Dhibiti yangu maguvu
Allah wewe una nguvu, umeniumba
kiumbe,
Wangu ujana na nguvu, visinioteshe
pembe,
Vikanipa ukomavu, kudhuru
wako viumbe,
Dhibiti yangu maguvu, ujana
usinishinde.
Allah umrehemevu, nakuita
unilinde,
Unikinge na maovu, nisije
kwenda upande,
Nifanye niwe shupavu, mabaya
nisiyapende,
Dhibiti yangu maguvu, ujana
usinishinde.
Nichukize na mabovu, hata
kama wayapambe,
Nipambane na waovu,
na wale wao wapambe,
Nivunje yao mabavu, niwazime
wasitambe,
Dhibiti yangu maguvu, ujana
usinishinde.
Ya kwangu haya maguvu, yafanye
haki itendwe,
Wanyonge waso na nguvu,
kwa zangu nguvu walindwe,
Masikini walemavu, wote
hawa wanipende,
Dhibiti yangu maguvu, ujana
usinishinde.
Nifanye mnyenyekevu, yalomema
niyatende,
Niwe na fikra pevu, ziongoze
ummah wende,
Niwe kijana mwerevu, na
stadi nizipende,
Dhibiti yangu maguvu, ujana
usinishinde.
Nifanye mkakamavu, vita nipige
uzembe,
Nisifanye ulegevu, wako
kufata ujumbe,
Nikitoka mvi ndevu, nyingi
hekima nipambe,
Dhibiti yangu maguvu, ujana
usinishinde.
Niwe mtu msikivu, machafu
nipige pande,
Nifunike utulivu, jazba
zitoke zende,
Nilinde na upumbavu, kwangu
usiranderande,
Dhibiti yangu maguvu, ujana
usinishinde.
Madhalimu wapotevu, niwatwange
kwa vijembe,
Uwakamate uchovu, wazidiwe
ndembendembe,
Yakome yao mabavu, kudhuru
wako viumbe,
Dhibiti yangu maguvu, ujana
usinishinde.
Nipe mwenza mtulivu, anilinde
nimlinde,
Aliye mvumilivu, mitihani
aishinde,
Kizazi chenye wakovu, akifunze
kisipinde,
Dhibiti yangu maguvu, ujana
usinishinde.
Aniamshe kwa nguvu, visimamo
tujipinde,
Usiku ulo mpevu, ili Allah
atupende,
Tuswali kinyenyekevu, atupe
nguvu tushinde,
Dhibiti yangu maguvu, ujana
usinishinde.
Nyumba iso na mabavu, ya
kupotosha viumbe,
Ing’are kama mapovu, meupe
yaso na chembe,
Iuzime upotevu, kwa nuru
giza lifumbe,
Dhibiti yangu maguvu, ujana
usinishinde.
Zangu pumzi na nguvu, kwa
wema zishe niende,
Itoke kwa utulivu, roho
mwili usidunde,
Nisitajwe kwa maovu, nyuma
mema yayashinde,
Dhibiti yangu maguvu, ujana
usinishinde.
Allah wamiliki nguvu, kwa
jihadi unipambe,
Washeheneze maguvu, Wajahidi
wasiyumbe,
Wawashinde wapotevu, wenye
akili za pombe,
Dhibiti yangu maguvu, ujana
usinishinde.
Peni inakuwa kavu, nakoma
mbele nisende,
Na waasa wanyenyekevu, dhulma
msiitende,
Allah anateza nguvu, atawavunja
vipande,
Dhibiti yangu maguvu, ujana
usinishinde.
Said Ally Mubaraka Soud
(Mzee wa Shaksiyya)
Ubungo Islamic College
of Education,
S.L.P. 55105,
Dar es Salaam.
Vazi lenye heshima
Bismillahi naanza, kutoa
yangu maoni,
Kwa baraka za Muweza, ya
Karima ya Manani,
Kwa kalamu nacharaza, kwa
moyo wenye imani,
Buibui natamka, ni vazi
lenye heshima.
Mungu ni mwenye busara, na
hekima teletele,
Katuwekea ishara, tujue
nyuma na mbele,
Sharia yake imara, kabisa
haina ndele,
Buibui natamka, ni vazi
lenye heshima.
Enyi wake watiifu, msifunge
masikio,
Sifuati uzandifu, kisha
takuwa kilio,
Wala dini sikashifu, andama
yote yalio,
Buibui natamka, ni vazi
lenye heshima.
Miaka tisa kitimu, uchanga
ushakimbia,
Fuata njema elimu, Kurani
ilotimia,
Wazee wako heshimu, sikia
wanakwambia,
Buibui natamka, ni vazi
lenye heshima.
Mungu amewatukuza, wanawake
Islamu,
Kawatoa kwenye kiza, kuwaonya
ya haramu,
Mwili kujifunikiza, Ni sheria
mufahamu,
Buibui natamka, ni vazi
lenye heshima.
Mola huwapenda waja, wenye
kuandama ndia,
Cheo cha mtu si hoja, ikiwa
hana sheria,
Amini Mungu mmoja, Mola
takuangalia,
Buibui natamka, ni vazi
lenye heshima.
Sijifanyi hayawani, kuwa
kiguu na ndia,
Ukosefu wa imani, jeuri
kupakilia,
Tuputupu manjiani, watu
kushangilia,
Buibui natamka, ni vazi
lenye heshima.
Na tabia angalia, sikuzunguke
na kelele,
Maguu kupigilia, jitembeze
pole pole,
Upuuzi si tabia, na maasi
yastole,
Buibui natamka, ni vazi
lenye heshima.
Mola tuongeze njia, tufate
yalo ya kheri,
Tufuate ya sheria, tujikinge
na ya shari,
Mema kuyashikiria, tuwe
Islamu kweli,
Buibui natamka, ni vazi
lenye heshima.
Kabola J. Sokwa,
Ubungo Islamic High School,
S.L.P. 55105,
Dar es Salaam.
Bismillahi naanza, naingia
mitamboni,
Nilo nayo kueleza, msikize
kwa makini,
Huenda mkajifunza, kupitia
shairini,
Mwaka mpya umefika, sote
tuupokeeni.
La mgambo limelia, toka bara
hadi pwani,
Mwaka mpya kuwadia, hapa
petu duniani,
Ni elfu nne mia, na ishirini
yakini,
Mwaka mpya umefika, sote
tuupokeeni.
Elfu na mia nne, pamoja na
ishirini,
Kwenye mema tuungane, mabaya
tuyahameni,
Na wala tusigombane, katika
mambo ya dini,
Mwaka mpya umefika, sote
tuupokeeni.
Bora tushukuru Mungu, ikiwa
tuna imani,
Kwa rehema zake Mungu, bado
tupo duniani,
Ni wangapi walimwengu, wametoweka
machoni,
Mwaka mpya umefika, sote
tuupokeeni.
Mema tuyatafakari, ya mwaka
jana jamani,
Pamoja na kukhiyari, kuyadumisha
yakini,
Dhambi kustaghfari, kwa
kutubu kwa Manani,
Mwaka mpya umefika, sote
tuupokeeni.
Tuupokee kwa wema, sote tuwe
furahani,
Kwa kula vilivyo vyema,
na vinywaji majumbani,
Kupongezana ni vyema, ulevi
tusithamini,
Mwaka mpya umefika, sote
tuupokeeni.
Nimelitunga shairi, ili tuwe
furahani,
Mwaka mpya umejiri, mwaka
wetu waumini,
Wa kuhama Mukhtari, kwenda
Madina mjini,
Mwaka mpya umefika, sote
tuupokeeni.
Shairi nimelitunga,
kupitia gazetini,
Ambalo hutupa mwanga, kwa
amri ya Manani,
Mtume kwambiwa anga, safari
na waumini,
Mwaka mpya umefika, sote
tuupokeeni.
Mtume kutoka Makka, kuhamia
ugenini,
Na Madina akafika, akakaa
kwa amani,
Ndipo ikakubalika, kalenda
yetu ya dini,
Mwaka mpya umefika, sote
tuupokeeni.
Alipofika Madina, walimngoja
njiani,
Kwa mashairi kunena, umechomoza
langoni,
Karibu kwetu Madina, tunakupa
shukrani,
Mwaka mpya umefika, sote
tuupokeeni.
Mwisho ninasisitiza, Mungu
tumuogopeni,
Atakayo kutimiza, mawi kuweka
pembeni,
Kwa wema kuzungumza, na
wenzetu duniani,
Mwaka mpya umefika, sote
tuupokeeni.
Twalaal Badru Alayna, Min
Thaniyyaatil Wadai,
Wajabash Shukru Alayna,
Madaalillaahi Dai,
Ayyuhal Mab Uthu Fiyna,
Jiita Bil Amril Mutwai,
Jiita Sharraftal Madina,
Marhaban ya Khayra Dai.
Juma M. Bwanakheri,
(Ustaadh),
S.L.P. 45245, Dar es
Salaam.
Ninamlaani shetani, alotoka
rehmani,
Nachukua Qur’an, nataka
yaliyo ndani,
Nipate kuzibaini, sifa zao
waumini,
Hawa ndio waja wema, awapenda
Rahmani.
Katika ya upuuzi, kuwakuta
ni muhali,
Na maneno ya kuudhi, wajipushie
mbali,
Tupu wanazihifadhi, kuzini
hawakubali,
Hawa ndio waja wema, awapenda
Rahmani.
Sala zinawahifadhi, wafanya
mambo azizi,
Na hawayawii radhi, machafu
yaliyo wazi,
Dhuluma kwenye ardhi, wakata
yake mizizi,
Hawa ndio waja wema, awapenda
Rahmani.
Mema wanayapupia, mabaya
wayakimbia,
Pale wanapokosea, haraka
wanatubia,
Na wanapokosolewa, wanarudi
kwenye njia,
Hawa ndio waja wema, awapenda
Rahmani.
Mema wayalingania, mabaya
wayakemea,
Muda wanautumia, na mapesa
kwa mamia,
Bongo wanazisugua, kalamu
wazitumia,
Hawa ndio waja wema, awapenda
Rahmani.
Islamu anuani, wanojitambulishia,
Nyingine hawazioni, zenye
kupoteza njia,
Nyongeza hawatamani, kamba
wanashikilia,
Hawa ndio waja wema, awapenda
Rahmani.
Mikakati wanabudi, lengo
wapate fikia,
Mbinu wazitathmini, mipango
wajiwekea,
Vikwazo wavibaini, vilivyoko
kwenye njia,
Hawa ndio waja wema, awapenda
Rahmani.
Daima huwa mfano, kwa vitendo
na maneno,
Watu wenye msimamo, mwenendo
wao ni kisomo,
Wenye kujali kisomo, pamoja
na kisimamo,
Hawa ndio waja wema, awapenda
Rahmani.
Pamoja washikamana, huruma
waoneana,
Mema huamrishana, maovu
wakatazana,
Wenye kusaidiana, wanaosameheyana,
Hawa ndio waja wema, awapenda
Rahmani.
Watu wasio papara, wenye
kufanya subira,
Wafanyao biashara, ya dunia
kwa akhera,
Wanosimama imara, wasokubali
khasara,
Hawa ndio waja wema, awapenda
Rahmani.
Watu wanotafakari, wasopenda
yafakhari,
Uongo hawakariri, ukweli
wanaukiri,
Tena hawi kiburi, kwa tajiri
na fakiri,
Hawa ndio waja wema, awapenda
Rahmani.
Watendao kwa Ikhlasi, mambo
bila wasiwasi,
Muumba hawamuasi, hata iwe
kwa risasi,
Wagumu kwa vishawishi, kawashindwa
Ibilisi,
Hawa ndio waja wema, awapenda
Rahmani.
Allah ndiye Mkwasi, tuondoe
wasiwasi,
Tukinge na vishawishi, tusome
kwa urahisi,
Moyoni tuwe wasafi, mema
yapate nafasi,
Nimechoka najihisi, kalamu
naijilisi.
Idd S. Kikong’ona,
Morogoro.
Wenzetu akinamama, Dada mwatuaibisha,
Mavazi yaso heshima, kuvaa
yasikitisha,
Yanaleta uhasama, waume
kutamanisha.
Hijabu ni vazi jema, tulivae
kinamama.
Tulivae kina mama, Hijabu
kulidumisha,
Staha ya mwili mzima, burudani
hiyo tosha,
Hakuna kukusakama, wala
kukubabaisha,
Hijabu ni vazi jema, tulivae
kinamama.
Vimini sasa kukoma, kuvaa
kuvifupisha,
Fahamu mwili mzima, jua
unauonyesha,
Maadili yamehama, ya asili
kupotosha,
Hijabu ni vazi jema, tulivae
kinamama.
Imebaki dhahama, matusi kutukanisha,
Wengine watu wazima, vijana
wawapotosha,
Wawe ni mfano mwema, kuweza
kuwafundisha,
Hijabu ni vazi jema, tulivae
kinamama.
Badala yake lawama, wazazi
kujibebea,
Wana Harakati Wima, fedheha
kuondoa,
Liwe jambo la lazima, mkazo
kulitilia,
Hijabu ni vazi jema, tulivae
kinamama.
Mwenyekiti Mama, Fatma Lazaro
katuambia,
Tusibakie kusema, vitendo
twarajia,
Yapungue lau kama, nguo
fupi kutupia,
Hijabu ni vazi jema, tulivae
kinamama.
Pongezi kwako Waziri, Elimu
Utamaduni,
Kupasisha vazi zuri, livaliwe
mashuleni,
Tunataka lisafiri, mijini
na vijijini,
Hijabu ni vazi jema, tulivae
kinamama.
Ni vazi la kujistiri, refu
hadi miguuni,
Linahimiri kikiri, hata
kazi za nyumbani,
Beni nane nasafiri, kalamu
naweka chini,
Hijabu ni vazi jema, tulivae
kinamama.
Umoja wa Kinamama Gongo
la Mboto,
Dar es Salaam.
|
|