KATIKA hali iliyotafsiriwa na wengi kuwa ni chuki ya baadhi ya watendaji wa vyombo vya dola dhidi ya Uislamu, Imamu wa Msikiti wa Chaurembo Mtoni Jijini, Jumatano wiki iliyopita alikamatwa na kuhojiwa kwa masaa kadhaa Kituo cha Polisi Kilwa Road kufuatia mahubiri yakikundi kimoja cha Kiislamu yaliyoandaliwa na Msikiti wake.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mmoja wa waumini wa Msikiti huo aliyefika ofisi za gazeti hili juzi (Jumatano), alisema Imamu wao Sheikh Abdallah Suleiman Fundi alichukuliwa na askari wa Kituo cha Polisi Mtoni majira ya saa 6:30 mchana wa siku hiyo.
Alisema wao walikuja kufahamu masaa kadhaa baada ya mkasa huo hali iliyowafanya watumie vipindi fulani vya swala kuhamasishana kufuatilia kujua kulikoni juu ya Imamu wao.
Akielezea kukamatwa kwa Imamu huyo, muumini huyo aliyejitambulisha kwa jina la Amani Mohammed alisema siku chache kabla ya tukio hilo Msikiti huo uliandaa mhadhara wa dini wa wazi uliowahusisha watu wa dini zote.
Bwana Amani alieleza kuwa taratibu zote za kisheria kuhusiana na mihadhara ya wazi ikiwa ni pamoja na kuomba kibali polisi zilifuatwa.
Alisema waliiandikia polisi kuomba kibali Machi 26, mwaka huu na kuruhusiwa kwa barua yenye Kumb. Na. TEM/C.13/4/Vol.1/317 ya Machi 30, 1999 iliyosainiwa na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Temeke Bwana Isaya Mngulu.
Hata hivyo, ameeleza muumini huyo kuwa ruhusa hiyo ya polisi iliandamana na sharti kuwa mhadhara huo ufanyikie siku mbili tu.
Bwana Amani ameeleza sharti lilitolewa na polisi lilipingwa na waumini wa eneo hilo kwa hoja kwamba iweje vikundi vya Wakristo viruhusiwe kufanya mihadhara mahali hapo kwa siku 20 mfululizo, Waislamu wapewe siku mbili tu.
"Huo ulikuwa upendeleo wa wazi kabisa kufanywa na vyombo cha dola ambayo katiba yake inaeleza wazi kuwa raia wote ni sawa na wanastahiki haki zote za kimsingi bila ya kubaguliwa", alidai muumini huyo.
Kwa sababu hiyo, Bwana Amani alisema kuwa waumini wa eneo hilo waliendelea na mhadhara tangu Machi 30 hadi Aprili 15 mwaka huu ambapo walifanikiwa kuwasilimisha watu kadhaa waliokuwa waumini wa madhehebu mengine.
Kufuatia hali hiyo, polisi kituo cha Mtoni Sabasaba wakiongozwa na Mkuu wa Kituo hicho Surgent Lucy waliamua kumsaka na hatimaye kumkamata Imamu wa Msikiti wa Chaurembo Sheikh Abdallah Suleiman Fundi (62).
Siku chache kabla ya mhadhara huo wa Waislamu, Wakristo wa dhehebu la Assemblies of God walifanya mhadhara katika uwanja huo kuanzia Februari 28 hadi Machi 8, mwaka huu.
Baada ya kumalizika mhadhara huo, mtu mmoja anayejiita Simbaulanga anayesemekana kuwa muumini wa dini ya Kikristo kwa kushirikiana na wafusi wake waliendesha mahubiri mahali hapo hapo kuanzia Machi 9 hadi Machi 21 mwaka huu.
Wakati huo huo, mwandishi wetu kutoka Tabora anaripoti kwamba Waislamu 15 waliokamatwa katika mhadhara wa kidini wilayani Nzega wameendelea kusota rumande kwa masiku kadhaa sasa.
Dhamana kwa ajili ya watu hao ilikataliwa kwa madai kwamba amani bado haijarejea wilayani humo na kwamba baadhi ya watuhumiwa bado hawajakamatwa.
Waislamu hao wanatuhumiwa kutoa kashfa katika mahubiri yao dhidi ya watu wa dini nyingine. Watafikishwa tena mahakamani Aprili 27 mwaka huu.
|
|