Kufungwa kwa Benki ya Greenland:
 
Museveni kutembelea Misikiti kujieleza
Na Mwandishi Wetu

RAIS Yoweri Museveni wa Uganda amesema kwamba atakwenda Misikitini kuelezea ni kwanini serikali yake imeifunga Benki ya Greenland na kwamba hataifungua abadan.

Akihutubia Kamati ya Utendaji ya chama chake kinachotawala Uganda huko Jinja wiki iliyopita Rais Museveni amesema alipoamua Benki hiyo ifungwe baadhi ya watu wamedai kwamba kuna siasa.

Hivyo akasema kwamba ataitembelea Misikiti nchini Uganda kutoa ufafanuzi . Hata hivyo Rais Museveni hakutoa ufafanuzi nini maana ya kuwa na siasa katika jambo hili na kwanini awazungukie Waislamu Misikitini kutoa ufafanuzi badala ya kuwaeleza wananchi wa Uganda kwa ujumla.

Kwa mujibu wa taarifa za gazeti la serikali ya Uganda The New Vision Vol. 14 No. 83 la Aprili 12, 1999; katika mgogoro huu wa Benki ya Greenland, Rais Museveni amejiteua kuwa mshauri pekee wa wa Benki Kuu ya Uganda akiielekeza nini cha kufanya katika suala hilo la Greenland.

Wachunguzi wa mambo wameeleza kwamba hatua hii ya Museveni imekuja kufuatia shutuma za wananchi wa Uganda dhidi yake kwamba ameifunga Benki hiyo kwa chuki zake binafsi na sio kwa sababu zozote za kisheria au kitaalamu.

Wananchi wa Uganda wamekuwa wakielezea tukio la kufungwa kwa Benki ya Greenland na sababu zinazotolewa, sawa na tukio la Marekani kuipiga mabomu Sudan kwa kisingizio kwamba inatengeneza silaha za kemikali.

Serikali ya Museveni inaituhumu Benki ya Greenland kwa rushwa na usimamizi mbaya wa fedha ambapo Mwenyekiti na Mkurugenzi Mkuu wa Benki hiyo Dk. Suleiman Kiggundu alifunguliwa mashitaka na kuwekwa rumande katika gereza la Luzira.

Alipotoka rumande wiki hii, Dk. Suleiman I. Kiggundu aliongea na waandishi wa habari na kueleza kwamba amesikitishwa sana na kitendo cha serikali ya Uganda cha kuichafulia jina Benki ya Greenland.

Kinyume na ilivyotarajiwa Dk. Suleiman hakuonyesha kusikitika kukaa jela lakini ameleezea hisia zake katika kujiongezea shahada mpya aliyoiita P.G. (Prison Graduate) yaani mhitimu wa jela.

Dk. Suleiman amesema kwamba heshima yake ni kitu muhimu sana kwake na familia yake lakini pamoja na yote anayoifanyia nchi yake, yeye pamoja na Greenland wamepakwa matope bila ya kupewa fursa ya kujieleza/kujitetea.

Akionyesha jinsi haki isivyotendeka, Dk. Suleiman amewaeleza waandishi wa habari kwamba toka serikali ya Museveni ianze kuishutumu Benki yao kwa shutuma mbalimbali wamekuwa wakifanya kila juhudi kuiona serikali toka Julai 1998 ili kutoa maelezo yao, lakini wamenyimwa fursa hiyo.

Kuhusu madai kuwa Benki hiyo imetoa mikopo mikubwa sana kwa makampuni ambayo haiwezi kurejeshwa na hivyo kuhesabika kama hasara, Dk. Suleimani amesema kwamba habari hizo ni za kupotosha.

Ameyataja makampuni hayo kuwa ni FIBA Coffee ambalo ni la tatu kwa ukubwa katika makampuni yanayouza kahawa nchi za nje Uganda. Amesema kampuni hiyo huingiza dola milioni mbili (US$ 2 million) kila mwezi, kwa hiyo kuipa mkopo wa shilingi za Uganda 410 milioni haiwezi kuitwa mkopo wa hasara.

Aidha, ameitaja kampuni nyingine Uganda Grain Milling Company (UGMC) kwamba ni kampuni kubwa kifedha na yenye mali ya thamani ya shilingi za Uganda Bilioni 17, kwahiyo kuipa mkopo wa shilingi bilioni moja haijakiukwa taratibu za kibenki.

Alisema hali ni hiyo hiyo kwa makampuni mengine yaliyotajwa na serikali kwamba ni makampuni yenye dhamana za kuaminika.

Dk. Suleiman ameeleza kwamba inaonekana lengo la Benki Kuu ya Uganda kutangaza mikopo hiyo kwamba ni hasara kwa Benki ni kuwatia hofu wateja ambapo suala la msingi lingekuwa kuangalia kama mikopo hiyo inalipwa kwa mujibu wa taratibu zilizokubaliwa.

Dk. Suleiman Kiggundu amedai kuwa kwa muda wa miezi minne toka Benki Kuu ya Uganda ijichukulie mamlaka ya kuiendesha Greenland Bank imeiingizia hasara ya Ushs 32 Bilioni.

Ama nini cha kufanya hivi sasa Dk. Suleiman amesema wanafanya tathmini juu ya hali ilivyo katika makampuni yao ikiwemo Benki, FIBA Coffee, Kampala University, Sapoba Printers, Entebbe Resort Hotel n.k., kisha watafute fursa ya kuzungumza na serikali namna ya kuutatua mgogoro huu.

Amesema Benki ya Greenland ina wateja zaidi ya 120,000, wafanyakazi 400 ambapo makampuni tanzu ya Greenland Group yana wafanyakazi 2500.

Dk. Suleiman Kiggundu amewaomba waandishi wa habari wasaidie kueleza ukweli wa jambo hili.

Vyombo vya habari vya kanda hii ya Afrika ya Mashariki vimekuwa vikiripoti kwamba Benki ya Greenland ilikuwa na wateja wapatao 100,000 kwa Uganda peke yake na kwamba zaidi ya kuwa ni ya tatu kwa ukubwa nchini Uganda imekuwa Benki pekee ya wazawa iliyopata mafanikio makubwa zaidi kuliko Benki nyingine yoyote ya wazawa katika Afrika Mashariki yote.

Baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikieleza kwamba Rais Museveni amekuwa akiituhumu Benki hiyo kuwa na uhusiano na makampuni ya Sudan.

Wakati mwingine sio kuhusishwa tu na makampuni ya Sudan lakini imekuwa inadaiwa ni ya Waislamu. Na hivyo kujenga madai mengine kwamba inatumia uwezo wake wa kifedha kuwasaidia waasi wanaopigana na serikali ya Museveni.

Imedaiwa kwamba uhusiano wa Benki hiyo na Rais Museveni uliharibika zaidi pale Benki hiyo iliposita kushughulikia mzigo wa wapiganaji wa John Garang kwa vile serikali ya Museveni ilikuwa haijaulipia.

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook