Katika tukio la kihistoria...
Wafungwa Moro wachanganyika na kusali Idd
  Musa Ally na Abu Faiza Suleiman, Morogoro

KATIKA tukio lisilo la kawaida na la kihistoria, wafungwa wa Magereza matatu ya Morogoro wamechanganyika na Waislamu raia mapema hivi karibuni kutekeleza ibada ya swala ya Idd el- Hajj kwenye Msikiti wa Gereza la Mtego wa Simba.

Wakiongozwa na Imamu wa Msikiti huo ambaye ni askari wa gereza la Mtego wa Simba Bw. Juma Lipala wafungwa hao wasiopungua 100 toka gereza la Mtego wa Simba, Mkono wa Mara na gereza la wanawake walijumuika katika Msikiti huo mpya wakiwa ndani ya mavazi marefu (wanaume) na hijabu wanawake.

Naye Mwalimu wa Madrasa ya gereza la Mtego wa Simba, Sheikh Omar aliwanasihi wafungwa hao kuwa wavumilivu na kujikurubisha mno kwa Mwenyezi Mungu, pamoja na kujipinda katika mafundisho ya dini yao.

Katika tukio jingine, shirika la Kiislamu lenye makao yake mjini hapa (Morogoro Islamic Foundation) ambalo hutoa misaada magerezani liliombwa kutosita kusaidia ndugu zao katika imani (wafungwa Waislamu) mara wahitajiapo msaada.

Akiongea kwa niaba ya jeshi la Magereza, Ofisini kwake wakati akipokea swadaka ya nyama kwa wafungwa, Mkuu wa Gereza la Mtego wa Simba Kamanda Ruvuga alisema kwamba misaada ya Islamic Foundation katika magereza hayo ni ya kupigiwa mfano wa kuigwa kwa taasisi nyingine na watu binafsi.

Mwisho Kamanda huyo aliwaomba Waislamu kuwasaidia wale wote walioko vifungoni hasa madawa, sabuni na mavazi ya kufanyia Ibada.
 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook