, Isaka na Yakobo a.s.) waliokuwepo kabla ya Nabii Musa (a.s.). Lakini tuliona kuwa alijifunua kwao kwa jina la "Mungu Mwenyezi". Pamoja na ukweli huo, tuliona pia kuwa Manabii na Waisraeli wka ujumla waliokuja baada yao (Nabii Ibrahimu, Isaka na Yakobo a.s.) walimtambua Mungu kwa jina la Yehova, Yahu, BWANA, Baba au kulingana na Mungu mwenyewe alivyojifunua au kujitambulisha kwao. Aidha, katika kuiendeleza kawaida yake hiyo (ya kujitambulisha kwa majina tofauti) tuliona pia jinsi Mungu alivyoamua kujitambulisha kwa Nabi wake wa Mwisho; Mtume Muhammad (s.a.w.) kwa jina lake kuu la Allah. Kwa hali hiyo, ikadhihirika kuwa Mungu-Yehova ndiye Mungu - Allah, ndiye BWANA, ndiye Mungu - Baba na ndiye Mungu - Mwenyezi. Hivyo basi, kama nilivyoahidi katika toleo lililopita, endelea kufuatana nami katika makala haya sehemu ya pili ili uone hoja za msingi zanazodhihirisha kwa uwazi zaidi majina ya Allah na Yehova kwamba ni majina yanayomhusu Mwenyezi Mungu yule yule mmoja.

Awali ya yote, kabla sijaingia kuzichambua hoja hizo muhimu, ni vyema kwanza tukaona pia ukweli kuhusu Allah japo kwa uchache, kama ambavyo tulivyoona katika toleo lililopita ukweli kuhusu Yehova.

Ukweli kuhusu Allah

Kwa mujibu wa mafundisho ya Qur'an tukufu, Allah ni jina tukufu la Mwenyezi Mungu, Muumba wa kila kitu, alilojifunua kupitia kitabu chake kitukufu cha Qur'an kwa Mtume wake wa mwisho kwa ulimwengu mzima; Nabii Muhammad (s.a.w.). Aya zifuatazo za Qur'an tukufu zinathibitisha ukweli huo, kama Mwenyezi Mungu alivyomfunulia Nabii Muhammad (s.a.w.) jina hilo, kwa kumwambia:

"Sema (Ewe Nabii Muhammad): Enyi watu! Hakika mimi ni Mtume wa Allah (Mwenyezi Mungu) kwenu nyinyi nyote, (Mungu) ambaye anao ufalme wa mbingu na ardhi, hapana aabudiwaye (kwa haki) ila Yeye; Yeye ndiye ahuishaye na ndiye afishaye. Basi muaminini Allah na Mtume wake, aliye Nabii Ummy (asiyejua kusoma wala kuandika) ambaye humuamini Allah na maneno yake. Na mfuateni yeye ili mpate kuongoka". (Qur. 7:158)

"Yeye ndiye Allah (Mwenyezi Mungu) ambaye hakuna aabudiwaye kwa haki isipokuwa Yeye tu. Anayeyajua yaliyofichikana na yaliyo dhahiri. Mwenye kuneemesha neema kubwa kubwa na mwenye kuneemesha neema ndogo ndogo".

"Yeye ndiye Allah (Mwenyezi Mungu) ambaye hakuna aabudiwaye kwa haki isipokuwa Yeye tu; Mfalme, Mtakatifu, Mwenye Salama, Mtoaji wa amani, Mwenye kuyaendesha mwenyewe mambo yake, Mwenye shani, Anayefanya analolitaka. Mkubwa, Allah yu mbali na hao wanaomshirikisha naye".

"Yeye ndiye Allah (Mwenyezi Mungu), Muumbaji, Mtengenezaji, Mfanyaji sura (za namna namna za viumbe); Mwenye majina (safi) mazuri. Kinamtukuza kila kilichomo mbinguni na ardhini. Naye ni Mwenye nguvu, Mwenye Hikima". (Qur. 59:22-24).

Pamoja na kujifunua kwake kwa Nabii Muhammad (s.a.w.) kwa jina lake hilo tukufu (la Allah) kama aya hizo juu zinavyojieleza, Mwenyezi Mungu pia hakuishia hapo tu. Lakini aliendelea kujidhihirisha katika aya nyingine nyingi mbalimbali za Qur'an tukufu kuwa Yeye ndiye Mungu yule yule mmoja aliyejifunua kwa Manabii wake wote waliomtangulia Nabii Muhammad (s.a.w.) kama aya ifuatayo (ya Qur'an tukufu) inavyomwambia Nabii Muhammad (s.a.w.) na Waislamu wengine wa umma wake kwa ujumla:

"Amekupeni sheria ya dini ile ile aliyomuusia Nuhu na tuliyokufunulia wewe na tuliyowausia Ibrahimu na Musa na Isa (Yesu), kwamba simamisheni dini wala msifarikiane kwayo...". (42:13).

Kwa ufupi, huo ndio ukweli halisi kuhusu Allah (s.w.). Kwamba ndiye Mungu Muumba wa kila kitu, mwenye sifa zote tukufu na kamilifu, ndiye Mungu yule yule aliyejifunua kwa Nabii Nuhu, Ibrahimu, Musa, Isa (Yesu) na kwa Mitume na Manabii wake wengine wote aliowaleta duniani. (Tazama Qur'an 6:83-87 na kadhalika).

Pamoja na ukweli huo, ni muhimu sasa tukaziangalia sifa hizo kuu za Mwenyezi Mungu wa kweli ambazo ndizo zinazodhihirisha kwa uwazi zaidi kwamba Allah na Yehova ndiye Mungu yule yule moja aliyejifunua kwa Manabii wake mbalimbali kwa majina tofauti. Aidha, kwa kuzingatia majina hayo (ya Allah na Yehova) na sifa hizo, tutaona pia kama kweli ndiye Mungu anayeabudiwa na Wakristo?

Kuwepo mwanzo (yaani kuwepo kabla ya yeyote na chochote)

Miongoni mwa sifa kuu zinazomdhihirisha Mungu wa kweli,sifa ya kwanza na ya msingi, ni kuwepo mwanzo, yaani kuwepo kabla ya yeyote na kabla ya chochote. Umuhimu kwa Mungu wa kweli kuwa na sifa hiyo, mbali na kutakasika na sifa sifa dhaifu (isiyomstahiki Mungu) ya kuumbwa au kuzaliwa, unazingatia Yeye kuwa Ndiye Mwanzilishi wa kila kitu (kinachoonekana na kisichoonekana). Kwa mantiki hiyo basi, ni dhahiri kuwa kigezo cha kwanza muhimu kinachoweza kuwa hoja ya msingi ya kutofautisha Allah na Yehova ni 'mmoja wao' kubainika kuwa hana sifa hiyo azizi.

Hata hivyo, tusomapo maanndiko ya Qur'an tukufu na Biblia takatifu, hatumuoni yeyote akidai sifa hiyo isipokuwa Mwenyezi Mungu yule yule mmoja aliyejitambulisha kwa Manabii wake mbalimbali kwa majina tofauti. Maandiko yafuatayo ya Qur'an tukufu na Biblia takatifu kwa pamoja yanathitibisha ukweli huu:

Biblia:

"Ni nani aliyetenda na kufanya jambo hilo, aviitaye vizazi tangu mwanzo? Mimi, BWANA, wa kwanza na wa mwisho, mimi ndiye". (Isaya 41:4)

"Ninyi ni mashahidi wangu, asema BWANA, na mtumishi niliyemchagua, mpate kujua, na kuniamini, na kufahamu ya kuwa mimi ndiye, kabla yangu hakuumbwa Mungu awaye yote, wala baada yangu mimi hatakuwepo mwingine". (Isaya 43:10)

Qur'an:

"Kinamtukuza Allah (Mwenyezi Mungu) kila kilichomo mbinguni na ardhini, na Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye Hikima. Ufalme wa mbingu na ardhi ni Wake, Anahuisha na Kufisha. Na Yeye ni Mwenye uweza juu ya kila kitu. Yeye ndiye wa Mwanzo na Ndiye wa Mwisho, naye ndiye Dhahiri na wa siri, naye ndiye Mjuzi wa kila kitu". (Qur. 57:1-3)

Kulingana na shuhuda hizo juu, tunaona wazi Biblia na Qur'an tukufu vyote vinamkariri Mwenyezi mmoja peke yake akijinadi kuwa ndiye wa mwanzo kuwepo ambapo kama mwenyewe (Mungu) anavyojieleza kwamba hakuna Mungu yoyote aliyemtangulia kuwepo; sembuse mzazi wa kumzaa!

Kwa shuhuda hizo ni wazi kuwa sifa hii pekee inadhihirisha kuwa Allah na Yehova ni Mungu yule yule aliyejitambulisha kwa Manabii wake mbalimbali lakini kwa majina tofauti.

Uumbaji:

Sifa kuu ya pili ya Mungu wa kweli baada ya sifa yake ya kwanza ya kuwepo kabla ya yeyote na chochote, ni Uumbaji. Kwani kwa kuwa kama tulivyoona hapo juu, Mungu mwenyewe akijieleza kwamba hakuna yeyote, chochote wala Mungu awaye yote aliyemtangulia kuwepo, hapana shaka ni lazima wote na vyote vilivyokuja baadae vitakuwa vimeumbwa na Yeye. Kwa kuzingatia mantiki hiyo na kwa vile hakuna yeyote wala chochote kilichodai au kuweza kudai kwamba kimejiumba chenyewe, ni dhahiri kuwa Yeye (Mungu) ndiye Muumba na vingine vyote ni viumbe vyake.

Kwa mantiki hiyo basi, sifa hii, pia ni kigezo kingine muhimu kinachoweza kuwa hoja ya msingi ya kutofautisha Allah na Yehova iwapo tu itabainika kuwa "mmoja wao" hana pia sifa hiyo (ya Uuumbaji). Hata hivyo, tusomapo maandiko ya Qur'an tukufu na Biblia takatifu tunaona ni Mwenyezi Mungu peke yake ndiye anayedai sifa hiyo. Ukweli huu tunaupata pia katika maandiko yafuatayo ya Qur'an tukufu na Biblia takatifu:

Biblia:

"BWANA, mkombozi wako, yeye aliyekuumba tumboni, asema hivi; Mimi ni BWANA, nifanyaye vitu vyote, nizitandaye mbingu peke yangu; niienezaye nchi; ni nani aliye pamoja nami?". (Isaya 44:24)

"Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi". (Mwanzo 1:1)

"Basi mbingu na nchi zikamalizika, na jeshi lake lote. Na siku ya saba Mungu alimaliza kazi yake yote aliyoifanya; akastarehe siku ya saba, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoifanya. Mungu akaibariki siku ya saba, akaitakasa kwa sababu katika siku hiyo Mungu alistarehe, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoiumba na kuifanya. Hivyo ndivyo vizazi vya mbingu na nchi zilipoumbwa". (Mwanzo 2:1-4)

"Umestahili wewe, Bwana wetu na Mungu wetu, kuupokea utukufu na heshima na uwazi kwa kuwa wewe ndiwe uliyeviumba vitu vyote na kwa sababu ya mapenzi yako vilikuwako, navyo vikaumbwa". (Ufunuo wa Yohana 4:11)

Qur'an:

"Na (juu ya hivi) wamemfanyia Allah (Mwenyezi Mungu) majini kuwa washirika wake, hali Yeye ndiye aliyeumba (si majini). Na wanamsingizia (Mwenyezi Mungu) kuwa ana mtoto wa kiume na wa kike. (Wakasema hayo) pasipo kujua. Ameepukana (Mwenyezi Mungu) na upungufu, na yu juu kuliko yale wanayomsifu nayo. Yeye ndiye Mwumba wa mbingu na ardhi. Inamkinikaje awe na mwana hali hana mke. Naye ndiye aliyeumba kila kitu (siyo badhi yake kavizaa). Naye ni mjuzi wa kila kitu. Huyo ndiye Mwenyezi Mungu,Mola wenu, hakuna anayeabudiwa kwa haki ila Yeye, Muumba wa kila kitu. Kwa hivyo mwabuduni Yeye (tu). Naye ni Mlinzi wa kila kitu". (Qur. 6:100-102)

Hapa tunaona wazi shuhuda hizo juu za Qur'an tukufu na Biblia takatifu zinamwonyesha Muumbaji pekee ni Mwenyezi Mungu yule yule mmoja aliyejitambulisha kwa Manabii wake mbalimbali kwa majina tofauti. Kwa shuhuda hizo basi, ni wazi kuwa sifa hii nayo inadhihirisha kuwa Allah na Yehova ni Mungu yule yule mmoja aliyeumba kila kitu.

Ukuu:

Kwa kuzingatia kuwa Yeye ndiye wa kabla ya yeyote na chochote na ndiye Muumba wa kila kitu, hapana shaka kuwa sifa kuu ya tatu ya Mungu wa kweli ni lazima iwe ni Ukuu. Ambapo tafsiri halisi ya sifa hii tukufu ni kwamba Mwenyezi Mungu amekizidi na kukipindukia kila alichokiumba kwa kila hali. Kwa mantiki hiyo, sifa hii pia ni kigezo kingine muhimu kinachoweza kuwa hoja ya msingi ya kutofautisha Allah na Yehova, iwapo tu itabainika kuwa 'mmoja wao' hana sifa hiyo. Hata hivyo, tusomapo maandiko ya Qur'an tukufu na Biblia takatifu hatumwoni yeyote akidai sifa hiyo zaidi ya Mwenyezi Mungu yule yule mwenye sifa tukufu tulizoziona hapo awali, kama maandiko yafuatayo ya Qur'an tukufu na Biblia takatifu yanavyodhihirisha ukweli huu:

Biblia:

"Kwa maana BWANA, Mungu wenu, Yeye ndiye Mungu wa miungu, na Bwana wa Mabwana, Mungu Mkuu, mwenye kuogofya, asiyependelea nyuso za watu, wala hakubali rushwa". (Kumbukumbu la Torati 10:17)

"Ee Mungu, njia yako i katika utakatifu; Ni nani aliye Mungu Mkuu kama Mungu?" (Zaburi 77:13).

Qur'an:

"Hivi ni kwa sababu Allah (Mwenyezi Mungu) ni haki (yuko); na wanachokiomba badala yake ni batili (hakiko), (ni uongo tu kwani hapana hata kimoja katika hicho kinachofanya anayofanya Mwenyezi Mungu) ndiye mtukufu (na ndiye) mkubwa". (Qur. 31:30)

"Kwa sababu mlikuwa akitajwa (akiombwa) Allah (Mwenyezi Mungu) peke yake mnakanusha na akishirikishwa mnaamini. Basi hukumu (leo) ni yake (Mwenyewe tu) Allah (Mwenyezi Mungu) alye juu, aliye Mkuu". (Qur. 40:12).

"Hayo ni kwa sababu Allah (Mwenyezi Mungu) yuko; na wale wanaowaabudu badala yake (Mwenyezi Mungu) hawako, na Allah ndiye aliye juu na ndiye Mkubwa". (Qur. 22:62)

Kulingana na shuhuda hizo juu, tunaona hapa Biblia na Qur'an tukufu vinafundisha sambamba kwamba sifa ya Ukuu ni ya Mwenyezi Mungu yule yule mmoja aliyekuwepo kabla ya yeyote na chochote, Muumbaji wa kila kitu.

Itaendelea toleo lijalo.
 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook