Na Mwandishi Wetu
FAMILIA za wanaodaiwa kufukiwa Bulyanhulu Kakola - Kahama wameiomba serikali iwapeleke wakaishi kwenye kambi za wakimbizi, kwani wapo katika dhiki iliyokithiri.
Akina mama wanaodai waume zao walifukiwa wakiwa hai, wamedai kwamba wanaoishi katika makambi hayo ni kama walioko mbinguni ikilinganishwa na hali yao wananchi waliojipanga juani kutwa kuiingiza serikali madarakani kwa njia ya kura.
Katika barua yao ya wazi kwa Mh. Rais Mkapa, akinamama hao wameeleza kiini cha dhiki inayowakabili kwamba ni kufukiwa machimbo ya Bulyanhulu ambapo waume zao (baadhi) walifukiwa wakiwa hai.
Wamesema kwamba awali waume zao na vijana wao walikuwa wakipata riziki kutokana na machimbo hayo. Lakini machimbo yaliuzwa kwa kampuni ya Canada.
Wamedai kuwa katika kuwakufukuza, waliokuwepo mashimo yao yalifukiwa bila tahadhari yoyote ambapo waume zao na vijana wao walifukiwa. Aidha wamedai kwamba nyumba zao zilibomolewa na kwamba toka wakati huo wanaishi maisha ya dhiki sana. Hawajapewa mahema wala chakula. Wameielezea dhiki yao kwamba imewafikisha kukosa hata ile hamu ya kuishi. Japo mvua ni faraja, lakini kwao wamedai itakuwa janga lingine baada ya njaa kwani hawana makazi.
Katika kilio chao hicho wamedai kuwa hata ardhi ya kijiji ambapo walikuwa wakiitumia kwa kilimo japo kidogo imezuiwa na kampuni ingawaje haina kazi nayo.
Akina mama hao ambao nakala ya barua ya malalamiko yao imetumwa kwenye vyombo vya habari wamemkumbusha Mh. Rais ahadi yake wakati wa kampeni 1995 kwamba angewasaidia katika mgogoro wa machimbo hayo.
"Tulishangaa sana na tutaendelea kufanya hivyo tulipoona badala ya wewe kuunga mkono haki...; inaonekana kinyume chake na inaonekana umeshasahau ahadi yako uliotuahidi sisi wananchi wanyonge", wamelalamika wananchi hao.
Mwaka 1997 wamedai kwamba walisikia katika vyombo vya habari kwamba serikali ya Canada ilitoa msaada wa fedha kiasi cha dola milioni mbili na laki tano (USD 2,500,000) ili wapatiwe chakula njaa isiwamalize.
Hata hivyo, wamemfahamisha Mh. Rais kwamba msaada huo mpaka leo haujawafikia na kwamba wanalisema hili ili Mh. Rais asije danganywa.
Aidha, wamedai kwamba ahadi ambayo walikuwa wamepewa ya kulipwa mali zao zilizoharibiwa pamoja na fidia za watoto na waume zao waliofukiwa wakiwa hai imekuwa ahadi hewa.
Katika mgogoro wa Bulyahulu pamoja na madai ya wananchi na vyombo vya habari kwamba wapo watu waliofukiwa wakiwa hai katika operesheni ya kuwafukuza wachimbaji wadogo wadogo; serikali imekuwa ikikanusha madai hayo.
Hivi karibuni Mh. John Cheyo ameripotiwa akidai kwamba ameshaandaa taratibu za kuishitaki serikali juu ya mauaji hayo.
|
|