KUTOKA MAGAZETI YA ZAMANI
 

Maswanya ndio kiongozi wa Halmashauri ya Africanisation

Ngurumo Jumatatu, Machi 5, 1962

MAJINA ya wajumbe watakaofanya ile Halmashauri ya Africanisation, yametajwa. Tayari mwafahamu, kuwa Mwenyekiti wake ni Bwana Saidi Maswanya. Wajumbe wengine ni:

Bwana Salehe Kibwana, O.B.E. Mwenyekiti wa Halmashauri ya Tanga, Bwana Magongo, Naibu wa Katibu Mkuu wa TUPE, Bwana Jhaveri, M.P. na Mwandishi wa Ujumbe ni Bwana A.J. Namata.

Ujumbe huo umefanya mkutano wake wa kwanza kabisa siku ya Jumamosi, Machi 3, hapa mjini Dar es Salaam.

Halmashauri ile itachungua kwa makini kabisa, kila kazi na kila daraja katika Idara za serikali, na kuhakikisha kabisa ya kuwa uko mpango wa kufaa kwa Waafrika kushika vyeo vya madaraka kazini.

Wajumbe wa Halmashauri hii wanayo ruhusa ya kumhoji mtu yeyote katika utumishi wa serikali au mtu yeyote yule ambaye anaweza kuwapa habari zaidi kuhusu kazi yao. Tena watachungua mipango ya kutoa mafunzo kwa wale watumishi ambao wanafanya kazi serikalini ili Waafrika wale waweze kupata ujuzi wa moja kwa mmoja katika zile sehemu zinazofaa kwa kazi zao na kadhalika.

Mnaarifiwa

Yule Mwenyekiti, yeye kila wakati atakuwa akipashwa habari na kupewa mashauri, katika idara fulani, kuna nafasi kadha, kadha. Tufanye hivi, kuijaza nafasi ile ama aajiriwe Ofisa Mzungu kwa nafasi kadha.

Kila wakati, Halmashauri hii itakuwa ikitoa taarifa ya kazi yake katika Baraza la Kutunga sehria na mapendekezo yake yanaweza kukubaliwa na Mawaziri wanaohusika.

Kwenye ule mkutano wake wa juzi Jumamosi, Halmashauri hiyo imezungumza kwa jumla, ni habari gani Halmashauri ile inahitaji kutoka Wizara mbalimbali na Idara mbalimbali.



Amri ya Rais: Kiongozi wa TANU atiwe ndani

Ngurumo, Alhamisi, Mei 21, 1964

RAIS wa Jamhuri, Mwalimu Julius K. Nyerere, katoa amri watu wawili, katika mkoa wa Mara, wazuiliwe. Mtu mmoja katika hawa, Timothy Munema ni kiongozi wa TANU. Anashika cheo cha Mwenyekiti wa TANU huko Mara. Mtu wa pili, Lucas Kitugi yeye ni mfanya biashara maarufu sana mjini Musoma. Mwalimu aliwasili Mwanza jana.

Tangazo la serikali lililotolewa jana kutangaza habari za kuzuiliwa kwa watu wawili hawa, halikutaja kwa nini watu hawa wamezuiliwa. Walakini, taarifa hiyo imeeleza kuwa Mwalimu alihutubia mkutano wa Wazee mjini Mara, Mwalimu anasemekana kuwa kasema kuwa hatavumilia hata kidogo, matendo ya mtu yeyote anayewania kukanyaga bidii za watu katika maendeleo.

Kwenye mkutano huo Mwalimu pia alieleza mpango wa maendeleo wa miaka mitano kwamba ni mpango ambao umewaniwa kuinua kipato cha watu kutoka shilingi 400 kwa mwaka mpaka shilingi mita tisa kwa mwaka, pia pindi ikijafika mwaka 1980 Tanganyika iwe imekwisha jipatia watu wake wa kufanya kazi na kuongeza matazamio ya maisha.



Matata mengine yazuka Congo
 

Ngurumo, Jumatano, Mei 20, 2964

MAMBO yameumuka tena huko Kwilu, Congo, Juzi, askari wa jeshi la Congo wapatao 400 hivi walisemwa kuwa walizingirwa na wale vijana wanaofanya ghasia kule katika jimbo la Kwilu. Hali ya askari hawa ilisemwa kuwa ni mbaya. Walikuwa wametindikiwa na risasi na hawakuwa na njia ya kutokea.

Majeshi ya UNO ambayo yamekuwa yakilinda amani huko Congo kwa muda wa miaka minne sasa, yanaondoka. Lakini hata hivyo, ndege moja ya UNO, iliondoka Leopoldvile ikichukua silaha za UNO kwenda kuwasaidia wale askari waliozingirwa.

Habari zilizofika hapa zinaeleza kuwa Kaskazini Mashariki ya Kwilu kuna mji mmoja unaoitwa Idiofa. Mji huu umeharibiwa kupita kiasi na waasi hao na nyumba zipatazo mia moja hizi ziliteketezwa kwa moto katika mwezi Januari mwaka huu.

Hii ni mara ya pili kwa vijana hawa kufanya fujo huko Kwilu. Mapema mwaka huu kulizuka fujo katika jimbo kubwa hilo na kulipatikana habari vijana hao walikuwa wanapiga ndege na wakati mmoja waliangusha helikopta moja kwa mshale.



Tunguli zaonyeshwa kortini

Ngurumo Alhamisi, Mei 21, 1964

WATU watatu, akiwemo mwanamke mmoja, jana katika Baraza la Hakimu wa Kinondoni, walishitakiwa kushiriki katika pilikapilika za uchawi kwa kumchanjia bibi mmoja jirani.

Mshitakiwa wa kwanza, Jumbe Ismaili anashitakiwa kwa kuomba cheti cha uganga. Mshitakiwa wa pili Juta Sungura (Mganga), anashitakiwa kufanya uganga kwa kutumia dawa tofauti pamoja kupokea kiasi cha shilingi 10 kwa njia zisizo halali. Mshitakiwa wa tatu na wa mwisho, Bi Hadija Chande, anashitakiwa kumwita mganga na kufanya dawa zake.

Kurogwa

Baraza lilielezwa kwamba siku moja mwezi uliopita, Bibie mmoja ajulikanaye kwa jina la Bi Habiba alikwenda kwa Hadija kule Kinondoni katika kijiji kiitwacho Moskow. Ile fika yake kule kwa Hadija kulimwacha Hadija awe na wasiwasi, maana alisema eti alikwenda kumroga!

Hata siku moja Hadija akamwendea Jumbe wa kijiji hicho na kumweleza kuwa angependelea atafutiwe mganga mathubuti wa kumlisha kiapo Bi Habiba ili asimroge yeye (Hadija) au watu wengine wa mtaani. Sasa katika pitapita ya Jumbe, akamfuma mganga mmoja aitwaye Juta Sungura ambaye alisema kuwa angeweza kufanya kazi yao kwa ufasaha.

Achanjwa

Hatimaye Bi Habiba kaitwa. Yakafanywa mashauri kwamba alishwe kiapo na mganga huyo hapo... Bibie akakubali akachanjwa michale chwa ... chwa...chwa.. na vile bado akanyolewa sehemu fulani ya kichwa. Wakaondoka. Lakini usiku mumewe Habiba akamwona mkewe kachanjwa vya kutosha tena kichwani kulikuwa sivyo! Kuuliza akapewa vipande. Hakutosheka, akamwamuru mkewe kuiarifu polisi.

Washitakiwa wote wamekiri makosa yao, na kesi itaendelea tena Jumatatu.



Mfalme aweka jiwe la msingi Magomeni

Mwafrika, Jumatatu, Juni 15, 1964

ALIPOKUWA akimkaribisha Mfalme wa Ethiopia Emperor Haile Selassie I ili aweke jiwe la msingi na aweze kujionea mwenyewe ni nini serikali ya Muungano inataka kuwafanyia wananchi wake kwa upande wa makao, Waziri wa Serikali za Mitaa Bwana Austin Shaba alimweleza Mfalme huyo kwamba ni nia ya serikali yetu kuvunja vibanda ambavyo wananchi wa Taifa huru wanaishi na kuwajengea nyumba safi za kisasa.

Waziri huyu alimwambia kwamba hapa sasa katika mpango wetu wa miaka mitano wa maendeleo serikali imeamua kuvunja nyumba kiasi cha elfu tano na kujenga mpya badala ya hizo ambazo ni za kisasa.

Aliongeza kusema mpaka sasa sisi tumekuwa wenye habati kubwa sana kwa kukubali kwako kuweka jiwe la msingi wa nyumba ya kwanza ya mpango wa majumba yetu haya.

Aliendelea kusema kwamba shughuli na nia zako katika kusaidia kuweka jiwe la msingi wa nyumba ya kwanza ya mpango wetu, na katika kujenga umoja wa nchi za Afrika na kupigania uhuru wa Afrika nzima zajulikana pote ulimwenguni.

Pia katika kuweka jiwe hili la msingi leo waweza kujisikia kwamba ni hatua ingine ya kujenga Afrika ya kesho ambayo sisi wote twaitumaini kwa moyo wetu.

Katika kazi yako kubwa ya leo ambayo raia wote wa Jamhuri hii ya Muungano wanaifurahia ninayo heshima alimaliza kukutunukia mwiko huu wa fedha ambao utakuwa kama alama ya kupigana na umasikini katika Bara zima la Afrika.

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook