DODOSO LA KUTAFAKARI
 
Mdahalo wa kuhamisha mada

Na Kipondo wa Changarawe
 

NI maajabu na kweli kwamba ukweli una nguvu na mvuto wa ajabu; Ukweli unapokutana na uongo, uongo hutetemeka, kugwaya na hatimaye kutoweka na kupotea kabisa. Si miujiza, bali ukweli ndio kawaida yake kwamba haushindwi mbele ya uongo. Ni jambo lililodhahiri kwamba ukweli una nguvu kwa kuwa umo ndani ya haki, na uongo ni dhaifu sana kwa sababu umejichimbia kwenye batili.

Ukweli na haki ni kama pande mbili za sarafu moja ambazo huwa ni vigumu sana kuvitenganisha. Daima ukweli hauhitaji nguvu ya kulazimisha wala propaganda na mashinikizo ili uwe kujulikana kwenye mabongo ya vichwa wasiokuwa na chuki, inda na husuda. Vinginevyo mtu awe labda ana mtindio wa ubongo ama yule mwenye akili za kushikiwa. Ukweli hautegemei kupambwa pambwa ili uweze kukubalika, bali ni kutokana na nguvu zake za asili, ukweli una mvuto unaoufanya ujitegemee na kusimama imara bila kuteteleka. Ni muhali na haijatokea ukweli ukazidiwa nguvu na uongo. Hata mara moja nasema haijatokea!

Kinyume chake uongo na batili vinahitaji mtu agharimike sana ili angalau aweze kuvifanya vionekane kama vinafanana na ukweli na haki. Vinahitaji mamilioni ya mapesa, wapambe, kutumia maguvu na mashinikizo, mauaji na kulazimisha. Pamoja na yote hayo, ili viweze kufanikiwa japo kwa muda basi inalazimu wakweli wote waliopo duniani wabanwe na wasiweze kupumua, na midomo yao ifungwe ili ukweli usipate hata upenyo wa kujitokeza kwenye jamii. Kwa kweli uongo unapopambanishwa na haki hauna ubavu wa kufurukuta si kuambii kushinda. Maana hata kama haki na ukweli vimefungiwa, bado uongo hauwezi kusimama kwa kuitumia miguu yake. Ni ukweli kwamba ukweli ni kiboko cha uongo wowote ule uliojichimbia ndani ya batili.

Madhalimu wasiotenda haki daima wanauogopa ukweli usijitokeze ukaja kuwaweka wazi wakajulikana katika jamii kuwa wao ni wanyonyaji na wababaishaji. Wanaogopa ukweli kama wanavyoyaogopa na kuyachukia mauti ambayo yanakata starehe zao na kuwafanya wasahaulike katika uso wa dunia. Lakini inawawia vigumu na imekuwa ni bahati ambayo kwa upande wao kuwa pamoja na jitihada zao kubwa wanazozifanya dhidi ya ukweli, hawawezi kamwe kuudhibiti usijitokeze kama wanavyoshindwa kuyazuia mauti yasikate tamu ya maraha wayapatayo kwa njia ya dhulma. Ukweli unawatishia maisha wale wote wasiopenda haki na uadilifu, unawafanya waishi maisha ya kutaabika na wasiwasi hata kama wamo katika ngome na 'mahekalu' yao.

Wamo kwenye wasiwasi mkubwa kiasi ambacho vyote vile vya kuwaliwaza havitoshi kuwaondoa wasiwasi. Wanajua kwamba wakati wowote ule ukweli utawaumbua. Wanawanunua na kuwafuga wapambe ili wawapambe kwa sifa nzuri nzuri zisizostahiki eti waonekane kuwa batili, dhulma na uongo wanaojipamba nao ugeuke kuwa haki, uadilifu na ukweli. Lakini wapi! Ukweli unazitafuna ghiliba zao kama moto unavyokula kuni. Ukweli unawatisha kama njaa. Maana mtu abobee kiasi atakachoweza na awe hodari asiyekuwa na mpinzani katika fani ya kuwazuga watu, apate sura ya kuzieneza propaganda zake kwa muda mrefu; ukweli huwa ni kiboko yake na haumkopeshi kabisa, huyageuza yale yote ya kuzuga aliyoyapandikiza vichwani mwa watu kwa kipindi cha muda mrefu kuwa ni mchezo na mavumbi.

Kuwa kipanga utakavyokuwa katika kuzuga zuga watu, elewa kuwa siku utakakutana na ukweli umekwisha. Katika hali yoyote ile ukweli unapodhihiri huwa haupingiki zaidi ya kumfanyia hila yule aliyeuwasilisha. Na kinachonyongesha zaidi ni pale ukweli unapomfanya dhalimu agundulike kuwa ni yeye hasa aliye adui wa maendeleo ya jamii pamoja na haki za watu. Siyo kama Kipondo ameamua tu kupamba maneno bali huu ndiyo ukweli kuhusu ukweli ambao madhalimu na wababaishaji wanauchukia na kuuogopa. Na kwa kuwa kuna watu ambao vinywa vyao na mwenendo wao vinauwakilisha ukweli, hao wamekuwa ni watu wa kuandamwa na kusakwa kila siku ili wakitaka watokomezwe.

Ukiwa na wasiwasi na mashaka, tulia dodoso lianze kukuvutia mafaili yatakayokuthibitishia namna ukweli ulivyo na nguvu na mvuto wa ajabu. Kisha dodoso litakupeleka kwenye bustani ya Qur'an iliyo na chemechem ambayo ni dawa ya kuyatibu magonjwa makubwa yote yanayoikabili jamii ya wanadamu kuanzia magonjwa makubwa yanayozaa mengine na yale magonjwa yanayozaliwa. Huko tutaona jinsi ukweli ulivyoshinda katika midahalo mbalimbali pamoja na hatua walizochukua madhalimu na wababaishaji baada ya kushindwa kukabiliana na haki.

Kabla ya miaka ya kuanzia thamanini na nne, walijitokeza watu wakarimu waliowahurumia sana Waislamu wasipotee na kuishia kuzimu. Wakafanya jitihada kubwa za kutaka kuwaokoa Waislamu, wakapita nyumba hadi nyumba ya Muislamu kwa kadri walivyoweza na kuwataka Waislamu wasafishwe madhambi yao kwa kukiamini kile "Kifo" ambacho damu iliyomwagika ndiyo utakaso. Wakatengeneza fursa pamoja na kuzitumia zile fursa zilizokuwepo, wakatuita kwenye viwanja vya wazi, wakatupitia mahospitalini na wengine wakatufikia mashuleni na kutugawia akina Kipondo neno la Mungu ili tukajisomee tukiwa nyumbani ikiwezekana kuwaelimisha wazee wetu.

Bahati nzuri iliwadondokea, yakajengwa mazingira ambayo yangerahisha kutuvuna kirahisi zaidi. Maguruwe yakafugwa mashuleni ikiwa ni hatua muhimu ya kutuandaa kwa kutupatia elimu ya kujitegemea ili kutuivisha tuweze kuwa viongozi bora wa siasa ya ujamaa na kujitegemea. Vile vile mazingira yakafanywa kuwa magumu kwa wanafunzi wa Kiislamu kufuata mila na utamaduni wa dini yao. Kuswali kwa mbinde na kuvaa mavazi ya Kiislamu ni kwenye ndoto. Pamoja na mazingira kuwa munasibu kwao mavuno yalikuwa madogo sana.

Walijitokeza akina marehemu Ngariba pamoja na wale wanaofuata nyayo zao wakiwa na hoja madhubuti na za kweli zilizosimama katika haki na ukweli. Wao hawakuhitaji wajengewe mazingira magumu ili wapate kuwakirimu watu na kuwarejesha kwenye Uislamu. Wao ni kiasi cha kukamata kipaza sauti na kueleza ukweli. Basi hapo utawaona wakijisogeza wenyewe katika meza na kuanza kuuliza maswali na haki inapowabainikia hurejea kwa hiari yao katika dini ya haki. Basi tunavuna tu makumi kwa mamia warejea kwenye dini ya kimaumbile, utaratibu wa haki na uadilifu.

Ama kweli ukweli unaposimama uongo unapiga mbio na hatimaye kutoweka. Kwa kuwa ukweli haupingiki. Siku zote wale ambao ni wababaishaji na wale walio madhalimu ukweli unapowazidi nguvu wanaanza kupanga hila dhidi ya wale wanaosema ukweli. Wao huwa wanahamisha mada ya madahalo ili wapate kukwepa na kuufifiza ukweli. Wanaweza kujenga hoja kuwa kuna watu wanatukana dini za wengine, mara kuna watu wanakashifu dini, kuna watu wanatumiwa kuvuruga amani kwa kupitia dini, kuna watu wenye siasa kali, msimamo mkali, imani kali n.k.

Wanapokutanishwa pande zote mbili na kutakiwa waonyeshe ili kuthibitisha kuwa ni maneno gani yanayokashifu, wao wanagwaya na kutetema kana kwamba wamemwagiwa maji ya baridi. Haya basi nendeni mahakamani ili ukafungue mashitaka! Wanapata kigugumizi cha miguu. Watasema nini mahakamani. Watasema nini na kutoa hoja gani ili kuufanya ukweli uwe uongo. Ama kweli ukweli ni kiboko cha wababaishaji. Katu ukweli hautazidiwa nguvu hata uongo ukikaririwa masikioni mwa watu kwa miaka mingi.

Kama inavyojitokeza katika kichwa cha maudhui ya dodoso, kwamba madhalimu na wababaishaji ni kawaida yao kutafuta mahali pa kutokea pale ukweli unapowabana wakati wao hawako tayari kutenda haki. Kwa hila wanazua mada nyingine ili kupoteza lengo na kuwaandama wale wanaosema ukweli, ambao huamsha watu kutoka usingizini na kuwafumbua macho yaone dhuluma ifanywayo na wababaishaji. Utawaona madhalimu wanahaha kutwa kucha wakifanya jitihada za kuufifisha ukweli ili dhuluma na uzushi wao vichukue nafasi ya haki na ukweli. Kadri siku zinavyopinduka ndivyo ukweli wa Uislamu unavyowadhihirikia walimwengu kuwa hakuna mfumo wa maisha uliobora wenye hakika na uadilifu, uletao furaha na amani ya kweli kuliko Uislamu.

Tazama jinsi Waislamu wanavyopachikwa majina mabaya ili waonekane kuwa watu wasiofaa na ni kinyaa katika jamii. Siku hizi kuna mapicha maalumu ya sinema yanayochezwa kiufundi na waigizaji walio mahodari ili kuwafunza walimwengu kuwa Waislamu wanajenga maadili mema katika jamii na kuleta haki na uadilifu katika uchumi, siasa na ustawi wa jamii kuwa ni watu hatari wanaofanya vitendo vya kigaidi na kuwauwa wasiokuwa Waislamu. Marundo ya mabuku yaliyojaa kurasa zinazozungumzia Uislamu visivyo yameandikwa na kusambazwa karibuni kila kona ya dunia.

Katika nchi za huku kwetu utakuta kwa makusudi kabisa yaliyo kinyume na ukweli, Uislamu unanasibishwa na biashara ya utumwa wakati inajulikana wazi kuwa walioanzisha , walionufaika na walioipiga marufuku ni wale wale waliousimika ukoloni kupitia Wamisionari wa Kikristo, wapelelezi (Wakristo) na makampuni yao ya kibiashara. Nilibahatika kukipitia kitabu kimoja cha historia kilichoandikwa na Bwana mmoja aliyekuwa mwanafunzi wa Peramiho Seminaries huko Ruvuma. Kilichonishangaza ni kwamba zile nukta zinazoonyesha unyama wa Wajerumani Wakristo ambazo zina ushahidi wa kihistoria kama vile namna walivyowatundika na kuwanyonga katika "Mwembe kunyonga" hazifafanuliwi, badala yake zinashadidiwa nukta kuwa Maakida na Majumbe ambao wengi wao ni 'Waarabu' walikuwa wakatili sana.

Yote haya yanafanyika kwa kuhamisha mada ya mdahalo ili ielekee kwingine na kuonyesha kuwa Waislamu ni watu wabaya sana wakati wale madhalimu wanawanyonga Waislamu wanaopigania haki na uadilifu kama vile walivyonyongwa akina Abushir bin Salim, Bwana Kheri na Hassan bin Omar Makunganya katika mwembe kunyonga; na hivi majuzi mauaji ya Waislamu yaliyofanywa Mwembe Chai.

Imekuwa ni faraja kwa Waislamu. Maana kadri wanavyokandamizwa ili wasifurukute ndivyo ukweli wa utaratibu wa maisha wa haki wa Kiislamu unavyojitokeza kupitia kijisehemu kidogo lakini kwa nguvu na kasi ambayo madhalimu na wababaishaji inawaumiza vichwa na wanashindwa namna ya kuzuia. Maguvu, vitisho na wakati mwingine umwagaji wa damu za Waislamu unafanywa hadharani kama ilivyokuwa Mwembe Chai.

Mfano wake imekuwa kama kutumia muda, nguvu, mapesa pamoja na hazina ya akili katika kuhangaika kuuzima moto unaowatekekeza wadudu waharibifu kwa kutumia petroli. Maana dodoso linaona kuwa ule unyama uliofanywa na polisi wa serikali ya chama tawala pale Mwembe Chai unadhihirisha ukweli kwamba nchini Tanzania, damu na uhai wa Muislamu si lolote si chochote ni kama vile kumuua sisimizi wakati wa kutembea.

Kwa muda mrefu istilahi za "siaka kali, wachochezi wachache, wanaotumika kuvuruga amani" zimekuwa zikitumika kuwapachika Waislamu wanaotoa mahubiri pamoja na wale wanaosimama kidete katika kudai haki za Waislamu zinazostahiki kupewa kama wanavyostahiki raia wengine. Kwa nembo ya 'siasa kali' na 'mihadhara ya kashfa' Waislamu wa Morogoro wakiwa Msikitini walivamiwa, wakashambuliwa kwa mabomu na kupewa kipigo, hatimaye wakafunguliwa mashitaka yasiyo na kichwa wala miguu.

Mambo yakawa yameiva! Tamko la Paroko likawaingiza viongozi wa jeshi la polisi kuwasaka na kuwakamata Waislamu na Masheikh wao pamoja na wahadhiri. Wakawaua Waislamu kwa kuwatungua kwa risasi. Wimbo ukawa ni ule ule, 'waliokamatwa ni siasa kali', 'waliouliwa ni siasa kali', 'waliosababisha vurugu ni siasa kali'.

Siku moja tu Sheikh Ponda Issa Ponda akaongea na waandishi wa habari. Kwa kuwa alichokisema ni ukweli, basi ukazigeuza propaganda zote kuwa 'utumbo'. Waheshimiwa wakahamaki na kubadilisha mada, ikawa Sheikh Ponda ndiye mchochezi wakati Paroko na vijana wake wanaachwa.

Cha kushangaza zaidi ni pale Mh. KK alipoeleza bungeni kuhusu ukweli wa dhulma wanayofanyiwa Waislamu dhidi ya haki zao za kimsingi wakiwa ni miongoni mwa raia wa nchi. Mada ikabadilishwa kutoka kwa Waislamu kudai haki zao badala yake ikaingizwa mada ya unyeti. Hapo ikatolewa mifano ya kuwalinganisha na watu wanaoishi maporini. Ni mifano isiyowiana na mada (Irrelavant and fake analogy). Kama haukutolewa kwa kuwachukia Waislamu (Prijudice) basi ni mifano inayokaribia kuwa ya kijazba.

Mtindo wa kuhamisha mada katika mdahalo na kuanzisha mada iliyo kinyume ili kukwepa ukweli haukuanza leo. Katika midahalo yote iliyofanywa baina ya haki na batili, ukweli unapodhihiri, madhalimu na wababaishaji wanabadilisha mada ili kuufifiza ukweli. Ukizitafakari aya zifuatazo utagundua:

"Nendeni kwa Firauni, bila shaka amepindukia mipaka. Kamwambieni maneno laini huwenda akashika muidha au ataogopa. Basi mwendeeni na mwambieni, kwa yakini sisi ni Mitume wa Mola wako. Basi waachie wana wa Israili watoke pamoja nasi na wala usiwaadhibu. Hakika tumekuletea ishara kutoka kwa Mola wako. Na amani itakuwa juu ya wale wanaofuata uwongofu. Na hakika tulimuonyesha (Firauni) ishara zetu zote. Lakini alikadhibisha na akakataa. Akasema; Umekuja kututoa katika nchi yetu kwa uchawi wako, ewe Musa? (20:43, 44, 47, 56, 57)

Wakasema: Nani aliyeifanya hivi miungu yetu? Hakika huyo yu miongoni mwa madhalimu. Wakasema: Tulimsikia kijana mmoja akiwataja vibaya anayeitwa Ibrahimu. Wakasema: Basi mlete mbele ya macho ya watu, wamshuhudie. Wakasema: Je; wewe umeifanya hvi miungu yetu, ee Ibrahimu? Akasema: Siyo, bali amefanya huyu mkubwa wao, basi muulizeni kama anaweza kusema. Kisha wakainamisha vichwa vyao (wakasema)Hakika umekwishajua ya kwamba hawasemi. Wakasema: Mteketezeni kwa moto na muinusuru miungu yenu, ikiwa ninyi watenda jambo. Na walimtakia ubaya, lakini tukawafanya wao ndio wenye kupata hasara. (21:51-73)

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook