Na Mjahid Mwinyimvua
WIKI iliyopita Watanzania wameshuhudia kampeni kubwa ya upandaji wa miti. Baadhi ya wataalamu wa historia wamesema kuwa kampeni hii ya upandaji miti mwaka huu imekuwa na msukumo mkubwa zaidi kuliko hata kampeni za magonjwa ya watoto kama vile polio.
Hoja hii inathibitishwa na wakubwa walioshiriki katika kampeni hiyo. Rais wa Jamhuri ya Muungano, Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Marais waliostaafu (Mwalimu Nyerere na Mzee Mwinyi), Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Waziri Kiongozi, Katibu Mkuu wa Chama tawala (CCM), Mawaziri, Wabunge, Wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na viongozi wengine hadi ngazi ya mtaa au kijiji.
Waheshimiwa hao wote waliacha ofisi zao kwa muda na kwenda katika "field" (sehemu ya kazi), kuhamasisha wananchi na pia kushiriki katika kazi ya upandaji wa miti.
Hoja kubwa katika kampeni ya upandaji miti ni kuiokoa Tanzania na janga la jangwa ambalo linaweza kuleta majanga mengine kama vile ukame na njaa (upungufu wa chakula). Hoja hii ni sahihi.
Hata hivyo, sote tunakumbuka kuwa mwaka jana kulikuwa na mvua nyingi zilizoleta mafuriko na hatimaye kuharibu mazao, na nchi ikaingia katika baa la njaa. Vile vile mwaka huu vyombo vya habari vimepasha kuwa mto Rufiji umefurika na maji yameharibu mashamba (mazao) ya wananchi.
Pia mvua za mwaka huu zimeleta maafa katika sehemu nyingine za nchi yetu. Kwa mfano kule Mkoani Mara daraja muhimu linalounganisha Tanzania na nchi ya jirani limevunjwa na maji ya mvua.
Tukitazama jiografia ya Tanzania tunaona kuwa bado tunapata mvua na pia tuna bahari, mito na maziwa. Kwa hiyo, kazi ya upandaji miti kuipa msukumo mkubwa kuliko ile ya kilimo na hali Watanzania wanakufa kwa njaa, itafika mahali kazi hiyo ya upandaji wa miti haitaleta faida yoyote kwa Watanzania na wananchi wengine duniani.
Hii ni kwa sababu, kazi siyo tu kupanda miti bali pia kuitunza. Mwananchi anayeshindwa kusimama kwa sababu ya njaa ataweza wapi kupalilia na kumwagilia maji (kama yapo) mti!
Katika utawala wa serikali ya awamu ya kwanza, chini ya Rais mstaafu Mwalimu Nyerere, Tanzania ilikumbwa na janga la njaa zaidi ya mara moja.
Hata hivyo, katika serikali ya awamu ya pili, chini ya uongozi wa Alhaj Ali Hassan Mwinyi, baa la njaa lilipungua kwa kiwango kikubwa. Na haikutokea watu kula dona (unga wa mahindi) linalostaili kulikuwa na wanyama, kama ilivyokuwa katika awamu ya kwanza.
Lakini neema ya wingi ubora wa vyakula Tanzania haikudumu. Mzee rukhsa (Alha Mwinyi) alivyoondoka madarakani kana kwamba kaondoka na neema hiyo.
Serikali ya awamu ya tatu chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Benjamin William Mkapa, ikaanza kuchapa kazi kwa kuchoma tani kadhaa za ngano, za mfanyabiashara Said Salum Bakhresa, kwa hoja kwamba ngano hiyo haikufaa kwa matumizi ya binadamu.
Kuanzia hapo, iwe mvua au liwe jua kila mwaka kuna baa la njaa, tena kubwa mpaka linatoa roho za wananchi walioiweka madarakani serikali ya awamu ya tatu.
Licha ya ahadi ya Rais na viongozi wengine wa chama (tawala) na serikali kuahidi kuwa hakutakuwa na mwananchi atakae kufa kwa njaa, makumi kama siyo mamia ya roho za Watanzania zimetoka kwa sababu ya njaa.
Sijui kama viongozi wetu wanakumbuka ahadi yao hiyo waliyoitoa kwa umma wa Tanzania. Nauliza swali hili kwa sababu hatujawasikia viongozi hao wakiomba msamaha kwa ahadi "hewa" waliyoitoa, achilia mbali kujiuzulu (kwa kuvunja ahadi jambo ambalo ni kinyume cha katiba).
Kukaa kimya kwa viongozi wetu, na huku kila kukicha hali inakuwa mbaya zaidi kwa wananchi,si ufumbuzi wa baa la njaa bali ni hatari zaidi.
Jumanne, Aprili 14 mwaka huu gazeti la Dar Leo liliripoti hali mbaya ya njaa katika eneo la Mahenge, wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro.
Gazeti hilo limeripoti kuwa hali ni mbaya mara dufu kulinganishwa na inavyosimuliwa katika vyombo vya habari, jogoo la kuku linauzwa kwa bei ya shilingi kumi na mbili.
Dar Leo linaendelea kuripoti kuwa, afya za watu zimedhoofu kiasi cha kutotofautisha kati ya vijana na wazee. Vile vile Dar Leo limesema kuwa, shule katika vijiji vya Chigandugandu, Lukande na Mwambunga zimeota nyasi kwani wanafunzi hawasomi tena kutokana na njaa.
Zaidi ya hayo, gazeti hilo linaripoti kuwa, serikali imekuwa ikipeleka misaada kidogo ambayo haitoshelezi kabisa kuleta unafuu wa baa hilo.
Tukitafakari hali ya dhiki ya njaa inayowakabili wananchi hasa wa vijijini, na tukitafakari juhudi ndogo ya serikali katika sekta ya kilimo, sambamba na juhudi mpya kubwa ya upandaji miti, tunalizamika kuizindua serikali kuhusu sera yake ya kilimo (kama ipo).
Wakati umefika sasa wa kuacha maneno badala yake viongozi wa ngazi zote watumie muda wao mwingi kwenye "field" (vijijini) ili kuleta mapinduzi ya kilimo.
Sote tunajua moja ya tatizo sugu linalochangia kudidimiza kilimo nchini ni wakulima kukopwa au nyakati nyingine kutolipwa kabisa mazao yao.
Nina hakika kama viongozi wangejitolea kama walivyofanya katika kampeni ya upandaji miti, wananchi wasingedhulumiwa mazao yao na wajanja wachache kwa hiyo wangekuwa na na nafasi kubwa katika kuboresha kilimo chao cha jadi na kuwa cha kisasa.
Wakubwa mlioko madarakani
na wale waliostaafu tunawaomba mbadili mtazamo na hatimae mwelekeo ili
kilimo kweli kiwe uti wa mgongo wa uchumi wetu. Vinginevyo wananchi hawataweza
kupanda wala kutunza miti.
|
|