WATU MAARUFU
 
Malcolm X (Alhaj Malik Al Shabbaz): Mwanaharakati aliyepigania usawa kwa watu wa rangi zote
 

Al Hajj Malik Shabbaz, maarufu kama Malcolm X, alikuwa Mmarekani mwenye asili ya Kiafrika ambaye alijotelea maisha yake katika kupigania haki sawa kwa watu wa rangi zote katika Amerika na ulimwenguni kote. Alipata kujiita na kujulikana kama 'The angriest man in America' yaani mwenye hasira kushinda wote Marekani. Harakati zake na maisha yake ni kichocheo kwa wengine wanaopigania usawa ulimwenguni kote na Waislamu wa Tanzania wakiwemo. Katika makala Makala hii ambayo chanzo chake ni kijitabu cha "Malcolm X: Kwa nini niliingia Uislamu" na Yusuf Siddiqui, yametolewa maelezo kwa kifupi juu ya historia ya harakati zake, kujiunga kwake na dhehebu lililojiita Taifa la Kiislamu ambapo Uislamu ulifundishwa kwamba ni dini ya mtu mweusi na Elijjah Muhammad ni mtume wake na mwishowe kifo chake miaka michache baada ya kurejea Uislamu wa kweli ambao ameuelezea kwamba unatoa suluhisho la ubaguzi wa rangi katika jamiiubaguzi ambao "unaielekeza Amerika katika njia ya kifo". Nukulu zote zimetolewa toka katika kitabu "The Autobiography of Malcolm X" kama kama alivyomsimulia mwandishi Alex Haley.

Malcolm X: Historia yake kwa ufupi:-

May 19, 1925 - Alizaliwa Omaha, Nebraska, USA na kupewa jina Malcolm Little.
Mwaka 1940 - Aliacha shule akiwa na miaka 15.
Mwaka 1946 - Alipatikana na hatia ya uvunjaji nyumba na kufungwa jela.
1949 - 1951 - Akiwa jela ajiunga na kupata mafundisho ya Taifa la Kiislam.
1952 - Atoka jela, na kujiunga rasmi na Taifa la Kiislamu, abadili jina kuwa Malcolm X.
Jan.14, 1958 - Amuoa Betty X
Dec. 4, 1963 - Asimamishwa Taifa la Kiislam.
March, 1964 - Aondoka rasmi Taifa la Kiislamu na kuanzisha msikiti wake aliouita Muslim Mosque, Inc.
April 22,1964- Afanya Hija na kuwa Al-Haji Malik al-Shabazz
June 28, 1996- Aanzisha umoja wa Wamarekani weusi (Organisation of Afro- American Unity).
July 17, 1964 -Apata nafasi ya kuzungumza katika mkutano wa OAU, Cairo.
Aug. 13, 1964- Ikulu ya Marekani na Idara ya sheria ya huko wagundua jinsi alivyowaathiri viongozi wa nchi za Afrika     katika Umoja wa Mataifa.
Feb. 21, 1965- Al Hajj Malik auawa New York.

Maisha yake ya Mwanzo

Mnamo Mei 19, 1925 huko Omaha, Nebraska, USA Malcolm Little alizaliwa na Mchungaji Earl Little na mkewe Louise. Mchungaji Little alikuwa ni mpiganiaji wa uhuru wa mawazo na umoja wa watu weusi. Malcolm alikulia katika mazingira ambapo watu walijigawa katika makundi yenye kuhusiana na rangi zao na weusi wakipigania heshima zao. Lakini vurugu zilienezwa na wabaguzi wa rangi wazungu, waliojaribu kuwanyamazisha watu weusi kama Mchungaji Little wasihubiri harakati za kudai uhuru na usawa kwa mtu mweusi.

Historia ya Malcolm juu ya mapenzi yake na mvuto wa kupigania haki za watu weusi, huenda zilichochewa na historiandefu ya uonevu dhidi ya familia yake. Akiwa mtoto mdogo, Malcolm na wazazi wake, kaka zake pamoja na dada zake walirushiwa risasi, wakachomewa nyumba moto, kusumbuliwa na kupewa vitisho dhidi yao. Hii ilifikia kilele chake baada ya kuuawa kwa baba yake na wabaguzi wa rangi Wazungu wakati Malcolm alipofikia umri wa miaka sita tu.

Malcolm akaacha shule katika umri wa miaka 15 licha ya kwamba alikuwa akiongoza darasani. Mwalimu wake Mzungu alimkatisha tamaa kwamba kwa kuwa yeye ni mweusi basi aache ndoto zake za kuwa mwanasheria na kujiandaa kuwa fundi seremala. Kauli hii ilimuudhi Malcolm X na akaamua kuacha shule.

Baadaye akajifunza mbinu za mitaani na Malcolm akajiingiza kwenye makundi ya wahuni, wezi, wauza madawa ya kulevya na kushawishi wanawake kwenye biashara za ufuska. Alipatikana na hatia ya uvunjaji nyumba katika umri wa miaka 20 na kukaa jela hadi alipotimiza umri wa miaka 27. Katika maisha yake ya jela alijitahidi kujielimisha. Zaidi ya hayo, katika kipindi alichokaa jela alijifunza na kisha kujiunga na Taifa la Kiislam, akijifunza mafundisho ya Elijah Muhammad kwa ujumla wake. Aliachiwa akiwa mtu aliyebadilika kabisa mwaka 1952.

Taifa la Kiislam

Mara tu alipoachiwa, Malcolm X alikwenda Detroit, akajiunga na kufanya shughuli za kila siku za dhehebu hili, na alipewa amri na maelekezo ya moja kwa moja toka kwa Elijah Muhammad. Jitihada za Malcolm X zilisaidia kulijenga Taifa la Kiislam nchini kote na kisha kumfanya mtu aliyejulikana kimataifa. Alifanyiwa mahojiano katika vipindi vya Televisheni na magazeti, akiongea katika vyuo vikuu mbalimbali na sehemu nyinginezo. Nguvu yake ilikuwa katika maneno yake, ambayo kwa uwazi na ufasaha mkubwa aliongelea hali ya mtu mweusi katika Amerika na kwa ukali akieleza ubaya na makosa ya wazungu. Na hata mzungu mmoja aliporejea katika ukweli kwamba katika chuo kikuu kimoja cha kusini mwa Marekani waliandikishwa wanafunzi weusi bila kutumia visu (akimaanishabila kutumia nguvu), Malcolm X alijibu kwa uchungu:

Na 'nilipoteleza' katika mahojiano ya televisheni, basi mtangazaji aliingia katika mtego wangu (aliingia kwenye ndoano yenye chambo) na kudai, "Ahhh! Hakika, Bwana Malcolm X huwezi kukanusha kwamba haya ni maendeleo kwa watu wenye rangi kama yako (kwamba na wao wameruhusiwa kujiunga na Vyuo Vikuu!)"

Kisha nilitikisa kidogo mti ulioshika hiyo ndoano yenye chambo na kusema "Siwezi kugeuka upande wowote bila kusikia kuhusu 'maendeleo ya haki sawa kwa watu wa rangi zote'. Wazungu wanaonekana kudhani kwamba watu weusi watashangilia kauli zao kama hizi na kupiga kelele za 'halleluyah'! Kwa muda wa miaka mia nne mtu mweupe amechomeka kisu chake chenye urefu wa futi moja ndani ya mgongo wa mtu mweusi, na sasa mzungu ameanza kuchomoa kisu hicho, tuseme kwa urefu wa inchi sita. Je mtu mweusi ana wajibu wa kushukuru hapa? Kwa nini? Hata kama mzungu atakitoa kisu chote nje bado na lazima litabaki kovu.!

Inaendelea toleo lijalo

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook