MUONGOZO WA KUNUNUA KOMPYUTA (3)

 

Tunaendelea na maelezo yetu juu ya mambo ya kuyaangalia unapotaka kununua kompyuta sasa hivi. Katika sehemu zilizopita tumezungumzia CPU, Motherboard na RAM. Kwenye sehemu hii tutaviangalia baadhi ya viungo muhimu ambavyo bado hatujavielezea.
 

Hard Disk Drive

Hard Disk Drive (HDD) ndiyo hifadhi kuu na ya kudumu iliyo kwenye kompyuta yako. Hii ni sehemu unayohifadhia operating system yako, programu mbali mbali unazozitumia, pamoja na mafaili yenye data mbali mbali.

Kwa ujumla kila HDD ikiwa na nafasi kubwa basi ndio vizuri zaidi. Kuna HDD zenye ukubwa mpaka wa kuzidi 13GB. Na kwa bahati nzuri bei ya HDD imepungua sana siku hizi, na hakuna tafauti kubwa kati ya bei za HDD za ukubwa mbali mbali. Kwa mfano, bei ya HDD ya ukubwa wa 4.3GB ni kama US$110 tu wakati ya ukubwa wa 13GB unaweza kuipata inayouzwa kwa bei ya US$250 tu. Napendekeza mtu anunue kompyuta yenye HDD ya ukubwa usiopungua 6.4GB.

Jambo la muhimu la kuliangalia ni watengenezaji wa HDD yako. Kuna baadhi ya watengenezaji wa HDD hawatengenezi HDD imara. Wanaotengeneza HDD imara ni pamoja na Western Digital, Quantum, na Maxtor. Kampuni ya Fujitsu, Samsung, na Hitachi, HDD zao si imara hata kidogo. Wauzaji kompyuta mara nyingi hukubambikia HDD za bei nafuu ambazo si imara, kwa hivyo ni muhimu kuuliza HDD yako imetengenezwa na nani. Jaribu kuomba kuwekewa HDD iliyotengenezwa na makampuni yaliyotajwa hapo juu yanayotengeneza HDD imara.

Ubora wa HDD si ukubwa tu bali pia kasi yake. Kuna mambo kadhaa yanayofanya HDD kuwa na kasi mbali mbali. Moja ni kasi ya mzunguko inayopimwa kwa RPM (revolutions per minute). Kuna HDD siku hizi zenye kasi ya mzunguko ya 10000RPM au zaidi ya hapo. Lakini HDD nyingi za kawaida zina kasi ya mzunguko ya 5400RPM ambayo kwa kweli si mbaya. Kila HDD ikiwa na kasi kubwa ya mzunguko ndivyo inavyotoa mvumo wa sauti kubwa zaidi unapoitumia kompyuta yako.

Kitu chengine kinachoamua kasi ya HDD ni aina ya kiungo (interface) kati ya HDD na na basi la data. Kwa siku hizi kuna viungo vya aina mbili: EIDE (Enhanced Integrated Drive Electronics) na SCSI (Small Computer System Interface) ambayo hutamkwa "skazi". HDD za aina ya EIDE ni za bei nafuu zaidi kuliko za aina ya SCSI. Ili kuweza kuitumia HDD ya aina ya SCSI huna budi kununua pia kadi inayoitwa SCSI controller. Kiungo cha aina ya SCSI kinaweza kutumiwa kusafirisha data kwa kasi kubwa sana mpaka kufikia 80 MBytes/second kwa kiungo cha aina ya Ultra-2 SCSI, wakati kasi ya juu ya kiungo cha EIDE ni 33.3 MBytes/second inayopatikana kama HDD yako inaweza kutumia kiungo kinachoitwa Ultra DMA/33. DMA ni ufupisho wa Direct Memory Access ambao ni uwezo wa HDD kuweza kuwasiliana na RAM bila kuhitaji udhibiti wa CPU. Kiungo kinachotumiwa na HDD za aina ya Ultra DMA/33 kinahimili kasi kubwa zaidi ya kasi ya kiungo kinachotumiwa na HDD za SCSI II chenye kasi ya juu ya 20 Mbytes/second.

Kama umenunua kompyuta yenye HDD kubwa, hakikisha kuwa HDD hiyo imefanywa kuwa na partitions kadhaa. Kama kompyuta yako inatumia Windows, kuwa na partitions kadhaa kunasaidia kunusuru kupotea nafasi kwenye HDD yako. Na faida nyingine ni kukusaidia kutoyaweka mayai yako yote kwenye mkoba mmoja! Partition moja ikiharibika unaweza kuwepo uwezekano wa kunusurika data zako zilizo kwenye partitions nyingine.
 

Monita

Monita ni kitu muhimu sana kwani ndiyo unayoiangalia wakati wote unapotumia kompyuta yako. Kila monita ikiwa kubwa ndio barabara. Kwa siku hizi usinunue monita iliyo na ukubwa wa chini ya inchi 15, lakini ni vyema zaidi kununua ya inchi 17.

 
 

 

Vitu muhimu vinavyotafautisha monita moja na monita nyengine ni pamoja na:

Ingawa unaweza kuona monita imesemwa kuwa ni ya inchi 17, sehemu ya kioo chake ambayo picha inaweza kuonekana ni ndogo zaidi ya hapo, pengine inchi 16 tu. Hiyo ndio huitwa viewable image size, kwa ufupi v.i.s, ambayo huwa tafauti kati ya monita na monita hata kama zinasemwa kuwa zote ni za ukubwa mmoja. Viewable image size hupimwa kimshazari (diagonally), na kila ikiwa kubwa ndio bara bara.

Kila monita imepakwa vidoto au mistari ya maadini ya phosphor yenye sifa ya kung’ara yanapogongwa na mionzi ya electrons. Monita za rangi huwa na phosphor za rangi nyekundu, kijani na buluu. Urefu kati ya vidoto au mistari ya phosphor ya rangi moja huitwa dot-pitch, kwa ufupi dp. Dot-pitch hupimwa kwa millimetre (mm) na kila dot-pitch ikiwa ndogo ndio picha inavyoonekana safi zaidi.

Tatizo ni kuwa baadhi ya watengenezaji wa monita hutumia udanganyifu wanapotoa ukubwa wa dot-pitch, na hii inasababishwa zaidi na njia mbali mbali zinazotumiwa kupima dot-pitch. Ikipimwa kimshazari (diagonal) dot-pitch huwa kubwa zaidi kuliko ikipimwa kwenye mstari uliolala (horizontal). Kwa mfano 0.28mm dp (diagonal) ni sawa na .25mm dp (horizontal). Kwa ujumla, hata hivyo, monita nyingi za siku hizi zinakuja na dot-pitch ya udogo wa kutosha kutoa picha nzuri. Dot-pitch ya kuanzia .28mm kujia chini inatosheleza haja. Na kwa kweli huwezi kuona tafauti kubwa kati ya monita ya .28dp na ya .25dp ingawa bei inaongezeka kila dot-pitch inapokuwa ndogo.

Resolution ya monita hupimwa kwa idadi ya pixels (picture elements) inazoweza kuzionesha kiupana na kwendea chini. Kila resolution inapokuwa kubwa ndivyo picha inavyoonekana safi zaidi. Kwa uzoefu wangu, resolution ya juu (maximum resolution) ya 1280x1024 inatosheleza kabisa.

Kawaida ya phosphor inapogongwa na mionzi ya electrons huwaka lakini baada ya muda mfupi huzimika. Inabidi ipitishiwe tena mionzi ya electrons ili iendelee kuwaka. Kama inachukua muda mrefu kupelekewa mionzi ya electrons monita inaweza kuonekana kama inapepesa. Refresh rate ni kipimo cha kuonesha ni mara ngapi kwa kila sekunde picha inachorwa upya kwenye kioo cha monita. Kila refresh rate ikiwa kubwa basi picha inaonekana safi zaidi. Refresh rate ya kuanzia 72Hz (non-interlaced) na kuendelea, inatosheleza kabisa.

Baadhi ya monita haiviwashi vidoto vyote vya phosphor kila mara bali huviwasha kwa kupishana. Yaani mkupuo mmoja inavichora vilivyo kwenye mstari wa kwanza, wa tatu, wa tano, n.k, na mkupuo wa pili inaviwasha vidoto vilivyo kwenye mstari wa pili, wa nne, wa sita, n.k. Mtindo huo unaitwa "interlacing". Monita zinazotumia "interlacing" si nzuri. Nzuri zaidi ni zile zinazoviwasha vidoto vyote kwa mkupuo mmoja, yaani non-interlaced. Refresh rate ya monita inategemea kama ni interlaced au non-interlaced. Kwa kutumia interlacing, vidoto vichache tu vinawashwa na kwa hivyo refresh rate inaweza kuonekana kubwa zaidi kuliko ile ya non-interlaced ambayo inawasha vidoto vingi zaidi, ingawa monita bora ni ile ya aina ya non-interlaced.

Mambo mengine ya kuangalia ni watengenezaji. KTX, AOC, Daytek, KDS, Goldstar, ni kati ya watengenezaji dhaifu wa monita. Monita madhubuti ni za Sony, NEC, Viewsonic, MAG, Hitachi, Digital, n.k. Watu wengi hupendelea monita zenye vioo bapa (flat screen) ambazo kwa bahati mbaya ni ghali zaidi. Na siku hizi pia monita zinazopendelewa ni zile zinazojuilikana kama short-depth monitors ambazo ni fupi na hazichukui nafasi kubwa kwa kwendea nyuma – yaani huwa na CRT (Cathode Ray Tube) fupi.

Lakini cha muhimu ni kununua monita ambayo ina sehemu za kurekebishia mambo mbali mbali ya picha inayoonekana kwenye kioo cha monita – mambo kama mwangaza (brightness), usafi (contrast), upana na urefu wa picha, n.k. Na zaidi, ni vyema kuchagua monita ambayo ina uwezo wa kutumia umeme wowote kati ya 110V na 250V yaani free voltage. Monita za namna hiyo ni muhimu kwenye nchi ambazo umeme unaongezeka na kupungua mara kwa mara.
 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook