BARUA
 

Masheikh zungumzeni ya msingi, msitupotoshe

Ndugu Mhariri

HII ni mara yangu ya kwanza kukuomba nafasi katika gazeti letu hili la ANNUUR, kwa kigezo hicho naomba uniachie nafasi ndogo ili niweze kutoa mawazo yangu juu ya ugeni wa Ustadh Salum Msabaha hapa Mwanza kuanzia Machi 12 hadi Machi 15, mwaka huu.

Kwa umaarufu wa muhusika Msabaha ni maarufu, ni mtu anayejua kujieleza na kufafanua mambo. Nakumbuka kuna kipindi kimoja cha Kiti Moto (ITV), Bwana Msabaha alijieleza vizuri nikampa alama zote zote kulingana na umahiri wake wa kujua kuzungumza na kufafanua mambo kwa sera zake anazozijua yeye mwenyewe.

Huyu Bwana alijinyakulia umaarufu katika kikao kilichoandaliwa kutatua masuala ya mwezi. Ni mtu ninayemfahamu kwa msimamo mzuri tokea nyuma na ni Answar-Sunna imara.

Ameanza kufungua ukurasa mpya ambapo anapitia na kuzunguka Misikiti kuhamasisha muungano na mshikamano wa Waislamu.

Ziara yake ya hapa Mwanza imefanikiwa sana, kwani amepokelewa na kutukuzwa sana na kupewa heshima kubwa sana ya kutembelea miradi mbalimbali ya Waislamu, pia amepata nafasi mbalimbali ya kuzungumza na Waislamu na yeye pia kutoa nafasi ya kuulizwa maswali na Waislamu na kuyajibu.

Kwa nilivyomsikiliza Msabaha ni mtaalamu wa kupanga maneno ya kuvuta watu lakini mtizamo wake ulinistua pale alipotamka maneno ya namna hii:

Uchaguzi wa mwaka 2000 usiwasumbue Waislamu kwani hata tukimchagua Muislamu bado ataapa kwa kutumia katiba ya nchi wala si Qur'an. Kiongozi atakayechaguliwa ni vigumu kuongoza kwa kutumia Qur'an. Misikiti isitumike kama jukwaa la siasa kwa sababu siasa itawagawa Waislamu. Tuwafuate na kuwaelewesha viongozi (makafiri) makosa yao ale wanapotukandamiza ili wajirekebishe na mengine mengi ya aina hiyo.

Ndipo nikageuza muelekeo wa kumsikiliza na nikaona ni mtu aliye kuja kisiasa na akiwa kabeba bango la uwakala wa chama fulani ili kuwapoteza Waislamu warejeshe moyo kwa yale yaliyowakuta nyuma kwa manufaa ya watawala walio madarakani.

Sisi Waislamu tumefahamishwa vyema matatizo yetu kupitia vyombo vyetu vichache vya habari na tumeyaelewa na dhuluma zote tunazijua vyema. Na bado mikanda mbalimbali kama ya mauaji ya Mwembechai inazunguka mpaka hivi sasa imeenea karibia nchi nzima.

Nina hakika hilo ni funzo tosha kuonyesha ni namna gani Waislamu wanavyoteswa na (makafiri), kuuliwa katika nchi yao bila makosa. Msabaha anapoza joto ili iweje? Potelea mbali angeshawishi kama haiwezekani bora tusipige kura mwaka 2000 ili kuonyesha Waislamu wote tulivyochukizwa na matukio ya (kikafiri).

Yeye anapotumia nafasi ya suala la mwezi kuacha yaliyo ya msingi, mimi simuelewi. Waislamu wa Tanzania hawana shida na mwezi ili Uislamu usimame. Bali yapo mambo makubwa mazito yanayoukabili Uislamu. Ashughulike na hayo.

Bakari Salumu Dotto,
P.O. Box 2688,
Mwanza.



Ujahili wa Bedui haupo leo

Ndugu Mhariri

NAOMBA japo nafasi kidogo niweze kutoa dukuduku langu kuhusu Ustadh Msabaha yaani Salum Msahaba.

Salum Msabaha mwanasiasa na Mbunge wa zamani wa Chama cha (CUF) hivi majuzi Machi 12, mpaka Machi 15, mwaka huu amefanya ziara ya ghafula mjini Mwanza ambayo hatufahamu ilikuwa na mwelekeo gani.

Katika mikutano yote aliyoifanya, alifahamisha pamoja na mambo mengine kwamba hakuna chama kitakachoweka mgombea Urais atakayeapa kwa kutumia Qur'an tukufu ila atatumia Katiba ya nchi hii, kwa hiyo Waislamu tusijisumbue, tujiepushe na mawazo hayo.

Ndugu Msabaha mwanasiasa inaonekana amekuja kutufundisha siasa? Hakuishia hapo akawataka Waislamu wasiwe na hasira na kuchukua hatua dhidi ya madhalimu .

Msabaha kama nilivyo muelewa hoja yake kubwa ilikuwa kuwataka Waislamu wa Mwanza watenganishe dini na siasa.

Kuhusu hoja yake ya kuwafundisha majahili Uislamu, kwa sasa hivi haina nafasi. Je; Kamanda Gewe hajui kuua ni kosa! Yupi jahili leo kama yule Bedui asiyejua kwamba kukojoa kibarazani kwa mtu ni kosa sikwambii Msikitini. Au unataka kuwatukana polisi wetu kwamba wana ujinga huo?

Naomba wanaotaka kuja kwa sura ya Bw. Msabaha wavunje safari zao kwani Mwanza tuliisha wajua hamtupati ng'o.

Saida Juma Ngemera,
P.O. Box 6368,
Mwanza.



Ni kweli kila kilicho ardhini kimelaaniwa?

Ndugu Mhariri

KWANZA kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu (s.w.) na Mtume wake Muhammad (s.a.w.) kwa kutujaalia kufika hapa tulipofika leo na kwa uwezo wake amenijalia na mimi kuweza kutoa yangu machache.

Ndugu zangu Waislamu kutokana na upeo wangu mdogo naomba mchango wenu wa mawazo kutokana na jambo hili linalofuata.

Siku moja kulitolewa mawaidha na mmoja wa viongozi wetu wa dini akafika mahali akasema; nanukuu "kuna hadith moja ya Bwana Mtume (s.a.w.) inasema kwamba kila kilichopo ardhini kimelaaniwa isipokuwa vitu viwili tu Qur'an na msomaji wa Qur'an". Mwisho wa kunukuu.

Hapo ndipo ulipoingia utata katika akili yangu, kwanza kabisa kila nikifikiri katika hii hii ardhi ndipo inapopatikana Misikiti mitukufu mikubwa mawili, huko huko maelfu ya Waislamu humiminika huko kwa ibada ya Hijja katika kukamilisha nguzo za dini yetu ya Kiiislamu na huko ndiko liliko kaburi la kipenzi chetu Mtume wetu Muhammad (s.a.w.).

Ndugu zangu Waislamu naomba mnitoe kutu katika kichwa changu kutokana na kalima hii pengine mimi ndio nimeshindwa kumuelewa vizuri Sheikh wangu, basi nawaomba Waislamu mliojaaliwa na Mwenyezi Mungu msifiche elimu yenu itoeni nami niweze kufaidika nayo na hili lisipite bila ya kuchangia hoja zetu ili nami niweze kufunguka macho.

Ally Sadiki,
S.L.P. 60508,
Mbezi Beach,
Dar es Salaam.



Waislamu hatuna haki ya kujitetea

Ndugu Mhariri

WAISLAMU katika nchi hii hatuna haki, hatuna kujitetea na wala hatuna ruhusa ya kufuatilia masuala yanayotuhusu serikalini.

Ikiwa si hivyo kwa nini akamatwe kiongozi wa kuongoza utetezi wa haki zetu? Kwani yeye ni jambazi? Ni kosa kuongoza kikundi fulani kutetea haki na maslahi yao? Au tatizo ni kuwepo kwa hiyo Kamati ya kutetea haki za Waislamu?

Wabunge walipozitetea haki zetu waliambiwa wameleta udini Bungeni. Rais Mkapa kwenye Baraza la Idd alisema hakuwa na habari kwamba Waislamu wanayo madai mazito kama yale na akashangaa sana.

Na mpaka sasa yupo kimya. Japokuwa tunasubiri tulidhani katika Idi hii kuwa angepeleka salamu na kutueleza hatua aliyokwishaifikia tangu pale alipoyagundua manung'uniko yetu.

Bila shaka sasa salam zenyewe ndio hizi za kumkamata yule tuliyemtegemea kuiongoza kamati yetu ya kuzitetea haki zetu.

Mpenda haki
Mfukamanga.



Kumsaka Sheikh Ponda sio suluhisho

Ndugu Mhariri

NAPENDA kuielewesha serikali ya CCM kwamba kumsaka Sheikh Ponda Issa Ponda sio suluhisho, Sheikh Ponda hana makosa, kama inavyodai serikali ya CCM.

Kudai haki sio uchochezi, kudai uwiano katika serikali hii iliyojaa udini sio kosa.

Sheikh Ponda amefafanua wazi tena kwa kina na kwa ushahidi katika nyaraka zake nne alizozituma Ofisi ya Rais, Chuo Kikuu, Mwanasheria Mkuu, Usalama wa Taifa.

Hapo la msingi serikali ijibu nyaraka hizo, kumsaka Ponda ni kukubali kwamba serikali ya CCM kwamba inawachukia Waislamu hapa nchini.

Sisi Waislamu tulipenda serikali ya CCM itoe majibu kuhusu nyaraka za Ponda, sio iseme ni mchochezi, uchochezi maana yake nini, tunapenda serikali ya CCM itoe majibu ya kina yaliyo sahihi.

Karimu Athumani,
Kinondoni (A),
Dar es Salaam.



 Sherehe za Mwaka Mpya wa Kiislamu

Ndugu Mhariri

NAPENDA kuchukua nafasi hii kuwakumbusha Waislamu nchini kote na nje ya nchi tuungane kwa ajili ya kusherekea mwaka mpya wa Kiislamu.

Kila mwaka Waislamu tumekuwa na tabia ya kuungana na matwaghuti kusherehekea mwaka wao mpya ambao ni wa kitwaghuti. Kwa kweli ndugu zangu Waislamu ni lazima tuwe mstari wa mbele kwa kushiriki masuala ambayo yanatuhusu sisi.

Sasa basi na sisi Waislamu tujumuike kusherehekea mwaka wetu mpya wa Kiislamu kila mtu atambue kama leo Waislamu wanasherehekea mwaka wao mpya wa Kiislamu.
 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook