JIFUNZE SHERIA
Mashitaka ya Jinai na utetezi-3

Dhamana

Na Dkt. Abdallah J. Saffari

Mtu aliye chini ya ulinzi wa kisheria anaweza akaweka na kupewa dhamana na kuachiwa huru hadi wakati wa siku ambayo atahitajika kufika sehemu anayotakiwa kama vile kituo cha polisi au mahakamani.

Dhamana huweza kuombwa na kutolewa katika hatua tatu tofauti: wakati wa upelelezi wa shauri (F.64(2), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j) usikilizaji wake (F.148, Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j) na mwisho, kabla ya rufani kusikilizwa. (F.368, Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j).

Wakati wa upelelezi wa kesi polisi wanaweza kumkamata yaani kumtia nguvuni mtuhumiwa ili awasaidie na upelelezi wa shauri linalohusika. Baada ya mahojiano wanaweza kumwachia mtuhumiwa huyo kwa dhamana. (F.64, Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Hii hujulikana zaidi kama dhamana ya polisi. Dhamana haiwezi kutolewa iwapo mshitakiwa anashitakiwa kwa kosa la mauaji au uhaini. (F.148(5) Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Hata hivyo baadhi ya mahakama duniani yamewahi kutoa dhamana katika kesi za mauaji licha ya sheria kukataza jambo hilo. Mathalan katika Owusu and Another v. The Public, (1980) GLR 469. Angalia pia Seida and Others v. The Ruplic (1978 1 GLR 67), Mahakama Kuu ya Ghana yalitoa dhamana kwa vile ilidhihirika kwamba shauri lenyewe lingechelewa mno kusikilizwa. Hadi wakati wa maombi ya dhamana, tayari mshitakiwa alikuwa amekaa rumande kwa zaidi ya miaka mitatu. Ilidhihirika pia kuwa hali yake ya afya ilizidi kuwa mbaya. Lakini sababu muhimu kupita zote ni kuwa mahakama yaliridhika kuwa hakukuwa na ushahidi unaotosheleza kufungua shitaka la mauaji ya kukusudia. Sababu kama hiyo pia ilitumiwa na Mahakama Kuu ya Tanzania kumpa dhamana mshitakiwa wa mauaji ya kukusudia katika R. v. Daimu Mkando na Wenzake (Maombi Maalum ya Jinai Na. 24, 1985, Mahakama Kuu, Arusha) na R. v. Patrick Soka na Wenzake( Uchunguzi wa Awali Na. 16, 1989, Mahakama Kuu, Arusha).

Licha ya makosa ya mauaji ya kukusudia dhamana pia haitatolewa iwapo mshitakiwa aliwahi kuvunja masharti ya dhamana au ameshitakiwa kwa kosa alilolitenda akiwa katika dhamana. Dhamana pia itakataliwa iwapo Mkurugenzi wa Mashitaka, atapinga kwa hati maalum kwamba dhamana isitolewe kwa vile itahatarisha usalama au manufaa ya taifa. (F.. 148(4) Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j. Angalia pia F.35(2), Sheria ya Makosa ya Kiuchumi, Na. 13, 1984).

Katika Daud Pete v. R (Shauri Maalum la Jinai Na. 80, 1989, Mahakama Kuu, Mwanza) uwezo huu wa Mkurugenzi wa Mashitaka kupinga dhamana ulionekana kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kwa vile unamnyima mshitakiwa haki yake ya kibinadamu ya kujitetea kabla hajakataliwa dhamana. Kwa bahati mbaya baadaye Mahakama ya Rufani ya Tanzania hayakulijadili suala hili kwa undani katika R. v. Daudi Pete (Shauri la Jinai la Rufani Na. 28, 1990, Mahakama ya Rufani ya Tanzania) wakati ambapo Jamhuri ilipania kutengua hukumu ya awali ya Mahakama Kuu katika shauri hilo.

Mtuhumiwa alipofunguliwa mashitaka rasmi hatua nyingine huanza, ambayo inamkabidhi mikononi mwa mahakama kuanzia wakati huo mpaka shauri lake litakapomaliza kusikilizwa.

Dhamana huweza kutolewa kwa washitakiwa wa makosa yote isipokuwa yale yaliyotajwa punde tu. Vinginevyo mahakama bado yana uwezo wa mwisho kumwachia mshitakiwa kwa dhamana au la. Na vile mshitakiwa sio mhalifu hadi inapothibitishwa hivyo, dhamana hukataliwa pale tu kunapokuwa na sababu za msingi sana.

Masuala kadhaa hutiliwa maanani na mahakama yanapofikiria kukubali au kukataa ombi la dhamana. Uzito wa kosa ambalo mshitakiwa anakabiliwa nalo ni moja ya masuala hayo. Hofu ni kwamba iwapo mshitakiwa atapatikana na hatia anaweza kupewa adhabu kali, jambo ambalo huweza kumtisha au kumshawishi kutoroka akiwa nje ya dhamana.

Kwa hiyo mahakama huwa tayari kukubali dhamana kuhusiana na makosa madogo kuliko yale yenye adhabu kali kama vile kifungo cha muda mrefu. Katika shauri la Asoke v. R. (1971 H.C.D. n.192). Mrufani alipinga uamuzi wa Mahakama ya Wilaya kuyakataa maombi yake ya dhamana. Mrufani alikabiliwa na shitaka la wizi la shilingi milioni 250,000 mali ya serikali ya Tanzania. Alikuwa raia wa Kenya, Mkurugenzi wa Kampuni moja kubwa ya biashara Uganda, alikuwa na nyumba nzuri Uganda na Kenya. Ingawa alikuwa na wadhamini Watanzania wenye mali ya kutosha, Mahakama Kuu iliitupilia mbali rufani hiyo kwa sababu uwezekano wa kutoroka katika mazingira ya kesi hiyo usingefaa kupuuzwa.

Uwezekano wa kutenda kosa jingine au kulirudia lile lile pia hutiliwa maanani. Mifano ni mashauri haya mawili yafuatayo:

Katika kesi ya John Mswani na Wenzake v R. (1970 H.C.D. n.59) mrufani alipinga uamuzi wa mahakama ya awali kumkatalia dhamana. Alikuwa anakabiliwa na shitaka la wizi. Hata hivyo Jamhuri ilithibitisha kwamba wakati ambapo mrufani aliachiwa kwa dhamana mara ya kwanza alijihusisha na kosa jingine la kughushi hundi. Mahakama Kuu yaliridhika na maelezo hayo ya Jamhauri na kuikataa rufani ya John Mswani.

Katika kesi ya Jonathan Mwaniki v. R. (1970 H.C.D. n.177) Mahakama Kuu yalikataa rufani ya kupinga kukataliwa dhamana kwa vile mrufani alionekana anaweza kuendelea kujidai kwamba yeye ndiye aliyepewa shahada ya Juu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa watu wengine (mbali ya mlalamikaji).

Kuvuruga amani na usalama wa jamii ni sababu nzuri ya kukataa dhamana iwapo itathibitisha hivyo. Kwa mfano katika kesi ya Mwita v. R. (1971 H.C.D. n.122). Mahakama Kuu yaliyakataa madai ya Jamhuri kupinga rufani kwa vile eti mrufani angepata nafasi ya kujilipiza kisasi dhidi ya mlalamikaji. Jamhuri haikutoa ushahidi kuthibitisha madai hayo ya kupinga dhamana. Aghalabu polisi hufanya hivyo kwa vile mashauri yao huyaanzisha kabla ya upelelezi kukamilika na ushahidi kamili kupatikana dhidi ya washitakiwa. Kwa bahati nzuri mahakama yanasisitiza kuwa hoja zote za kupinga maombi ya dhamana ziwe na ushahidi madhubuti au zitolewe kwa kiapo. Kwani endapo mahakama yatasikiliza na kuafikiana na madai, wasiwasi, na pengine hofu tu za waendesha mashitaka basi kutakuwa hakuna upeo wa madai hayo kiasi kwamba dhamana zitakataliwa kila wakati madai hayo yatakapotolewa.

Katika shauri la Bhangwanji Kakubhai v. R. ( T.L.R. 143) mrufani alipinga amri ya mahakama ya awali kumkatalia dhamana. Mrufani alikuwa ameshitakiwa kwa kosa la kuwa na dhahabu kinyume cha sheria. Upande wa mashitaka ulipinga dhamana kwa madai kuwa mshitakiwa alikuwa na nafasi na vielelezo ambavyo angeweza kuvitumia kuzuia kugunduliwa kwa biashara haramu ya dhahabu katika sehemu nyingine za Tanganyika. Yakikataa hoja hiyo Mahakama Kuu yalisema kwamba dai tu kuwa mrufani anazo habari na vielelezo ambavyo iwapo vitatumiwa vitavuruga upelelezi mzuri wa polisi ni la kinadharia mno, halieleweki na wala halitoshi kuwa sababu ya kumweka mrufani ndani wakati hakuna shaka yoyote kuwa atatoroka iwapo atapewa dhamana.

Mahakama hayo yalimaliza kwa kusema kwamba: "Sababu kuu ya kumtia mtu ndani ni kuhakikisha kuwa atahudhuria kusikiliza kesi dhidi yake. Sio sehemu ya sheria zetu kumweka mtu ndani kwa vile tu polisi hawapendi kuiona sura yake. (K.h.j). Hivyo kwa hakika hadi sasa suala kubwa kupita yote ambayo mahakama hujiuliza wakati wa kusikiliza maombi ya dhamana ni iwapo mwombaji atahudhuria kusikiliza shauri kila saa na siku mbele ya mahakama yanayohusika.

Masharti ya dhamana hutolewa na mahakama. Baadhi yake ni kuwa mshitakiwa aache hati ya kusafiria mikononi mwa polisi, kama anayo, pamoja na kuzuiliwa kutoka nje ya eneo maalum kama vile kijiji, mji na kadhalika. (F.148(6), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Mshitakiwa anaweza kupewa dhamana kwa uzito wa idadi ya wadhamini ambayo mahakama inaona inafaa.

Wadhamini hao wanatakiwa kuwa watu wenye kuaminika. Wanaweza kutakiwa walipe kiasi fulani mahakamani au watie saini mkataba wa kulipa kiasi fulani cha fedha iwapo mdhaminiwa atashindwa kufika mahakamani tarehe iliyopangwa. (F.151, Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Au mshitakiwa anaweza kujidhamini mwenyewe kwa kutia saini mkataba wa kufika mahakamani siku inayotakiwa. (K.h.j).

Kiwango cha fedha za dhamana hutegemea mazingira ya shauri lenyewe lakini hakitakiwi kuwa kikubwa mno. (F.148(2), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Mahakama ya rufani yanaweza kupunguza kiwango cha fedha ambazo zimetakiwa kama dhamana au kubadilisha masharti mengine yoyote yaliyotolewa na mahakama ya awali kuhusiana na dhamana. (F.149, Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j) Hii ina maana mshitakiwa anaweza kukata rufani ili apewe dhamana na Mahakama Kuu iwapo alinyimwa dhamana awali.

Mdhamini anaweza kujitoa kumdhamini mshitakiwa wakati wowote anapopenda kufanya hivyo mahakamani. Hali hiyo ikitokea mahakama yatamjulisha mshitakiwa atafute wadhamini wengine.

Mahakama ambayo awali yaliyakataa maombi ya dhamana yanaweza kuyakubali iwapo kutakuwa na sababu za maana za kufanya hivyo baadaye. Kwa mfano ikiwa upande wa mashitaka haupingi tena mshitakiwa hupewa dhamana, au pengine mshitakiwa ameweza kutimiza masharti ya dhamana yaliyomshinda awali kama vile kupata idadi ya wadhamini wanaoaminika au kima cha fedha kilichohitaijka. Na pengine dhamana hutolewa kwa vile sababu ambazo awali zilizuia dhamana kutolewa hazipo tena. Ikiwa mshitakiwa amewekwa ndani kwa kushindwa kutimiza masharti ya dhamana anaweza kuomba kupewa dhamana mara tu anapoweza kutimiza masharti hayo.

Kwa upande mwingine mahakama yanaweza kufuta dhamana yaliyompa mshitakiwa kama kuna sababu za maana za kufanya hivyo.

Mshitakiwa akitoroka mdhamini atafidia utoro huo kwa kulipa kiwango kilichokubaliwa na mahakama hapo awali. Dhamana kabla ya rufani zitajadiliwa katika matoleo yajayo.

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook