TUITION
Elimu ya Dini ya Kiislamu kwa shule za Sekondari
Fiqh Form iv
Siasa na uendeshaji wa dola
 

WAPO wanaodhania kuwa Uislamu hauna siasa, wapo wanaodhania kuzungumzia serikali ya Kiislamu ni kuchochezi. Mbaya zaidi ni kule kutofahamika na Waislamu wengi kuwa pasipo serikali ya Kiislamu Uislamu mashakani.

Sura halisi ya Uislamu ilijitokeza Madina ambapo Uislamu uliasisi kanuni za uendeshaji mambo ya kijamii. Dola ya Kiislamu Madina ilionyesha sura halisi ya haki, sheria, mahakama, katiba, mikataba, diplomasia,usawa, umoja na kadhalika. Maeneo yote haya ya kijamii yalielezwa kwa nadharia na kutafsiriwa kwa vitendo ndani ya dola ya Kiislamu chini ya uongozi wa Mtume (s.a.w.).

Fiqh kidato cha nne inajadili na kuchambua ujenzi na uendeshaji wa familia na jamii kwa mtazamo wa Kiislamu huku ikilinganishwa na mifumo ya kijamii iliyopo. Kutokana na ufinyu wa nafasi mafundisho yetu katika sehemu hii yatazingatia mfumo wa kijamii tu ambapo tutaanza na: Siasa na uendeshaji wa dola, sheria na uchumi. Panapo majaaliwa tutahitimisha sehemu hii kwa kuangalia suala la uadilifu.

Maana ya siasa:

SI rahisi kuwa na tafsiri moja ya siasa, lakini Wataalamu wa mambo ya siasa kwa ujumla wamejaribu kuianisha siasa kwamba ni mambo yanayohusu jamii. Kiistilahi wanaeleza kuwa ni dhana ya mpangilio wa uendeshaji mambo kijamii, ambayo hutokana na itikadi ya mtu, kikundi cha watu au ufunuo toka kwa Muumba. Pia siasa ni mfumo wa uratibu na ufahamu wa hali zinazojitokeza kijamii katika utumiaji wa rasilimali. Vile vile ni kanuni au njia ambayo baadhi ya watu huitumia kupata uwezo wa kutawala wengine ili kukidhi matashi yao binafsi. Hii ina maana kuwa siasa ndio ufafanuzi wa maingiliano na mahusiano ya watu na shughuli zao, kwani katika maisha yao, wanaadamu huhitajiana na kuhitajiana huko ndiko kunakojenga mahusiano na maingiliano yao ya kila siku. Kwa hivyo ni dhahiri kuwa siasa ni plani au mwigo wa uyakini ambao hutumika kufahamu na kuendesha shughuli zote za jamii kitaifa na kimataifa (Taz. Theories of the state by Patric D and B O' Leavy).

Kumbukumbu za kihistoria zinafahamisha kwamba, siasa ilianza pale wanaadamu walipoanza kuishi pamoja kama kijiji, mji, taifa hadi kufikia mataifa. Hivyo, siasa ni jambo kongwe kama ilivyo historia ya mwanaadamu mwenyewe.

Dhana kuu za siasa ni; utawala (mamlaka), itikadi, matashi na maamuzi. Yaani kule kuwa na madaraka ya kutumia vyombo vya dola ili kuweka, kusimamia na kushinikiza utaratibu, sera, au matakwa fulani. Aidha kuwa na mkusanyiko wa fikra zinazounda mwongozo na mwelekeo katika utendaji wa shughuli mbalimbali (itikadi) za kijamii. Msukumo wa mawili hayo hutegemea matashi na maamuzi ya wahusika (Taz. Introduction to politics by Godffrey Ponton & Peter Gill). Hivyo kwa upande mwingine tunapoitazama istilahi ya siasa hatunabudi kuzingatia kuwa ni; mfumo wa utawala (power), itikadi (system of thought and action), matashi (interest) na maamuzi ya ama mtu, kikundi cha watu, au ufunuo kutoka kwa Muumba.

Mifumo ya siasa katika jamii ya mwanaadamu

Kwa mtazamo wa Uislamu zipo aina kuu mbili za mifumo ya siasa:

(1) Mifumo ya siasa iliyobuniwa na wanaadamu (siasa za kitwaghuti)

(2) Mfumo wa siasa wa Kiislamu.

(1) Mifumo ya siasa za Kitwaghuti

Kwa mtazamo wa Kiislamu, masuala ya kijamii yenye kufuata mitindo na mipangalio iliyobuniwa na watu, hutazamwa kama siasa za Kitwaghuti. Siasa hizi hutokana na fikra au matashi ya watu. Katika historia yake, ambayo humnasibisha mwanaadamu na mnyama aliyepitia mabadiliko kadhaa ya kimaumbile, siasa hizo zimepita vipindi mbalimbali hadi kufikia karne hizi. Vipindi hivyo ni pamoja na:

(i) Ujima wa mwanzo

(ii) Utumwa

(iii) Umwinyi

(iv) Ubepari

(v) Ujamaa na Ukomunist

(vi) Demokrasia

Kuibuka kwa siasa za Kitwaghuti

(I) Ujima wa awali

Nadharia za Kitwaghuti zinamuangalia mwanaadamu kama ni mnyama ambaye katika kipindi cha ujima wa awali hakutofautiana na wanyama wengine. Yeye pia aliishi mtini, akaenda kwa miguu na mikono kwa pamoja. Hakutofautiana sana na nyani alipokuwa katika hali ya usokwe-mtu. Kutokana na mabadiliko ya kimazingira baadhi ya wanyama, miongoni mwao akiwemo sokwe - mtu walitoka katika hali ya kuishi mitini, wakateremka chini. Hapo ndipo yalipotokea 'mabadiliko' ya maumbile ya miili yao kulingana na mazingira mapya. Lakini kutokana na uhasama uliokuwepo katika mazingira hayo mpya, kwani misitu na wanyama wakali ilikuwa imeenea kote, mtu wa mwanzo hakuweza kuishi peke yake kiubinafsi. Hali hizo za kimazingira zilimlazimisha mtu wa mwanzo aishi kwa ushirikiano na wenziwe ili aweze kupambana na mazingira hayo makali. Hapo ndipo ilipoanza siasa kwa mujibu wa nadharia hii.

(ii) Mfumo wa siasa za utumwa

Mfumo wa sisa za kitumwa unafuatia baada ya ujima katika mlolongo wa siasa za kitwaghuti. Huu ni mfumo wa siasa za kitabaka huruhusu baadhi ya watu kuishi kwa jasho la watu wengine. Watu hao wenye fursa za mali au hadhi katika jamii huishi kwa kuwatumikisha wengine. Katika mfumo huu, utawala ulikuwa mikononi mwa matajiri ambao waliendesha siasa za kuwatumikisha wengine na wao kuishi maisha ya raha. Chini ya mfumo huu wa siasa, uzalishaji mali uliwekwa migongoni mwa watu wa tabaka la chini la watwana.

Inaelezwa na wachambuzi kuwa mfumo huu wa kitumwa ulianza kuyumba kwa migongano mbalimbali. Watumwa walianza kuamka na kujidhatiti kisha kuanza kupinga vikali sana hali hiyo ya utumwa. Nao Watu ambao awali walinyang'anywa mali zao na mabwana wenye watumwa waliungana na watumwa yakawa mapambano ya watwana na mabwana hatimaye kuufuta utumwa.

(iii) Mfumo wa siasa za Kimwinyi

Siasa za Kimwinyi ambazo inadaiwa zilifuatia baada ya siasa za kitumwa. nazo vile vile zilikuwa na minyororo yake. Katika mfumo huu tabaka la kimwinyi lilitawala njia zote za kijamii. Njia za uchumi zilitawaliwa kwa kukodisha mashamba halafu kutoa fungu kubwa kwa mwenye shamba wakati wa mavuno. Wazalishaji kwenye mashamba hayo chini ya mfumo huu, tofauti na utumwa, walilipwa posho ndogo kama malipo ya kazi nzito walizotumikishwa na mabwanyenye. Inadaiwa kuwa taasisi za dini pia zilitumika "kuhalalisha" ubwana na utwana! Mfumo wa siasa za kimwinyi ulisita kuendelea baada ya wanyonywaji kujiunga pamoja dhidi ya wanyonyaji.

(iv) Mfumo wa siasa za kibepari

Siasa za kibepari ni moja ya mifumo ya Kitwaghuti iliyokita mizizi katika jamii nyingi. Katika mfumo huu kila kitu kinachowezekana kufanywa ili "kuzalisha" pesa hufanywa. Wachache walio na fursa za mali na hadhi ndiyo huendesha masuala yote ya jamii na kundi kubwa la wanajamii huishi kwa kuuza nguvu, vipaji na taaluma zao kwa wachache hao, na wale wasio na chochote hulazimika kuishi maisha ya magumu na ya kubahatisha (kwa upande wa wanawake) kuuza miili yao, na wanaume kufanya vitendo vyovyote vile ili mradi waweze kujikimu kimaisha.
 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook