Na Abu Halima Sa Changwa
SIKU moja nilikuwa nje ya nyumba ninayoishi, ambapo niliona watoto wadogo wakicheza. Watoto hawa walikuwa wakifukuzana huku na kule wakifurahia wakati wao wa utoto. Lakini mara kukazuka ugomvi mkubwa miongoni mwao. Zogo lilikuwa kubwa na mchezo uliharibika. Kwa vile ninapenda somo la Saikolojia, nilipenda kufanya kauchunguzi kadogo kufuatana na mwenendo wa watoto wale. Niliwauliza ni nini kilikuwa chanzo cha ugomvi wao, mmojawapo akatoa maelezo ya upande wake kwa hasira kabisa, akisema kwamba, walikuwa wanacheza mchezo wa kufukuzana. Katika mchezo ule, mmoja wao alikuwa akijifanya ni mbwa, na alikuwa anawafukuza wenzake. Sasa yule kijana aliyekuwa anaelezea alikuwa analalamika kwamba ilikuwa ni zamu yake yeye kuwa mbwa, awafukuze wenzake, lakini wenzake walikuwa wanamdhulumu.
Nilielewa kwamba chanzo cha ugomvi ule ni kwamba kila mmoja alikuwa anagombania kuwa "mbwa" awafukuze wenzake. Kwa hiyo, katika mchezo wao, nafasi iliyokuwa na raha sana, kila mmoja alikuwa anataka aipate ni ya kuwa "mbwa". Watu wachache waliopita pale na kusikia habari zile, kwamba kila mmoja alikuwa anagombania kuwa "mbwa", walicheka tu na kusema: "Ah, utoto bwana!"
Hiyo ni athari ya kisaikolojia katika akili ya kitoto. Watoto wanaweza tu kufurahia kitu cha kijinga, na wakaona hakuna raha duniani kama kufanya kitu hicho.
Lakini, je, kama huu tunaita utoto, mtu mzima naye anapoona raha kufanya jambo la hovyo, tutamwitaje? Pengine yapo majina mengi. Nililozoea kulisikia ni "limbukeni".
Hebu tuchukua mfano wa watu wazima kuona raha kuwa "mbwa". Hakuna asiyejua ubaya wa pombe. Mtu yeyote mwenye akili timamu duniani anajua pombe ni mbaya, kwa vile yenyewe ni ulevi. Ulevi humtoa mtu kwenye hali ya akili na kumuweka kwenye hali ya kutokuwa na akili. Tunafahamu pia kuwa tofauti iliyopo kati ya wanyama na binadamu ni kwamba binadamu ana akili. Sasa mtu anapofurahia ulevi, au unapoona raha kutokwa na akili, ana tofauti gani na wale watoto walioona raha kuwa mbwa? Au kama wale watu walivyocheka na kusema: "Ah! Utoto bwana!" Basi na sisi tuseme; "Ah! Ulevi bwana!?"
Utoto hauna athari kwenye jamii yetu, unaishia kule kule michezoni, lakini ulimbukeni una athari, na athari yake inaonekana na wenye macho na akili. Unaweza ukatafuta chanzo cha matatizo ya nchi, kwamba mipango yote haitengemai, lakini mipango itatengemaa vipi wakati mikutano mikubwa ya kupanga mikakati ya nchi huwa haifani mpaka watu wawe wamelewa, yaani wawe hawana akili?
Walevi wengi husema ulevi huwasaidia kusahau matatizo, nadhani ndio maana matatizo ya wananchi hayaishi kwa sababu wanaotakiwa kuyatatua kila siku wanayasahau kwa ulevi. Tutafika! Na hivi ndio viwanda vinazidi, bado watu wanavumbua "dhahabu", na nchi imekumbwa na balaa la watu kuona ufahari kutokuwa na akili. Kila mmoja anataka kuwa "mbwa", isipokuwa Waislamu na walokole wachache.
Watu wenye akili huwa wanatahadhari kuwapa amana binadamu wenye kichaa cha kutamani au kufurahia kuwa mbwa, yaani kuona raha wakiwa hawana akili, kwa hiyo huwa hawawapi amana zao. Je, kuna amana kubwa kama uongozi? Na je, amana hiyo hatujawapa watu wa aina hiyo? Au na sisi tunafurahia kuona raha kuongozwa na watu wanaoona raha kutokuwa na akili? Nauliza hivi kwa sababu Mtume Muhammad (s.a.w.) alisema hivi:
"Kama takuunu, yuwalla 'alaykum". Kama mlivyo ndivyo mtakavyotawaliwa, kwa maana kwamba wenye akili huongozwa na wehu. Wazungu wana methali yao inasema: "Where ignorance is a blessing, it is folly to be wise". Yaani "Mahala ambapo ujinga huonekana ni baraka, basi ni ujinga kuwa mwerevu". Labda ndio maana tunaona kuongezeka kwa idadi ya viwanda vya ulevi na vibanda vya pombe ni kawaida tu, ndio maana tumekaa kimyaa.
Mimi kama mwanasaikolojia nasema tu, dawa ya maradhi haya hakuna, ila ni Uislamu, ambao hauruhusu mtu awe na hadhi ya mnyama, ya kutokuwa na akili (kwa makusudi), hata kwa sekunde moja tu. Ndio maana Waislamu hawaruhusiwi hata kuonja. Hivyo ili nchi iendelee, inahitaji watu ambao saa zote wana akili zao, na ili nchi iwe na watu wenye akili zao saa zote, inahitaji Uislamu.
|
|