DODOSO LA KUTAFAKARI
 
Ujinga unaudhia
 

Na Kipondo wa Changarawe

IMEKUWA ni mwenendo wa kawaida kwa watu walio wengi kumgeuzia hasira zao Mwenyezi Mungu kutokana na matatizo yanayowasibu. Wakikumbwa na ugumu wa maisha wanamlalamikia Mwenyezi Mungu, wakidhulumiwa wanamlalamikia Mwenyezi Mungu. Wengi wanaomlaumu na kumsingizia Mwenyezi Mungu tu bila ya kuangalia kwa kina chanzo na kiini cha matatizo yanayowakumba, badala yake wanamshupalia Allah (s.w.) wakati makosa ni yao.

Vitu vyote vilivyomo ulimwenguni wakiwemo wanyama na mimea makusudio ya kuwepo kwake ni kumnufaisha mwanadamu. Allah (s.w.) kwa ukarimu na rehma zake ameijaza dunia kwa neema zisizo hisabika za kila namna na za aina mbalimbali. Si mwingine bali ni mwanadamu aliyewekewa vitu vyote hivyo ili avitumie. Neema za Allah (s.w.) zimekuwa nyingi sana kiasi ambacho hata kama wanaadamu wote wangalikuwepo kwa wakati mmoja basi zisingalikatika. Lakini ni mpango wa Allah (s.w.) aliuweka kuwa kila watu wana kipindi chao maalum cha kupumua kwenye uso wa dunia.

Si uficho kuwa zipo kanuni na sheria za kimaumbile zisizotetereka ambazo huongoza utendaji kazi wa maumbile na vitu vyote kuanzia kile kilicho kidogo sana mpaka kile kilicho kikubwa. Cha kuzingatia hapa ni kwamba, hakuna mtaalamu yeyote yule katika wale waliobobea na asiye mushikeli wa akili atakayekuwa na ubavu wa kuutangazia ulimwenguni kuwa kanuni hizi za kimaumbile zimewekwa na mwanaadamu. Na akajitokeza mtalaamu wa sampuli hiyo basi ulimwengu wote utambeza na kumuona majinuni.

Ni dhahiri kwamba ataonekana kuwa ni kioja, atakuwa anaushangaza ulimwengu kwa sababu atakuwa amesema kitu ambacho akitohitaji watu kuwa razini sana ili wang'amue kuwa kilichosemwa ni kinyume cha ukweli ikiwa haingii akilini wala haikubaliki kwa mwanaadamu ambaye imekwishadhihirika kwamba anao uwezo wa kupanga, kuweka taratibu na kutengeneza vyenye manufaa vinavyofanya kazi kwa utaratibu kama vile Kompyuta, iweje ionekane kuwa ni usoni kukubali kuwa ulimwengu na vilivyomo pamoja na kanuni imara zinazouongoza kuwa ulitokea kwa bahati nasibu.

Upo uwezekano kuwa mtu anayedai kuipa kazi akili yake katika kuyachangua mambo anayoyasoma au kusomeshwa, akasoma na kuyapokea mabuku mengi pamoja na kuyahama madarasa moja baada ya jingine na akawa bado amefunikwa na giza la ujinga bila ya kuelimika, Hili litamtokea yeyote atakayezipumbaza fikra zake kwa kuamini kuwa kilichosahihi ni kile alichofundishwa na watu wa mtazamo fulani. Mtu wa namna hii anakuwa na akili za kushikiwa, maana kile kile alicholishwa ndicho ataking'ang'ania kuwa ni sahihi kwa sababu aliyesema ni Profesa au amemwona Profesa fulani akifanya jambo kadhaa.

Kutenda namna hii hakutoi tafsiri nyngine zaidi ya mtu kuthibitisha kuwa anaufanya ujinga wake kuwa ndio usomi. Katika hali hii mtu anafungika upande mmoja, fikra na akili zake haziko huru katika kuchambua na kufanya mambo. Hawa ni watu wasioelemika. Atafanya ambo mengi ya kipuuzi, ya kijinga na hata ya kuidhuru nafsi yake pamoja na jamii kwa sababu tu amewafanya akina fulani kuwa ndio vigezo vyake kinyume na mwongozo wa Muumba wake.

Kuna wengine wamesoma vilivyo sahihi, wanazitumia sana akili zao katika kuvichambua wanavyovisoma lakini wana tatizo linalowafanya wasitofuatiane na wajinga. Wao wanajua ubaya na uzuri wa jambo lakini wanatenda kinyume na ufahamu wao, hao nao wanakusanyika katika mkondo ule ule wa wasioelemika. Kwanini wasiwe miongoni mwa wasioelimika hali ya kuwa kiutendaji hawatofautiani na wajinga.

Yupo mwenzangu aliwahi kuonyesha masikitiko aliyonayo kwa kutumia maneno machache, alisema kuwa ' kujua ni kuhuzunika'. Nami Kipondo ninaungana naye kwa namna nyingine kwa anuani isemayo kuwa ujinga unaudhia. Ni udhia ikiwa msomi asiyeelimika anaugeuza ujinga wake huo kuwa ni usomi, kisha akatembea kwa kunata akiwa kifua mbele na kuvimba kichwa. Akawaona wanadamu wenzie kama mijusi ambao wanathamani ndogo mbele ya macho yake.

Ukiondoa Uislamu ambao ni utaratibu wa maisha unaotoka kwa Muumba wa ulimwengu na vilivyomo akiwemo mwanadamu, hakuna mfumo wowote wa maisha ulioipa elimu kipaumbele kinadharia na kivitendo kuliko ile hadhi na nafasi aliyopewa ndani ya Uislamu. Wakati njia nyingine za maisha zikimdogesha mwanadamu kwa madai kuwa ameibuka kutoka katika kizazi cha jamii ya manyani aliyozuka kwa bahati nasibu. Uislamu unamwelezea kuwa mwanadamu ni kiumbe bora aliyekabidhiwa jukumu la kuutawala ulimwengu na vilivyomo kwa kutumia mwongozo utokao kwa Muumba wake.

Kinyume na nadharia ya unyani ambayo inajitutumua bila ya mafanikio kuelezea eti mtu wa kwanza alikuwa mbumbumbu na mshamba hapa duniani, mwongozo wa maisha usio na shaka unatubainishia kuwa yule mtu wa kwanza alikuwa mweledi na mwenye hadhi kubwa hata mbele ya Malaika ambao kwa kuonyesha heshima na hadhi yake walimwinamishia 'vichwa' vyao. Kwa mujibu wa Qur'an, mtu wa kwanza alikuwa na elimu iliyozidi iel ya malaika. Hili linatokana ukweli kwamba alifundishwa elimu inayohusu tabia na namna ya utendaji kazi wa kila kitu (the nature of all things).

Tangu awali mwanadamu aliumbwa akiwa mtu kamili aliyepewa elimu iliyompa hadhi ya kuuweka ulimwengu kwenye kiganja cha mkono wake na kuvitumia vyote vilivyomo kwa manufaa yake ili aweze kuusimamisha ufalme wa Mwenyezi Mungu hapa duniani kama ilivyo mbinguni. Ukhalifa ndiyo istilahi inayotumika ndani ya Qur'an katika kuielezea dhamana hii adhimu aliyokabidhiwa kutawala ulimwengu kwa kutumia mwongozo wa Mola wake.

Nadharia inayosema kuwa Dunia haina Muumba inaonekana kuwaathiri wengi kiutendaji miongoni wanaoingia Makanisani na Misikitini. Haitakuwia vigumu kuwatambua wale wote walioathiriwa na kutekwa nyara kwa nadharia ya kumkana Muumba, utawatambua hata kama ni watu wanaoswali na kufunga au wanaoshiriki katika kumwimbia Bwana. Utawagundua tu maana mwelekeo wao, maneno na matendo yao yanatoa picha mbili zisizofautiana kabisa kana kwamba ni mapacha waliotokana na rutubisho la yai moja.

Huenda ikadhaniwa kuwa dodoso limekusudia kutoa mifano inayoachana kama mifano ile inayopigwa ya kuwafananisha Waislamu wanaotetea haki na kudai haki zao za kimsingi, kuwa ni wachochezi wanaopania kuvuruga amani. Wale walilotoa mifano kama ile iliyotolewa bungeni, mifano ya kuwalinganisha Waislamu wanaodhulumiwa haki za kikatiba na wale watu wa porini. Dodoso halitotumia mifano butu ya namna hiyo.

Nataka kutoa mfano hai unaoishi, mfano utakaokuonyesha na kukuthibitishia kuwa wengi miongoni mwa wanaoingia Misikitini na Makanisani bado wanamkanusha Muumba katika matendo yao na kwamba wanakubaliana na wale watu wanaompinga Mungu. Nao ni kwa namna gani wanakubaliana. Sasa tega sikio nikupe tamathali.

Kipondo nina marafiki zangu wanne ambao ni watu wa 'dini' kwelikweli hawakosi kuhudhuria katika majumba ya ibada, mara nyingi wanakwenda huko kufanya ibada ziwajengee mapenzi kwa Mwenyezi Mungu. Katika wale rafiki zangu wanne, wawili miongoni mwao wanakwenda Kanisani. Kwa unyenyekevu kabisa wanasema maneno yafuatayo:

Baba yetu uliye mbinguni, jina lako litukuzwe, Ufalme wako uje. Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni. Utupe leo riziki yetu. Utusamehe deni zetu kama nasi tuwasamehavyo wadeni wetu. Na usitutie majaribuni, lakini utuokoe na yule mwovu. (Kwa kuwa Ufalme ni wako, na nguvu, na utukufu, hata milele. Amina).

Na katika wale wanne, wale marafiki zangu wawili waliobaki ni wasalihina. Wanakwenda Msikitini mara tano kwa siku. Nao kwa unyenyekevu kabisa wanarukuu na kusujudu wakiongozwa neno 'Allahu Akbar' katika kuswali kwao wanalazimika kusema yafuatayo:

Kwa jina la Allah, Mwingi wa rehma, mwenye kurehemu. Shukrani zote njema anastahiki Allah, Mola wa walimwengu. Mwingi wa rehema mwenye kurehemu. Mwenye kumiliki siku ya malipo. Wewe tu ndiye tunayekuabudu, na Wewe tu ndiye tunayekuomba msaada. Tuongoze njia iliyonyooka. Njia ya wale waliwaneemesha, siyo ya wale waliokasirikiwa wala ya wale waliopotea. (1:1-7)

Baada ya sala zao, rafiki yangu mmoja kutoka Msikitini akakutana na mmoja wa Kanisani. Wote wawili wakaongozana kwenda mkutanoni huko wakutane na wale watu wanaompinga Mungu; matokeo ya mkutano wao ni mwongozo waliounda kwa pamoja ambao haukubaliani na sala ya Msikitini wala ya Kanisani. Maana sala zote mbili zinataka mwongozo wa Mwenyezi Mungu ndio uyaongoze maisha ya wanadamu.

Waliporudi kutoka mkutanoni wakakutana na wale rafiki zangu wawili ambao hawakushiriki kwenye kikao. Baada ya kuelezwa matokeo ya mkutano, wale wasiokwenda wakakubaliana na wakasema kuwa wao watabakia kuwa viongozi wa kiroho waongozao sala Misikitini na Makanisani. Wakafikia muafaka kuwa wote wataongozwa kwa kutumia mwongozo huo.

Huu ni mfano unaorandana na maisha yatu katika hali tunayokwenda nayo. Ni wazi kuwa wote tumekubaliana na hoja ya kibubusa kuwa ulimwengu huu hauna Muumba. Je, huo ufalme wa Mungu na mapenzi yake utakujaje duniani hali ya kuwa tunaongozwa kwa mawazo ya wale wanaompinga Mungu. Kweli inaingia akilini kuwa Mwenyezi Mungu aumbe ulimwengu na vilivyomo halafu atawale maisha ya watu wakiwa Misikitini na Makanisani na wakitoka humo waongozwe kwa matamanio ya watu wanaomkufuru na kumkanusha Muumba.

Na huko kuomba tuongozwe njia iliyonyooka kuna maana gani wakati umeshahiari kuwa matashi na matamanio ya nafsi, uzoefu pamoja na fikra za kudhani, kuwa ndiyo njia iliyonyooka tunayoiamini kivitendo. Ni upotevu gani tunaoomba tuepushwe nao wakati tumeshachagua kupotoka kwa kule kuzifanya fikra za wanaompinga Mungu kuwa ndiyo dira ya maisha yetu. Ni watu gani waliokasirikiwa na Allah (s.w.) kama siyo wale waliokubali kwa makusudi kuongozwa na vipofu wakati huo huo wanaomba waongozwe njia iliyonyooka.

Hivi ni ujinga wa kiasi gani kuamini kuwa Allah (s.w.) ambaye baada ya kuviumba, akaviwekea vitu vyote kanuni madhubuti za kufuatwa, lakini akaacha maisha ya kijamii yaendeshwe kiholela kwa namna mtu au kikundi cha watu kinavyotaka. Ikiwa mwanadamu hawezi akatengeneza kitu bila ya lengo na kikuacha kitumike bila ya kukiwekea mwongozo wa utumiaji wake, basi inakuwaje tukubali kirahisi kuwa Mwenyezi Mungu katuacha tuunde mwongozo wetu wenyewe wa maisha yetu. Je, tumejiumba wenyewe. Hivi ni kweli Allah (s.w.) mwenye hikma ameamua kuchea, akaumba bila lengo wala kuweka sheria au mwongozo wa kuiongoza jamii ya wanadamu.

Kanuni za kimaumbile zinakwenda sambamba na mwongozo wa maisha aliouleta Muumba kupitia kwa viongozi ambao ni Mitume aliewachagua miongoni mwa wanadamu. Kama ilivyo kwa kanuni za kimaumbile kwamba mwanadamu akijipa umwamba wa kuzikiuka basi zitamrudi, hali kadhalika mwanadamu asipofuata mfumo wa aliouweka Allah (s.w.) maisha atayaona kuwa machungu. Machungu yatakayomfika kutokana na kukiuka kwake utaratibu wa maisha unaokwenda barabara na kanuni za kimaumbile, hayo ni matokeo yaliyosababishwa na mikono yake mwenyewe na adhabu ya Allah (s.w.) bado inamsubiri.

Inajulikana fika kuwa moto ni wenye kuunguza, hilo halina pingamizi. Mtu akafahamishwa madhara ya moto kisha kwa hiari yake akajiuza, basi ile 'joto ya jiwe' atakayoionja ni matokeo ya kuutumikia ujinga wake. Sio siri kuwa zinaa ni kinyume cha utu na ubinadamu. Watakaofanya kuwa ndiyo starehe yao ya maisha wajue wazi kuwa kitakachowakuta ni matokeo ya kuyafanya matashi ya kinyama kuwa kiongozi wao. Vivyo hivyo, watu wanapoamua kujitungia au kutungiwa mwongozo ulio kinyume cha ule wa Muumba wao wanapaswa kufahamu kuwa kizaazaa kitakachowaandama ni matunda ya kazi iliyofanywa na mikono yao.

Leo hii tumewashikisha usukani matwaghuti wanaotukimbiza mchakamchaka, tena kwa kasi kubwa wanatuelekeza kwenye unyama, kwenye giza na kwenye moto. Ufalme wa Mungu pamoja na ukhalifa umepigwa marufuku usionekane kabisa katika viwanja vya uchumi, siasa na maisha ya kijamii, badala yake vimejengewa uzio Misikitini na Makanisani.

Matwaghuti wamepata wasaaa na uwanja mpana wa kuiharibu jamii, wanaujaza ulimwengu kwa mapombe ya kila aina, madawa ya kulevya, masinema ya kinyama, madanguro, magazeti ya kuchochea zinaa, mipira ya zinaa. Hawakuishia hapo, wanafanya kila jitihada za kuwashawishi watu wabobee kwenye machafu na maovu. Si mikanda ya video, si televisheni wala radio zote zimejaa ushawishi tu.

Sheikh, Padri, Mchungaji wanapewa vidakika vichache tu na wanatakiwa wazungumzie mambo ya kiroho. Kila unapogeuzia uso ni uozo na uvundo, ukitembea hatua tatu ni baa na walevi kibao. Basi kwanini rushwa isishamiri, kwanini huduma muhimu za kijamii zisipotee, kwanini maisha yasiwe magumu, kwanini vibaka wasiongezeke, kwanini wanawake wasishindane kuvua nguo zao, kwanini wachangudoa wasizidi, kwanini ndoa zisivunjike, kwanini watoto wa mitaani wasiibuke, kwanini magonjwa ya zinaa yasichukue nafasi yake na kwanini uchumi usishuke. Je, ikiwa tutamlaumu Mwenyezi Mungu tutakuwa tunasema ukweli. Au tukisema kuwa ni Allah (s.w.) ndiye aliyesababisha eti anatupima, hapo hatumzulii na kumsingizia. Si ni sisi wenyewe tumekubali kuuweka kando mwongozo wa haki na uadilifu aliotuletea, badala yake tukajifanya wajanja kuukumbatia utwaghuti na kuwapa nafasi ya Allah (s.w.) wale wasiozingatia mipaka ya Mwenyezi Mungu katika kuendesha maisha.

Dodoso lina huzuni kubwa sana,e ti nasikia kuwa kuna watu wanatangaza kuwa wao ni ummah bora, wanaamrisha mema na kukataza mabaya. Yako wapi hayo mema mnayoyaamrisha, mbona hayaonekani. Yako wapi hayo mabaya mnayoyakataza, mbona kila siku yanaongezeka. Na huku kusali kwetu, kufunga kwetu na kuhiji kwetu kinyme na malengo aliyoyaweka Allah (s.w.) tunadhani kuwa ukutatuingiza peponi. Ngoja tuzitafakari aya zifuatazo:

Mfano wa wale waliopewa Taurati, kisha hawakuichukua kwa (kuitumia) ni kama punda anayebeba vitabu vikubwa vikubwa. Ni m-baya kabisa mfano wa watu walizipinga aya za Mwenyezi Mungu; na Allah hawaongoi watu madhalimu. (62:5)

Je! Mnaamini baadhi ya kitabu na kukataa baadhi yake. Basi hakuna malipo kwa mwenye kufanya yaya kutoka ninyi ila fedheha katika maisha ya duniani, na siku ya kiyama watapelekwa katika adhabu kali. Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika na yale mnayoyatenda. (2:85).

Na atakayejitenga na mawaidha yangu, basi kwa yakini atapata maisha yenye dhiki, na siku ya kiyama tutamfufua hali ya kuwa kipofu. Aseme: Ewe Mola wangu! Mbona umenifufua kipofu, na hali nilikuwa nikiona. Allah atasema: Ndivyo vivyo hivyo zilikujia aya zetu ukazisahau na kadhalika leo utasahaulika. (20:124-126)

Sema: Je! Tukujulisheni wenye hasara katika vitendo vyao? Hao ni wale ambao bidii yao hapa duniani imepotea bure katika miasha ya dunia, nao wanafikiri kwamba wanafanya matendo mema. Hao ni wale waliokataa mwongozo wa Mola wao na wakakataa kukutana naye. Kwa hiyo vitendo vyao vimeruka patupu wala hatuwazidishii mizani siku ya kiyama. (18:103-105)
 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook