Kanda ya mauaji yaangaliwa karibu na Ikulu
 

Na Mwandishi Wetu, Tanga

MSIKITI Manara wa Nguvumali mjini hapa, nao umetoa nafasi kwa Waislamu wanaouzunguka kujionea kwa macho yao mauaji ya Mwembechai hapo Jumapili Aprili 11 mwaka huu.

Ukiwa masafa mafupi tu kutoka Ikulu ndogo ya mjini hapa, onyesho la Msikiti huo liliwakilisha kwa kasi yenye kuongezeka sikitiko la Waislamu kutaka wauaji wachukuliwe hatua.

"Waangalie wale, si wanaonekana waziwazi sijui kwanini hawakamatwi!", mmoja wa watazamaji wenye uchungu alisikika akilalama huku akionyesha kundi la askari lililokuwa likiwatwanga kwa marungu Waislamu waliokuwa tayari chini ya ulinzi wao.

Mtazamaji mwingine aliyeitwa na mwenzie kwa jina moja tu la Omar, akiwa amepandwa na hasira alisema; "Ningekuwa mimi pale wangenimaliza kabisa", pale kijana mmoja alipokuwa akivunjwa vunjwa mifupa kwa marungu kwa sauti ilisikika vizuri hewani, baada ya kutengwa kutoka kwa wenzake.

Kuwepo kwa akinamama kulihisiwa katika sehemu mbili za mkanda huo, kwanza pale kijana aliyeshika jiwe akikata roho huku akiwa amezungukwa na dimbwi la damu yake na vitu vyeupe kama ubongo. Sehemu nyingine ni pale wenzao walipokuwa wakiwashambulia askari kwenye viwanja vya mahakama ya Kisutu kwa maneno makali wakitaka jamaa zao wapewe dhamana.

Onyesho hilo lilisimamiwa na msaidizi Imamu wa Masjid Manara, Sheikh Mzee Balozi. Mapema kabla ya tukio hilo pia kiongozi mmoja wa makundi ya Tabligh alisimama na kuelezea umuhimu wa Waislamu kujitolea kwa mali na nafsi zao ili kuipigania dini ya Allah (s.w.).

Alipowauliza Waislamu wako tayari! Kwa mara tatu, Waislamu walijibu "ndiyoo!" Masjid Manara inasemekana ni wa mwanzo kwa mjini Tanga kuonyesha mkanda huo. Hata hivyo utafiti unaonyesha wengi wamekuwa wakinunua kutoka maduka ya kukodisha mikanda ya video.


Wasilimisha Kijiji

Na B. Mwakangwale

WATU kadhaa wasiokuwa Waislamu katika kijiji cha Mchito Dodoma Vijijini wameufuata na kuingia katika Uislamu imefahamika.

Akiongea na Mwandishi wa habari hizi katika ofisi za gezeti hili, Sheikh Salum Abubakar Kazi, alieleza kuwa yeye ni wa kwanza kusilimu kijijini kwao tangu mwaka 1991, baada ya kusilimu alipata mafunzo yake ya Uislamu Kimamba (Morogoro) kwa Sheikh Abubakar Swalehe Bombaheka kwa muda wa miaka mitatu (1993-95).

Baada ya kurejea nyumbani (Mchito) alikuta kuna Waislamu wawili, hivyo pamoja na yeye wakawa watatu; "Tulikuwa tukiendesha ibada zetu chini ya mwembe", alisema.

Alisema kuwa kwa kushirikiana na wenzake walifikisha ujumbe kwa wenzao na kufanikiwa mpaka sasa kuna Waislamu 220 wake kwa waume kijijini hapo.

Alieleza mafanikio mpaka hivi sasa wana Msikiti mkubwa na madrasa ya watoto, kinamama na kina baba.

Aidha, alieleza kuwa matatizo yanayowakabili ni upungufu wa walimu pamoja na kukamilika kwa madrasa na Msikiti.

Alipoulizwa ni nini kilichomfanya yeye Sheikh Salum kusilimu, alisema zamani alikuwa anaitwa Gilbart Ben, baada ya kusoma Injili (Biblia) kwa muda mrefu nilipata ukweli wa dini sahihi, Uislamu.


Waislamu Dodoma waomba Imam

Na Abu Zubeir, Dodoma

WAISLAMU wa kijiji cha Chamwino (Ikulu) wametoa wito kwa Waislamu wote wa kupatiwa Imam na mwalimu wa dini ambaye ataweza kutoa taaluma ya elimu ya dini kwa watu wazima na watoto, pia wanahitajia Imam kwa ajili ya Msikiti wao Masjid Taq'wa.

Msikiti huo uliwekwa jiwe la msingi na mstaafu Rais wa awamu ya pili mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi Machi 22, 1999. Ujenzi wa Msikiti huo umekamilika na ulizinduliwa rasmi kwa kusaliwa sala ya Eid el Fitri Januari 1999, na Sheikh kutoka kijiji cha Msanga (km 5 kutoka hapo Chamwino) Sheikh Mwinshehe.

Akiongea na mwandishi wa habari hizi aliyetembelea kijiji hicho hivi karibuni, Mwenyekiti wa Msikiti huo Bw. Hamis alisema miongoni mwa matatizo waliyonayo baada ya Msikiti kukamilika ni ukosefu wa mtu wa kuwaongoza katika ibada, Imamu na mwalimu wa Madrasa.

Bw. Hamisi alisema wapo watu tayari wameshajitolea nyumba kuwapangisha Imamu na mwalimu (bure) hivyo wanalohitaji ni kujitokeza Waislamu wenye elimu ya kutosha ili waweze kushiriakana katika kuhuisha Uislamu hapo kijijini.

Aidha, Bw. Hamis alisema kwa masikitiko makubwa kuwa sehemu hiyo ya Chamwino inafikiwa na wengi kutoka ndani na nje ya nchi hivyo wanapata aibu kubwa wageni wanapoingia Msikitini (kusali) na kuona Msikiti hauna Imam wa kudumu.

Kijiji cha Chamwino kina Waislamu 50 wote wakiwa ni wahamiaji (wafanyakazi) katika idara mbalimbali za serikali, aidha Muislamu mkazi (mzawa) ni mmoja tu.

Wakati huo huo, mwalimu Kimoro ambaye ni miongoni mwa akina mama wa kamati ya Msikiti huo, alisema hali zao ni mbaya sana hasa zile za kukosa Imamu na mwalimu wa watoto na watu wazima, kama Kimoro alisema pale inapotokea mtu (Muislamu) amefariki inawalazimu kutembea km 5 kumfuata Sheikh kijiji cha Msanga ili aweze kutoa huduma hiyo (faradhi kifaya) kwa marehemu.


   Mwinyi ashangiliwa kwa vifijo Tanga

Na Kassim Billo, Tanga

RAIS Mstaafu Alhaj Ali Hassan Mwinyi alishangiliwa kwa vifijo na vigelegele alipozuru mjini hapa kwa ziara ya siku tano kwa mualiko wa Taasisi ya kidini ya Kiislamu ya Maawal.

Akiwa katika ziara hiyo ya siku tano Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili aliweza kufungua vituo mbalimbali vya taasisi za Kiislamu mojawapo ikiwa ni ufunguzi wa shule ya watoto wadogo ya Maawal Islamic Centre iliyopo Mng'amboni mjini hapa katika siku ya kwanza ya ziara yake mjini hapa.

Katika hotuba yake aliyowahutubia Waislamu kwenye sherehe hiyo ya kufungua shule hiyo ya watoto wadogo, Alhaj Mwinyi alisema kuwa jambo bora zaidi lenye manufaa kwa Waislamu ni kudumisha umoja ambao utawawezesha kutekeleza kazi za mipango yao ya maendeleo.

Alhaj Mwinyi alifuatana na viongozi kadhaa wa kidini wakiwemo Masheikh alihudhuria sala mbalimbali katika Misikiti na baadae alijiunga na maandamano ya Dhafa iliyoandaliwa na Taasisi ya Maawal Islamu Association ya Tanga ambapo Dhafa hiyo ilizunguka katika barabara kadhaa za mji wa Tanga zikianzia Msikiti Mkuu wa Maawal.

Alhaj Mwinyi kila barabara aliyopita wananchi wa Tanga walionyesha mapenzi yao kwake kwa kumshangilia akifuatana na maofisa wa serikali pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Kepteni George Mkuchika pamoja na Sheikh maarufu Mohammed Hariri.


Nchi za Magharibi zimeanguka kimaadili - Sheikh Mbukuzi

Na Said Shariff

Sheikh Mbukuzi amesema kwamba pamoja na kuwa nchi za Magharibi ndio vinara wa madai ya kutetea haki za wanawake, lakini maadili ndani ya nchi hizo yanazidi kwenda kombo siku hadi siku kwa sababu sera zao zimeelekezwa kupinga mwongozo wa Mwenyezi Mungu.

Amesema nchi hizo zimeanguka kimaadili ambapo ulevi, uzinzi, kutembea uchi, kutokujali maisha ya kifamilia imekuwa ni sehemu ya utamaduni wa nchi hizo.

Sheikh Mbukuzi amesema katika nchi za Magharibi wanawake wamejivua utu wao na kujivika unyama. Kwao kutembea uchi ni jambo la kawaida. Nani atakayekubali kuwa sawa na watu hao? amehoji Sheikh Mbukuzi.

Kutokana na hali hiyo, Sheikh Mbukuzi amewataka wanawake wajihadhari na utamaduni huo wa nchi za Magharibi kwa sababu unavua utu, hadhi na thamani ya mwanamke inapotea.

Aidha, Sheikh Mbukuzi amewataka wanawake wa Kiislamu waendelee na msimamo wa kuvaa hijabu kwa kutaraji radhi za Allah (s.w.).

Sheikh Mbukuzi amesema wao wanawake wa Kiislamu ndio mfano mwema wa kuigwa na jamii. Alisisitiza kuwa wasiyumbishwe na majina ya kejeli wanayoitwa kutokana na kuvaa kwao hijabu.


Njaa yaikumba Handeni

Na Kassim Billo

HABARI za njaa wilayani Handeni zilithibitishwa na kiongozi mmoja wa kidini Sheih Mohamed Salimu ambaye alifika mjini Tanga kuomba misaada ya chakula kwa wafadhili na wahisani hivi karibuni.

Bwana Mohamed Salim aliwahi kuzungumza na mwandishi wa habari hizi na akamueleza shida ya njaa ambayo imeikumba wilaya ya Handeni akisema kuwa hali ni mbaya sana jambo ambalo limewafanya wananchi wa sehemu hiyo kuathirika vibaya hadi kula mizizi.

Alisema kuwa, tatizo la njaa limetokna na kuweko kwa ukame kwa muda mrefu na kwamba wakulima waliokuwa wameweka mbegu za mahindi ya kupanda wakati wa majira ya mvua, mahindi hayo ya mbegu wameyafanya chakula kwa ajili ya kukawia kwa mvua kunyesha kwa wakati maalum uliotazamiwa.

Hata hivyo, alisema kuwa hivi sasa mvua imeanza kunyesha lakini wakulima hawana mbegu za kupanda.

Alizidi kueleza kwamba japo serikali ilipeleka mbegu za mahindi katika sehemu hiyo hivi karibuni, lakini mbegu hizo za mahindi zilikuwa chache na hazikuweza kuwatosheleza wakulima wa sehemu hiyo ambao kila mwaka hulima zaidi ya ekari kumi na hata kumi na tano kwa kila mkulima.
 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook