Wanafunzi Waislamu wanyanyaswa ndani ya shule ya Waislamu
 

Na Mwandishi wetu, Mwanza

IMEELEZWA kwamba wanafunzi Waislamu wa shule ya Taq'wa wamekuwa wakinyanyaswa na uongozi wa shule kinyume na matarajio ya wazazi na wanafunzi.

Katika tukio la hivi karibuni imedaiwa kwamba Mwalimu Mkuu Msaizidi aliye Mkatoliki aliwazuia wanafunzi kwenda kuswali Ijumaa.

Taarifa ya umoja wa wanafunzi Tanzania - TAMSA tawi la Mwanza imeeleza kuwa mwalimu huyo aliye na uhusiano mzuri sana na shirika la Kikatoliki la Josuits Fathers Nyakahoja siku ya tukio aliwaambia wanafunzi Waislamu; "Leo Ijumaa hakuna kuswali; kwani mkiacha leo tu mtakuwa na nini".

Aidha, imeelezwa kwamba mwalimu huyo amekuwa na tabia iliyokubuhu ya kuwafunua skafu wasichana kwa kisingizio cha kukagua nywele.

Wakati huo huo, Sheikh Mkuu wa Msikiti wa Ijumaa Sheikh Jabir Katura amekanusha vikali tuhuma zilizotolewa na baadhi ya Waislamu waliotaka kujua utaratibu unaotumika kuwapata vijana wa kwenda kusoma Afrika Kusini. Waislamu hao walidai kuwa nafasi hizo zinatolewa kwa upendeleo bila kuzingatia sifa za walengwa.

Tuhuma hizo zilitolewa baada ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Msikiti wa Ijumaa Alhaj Sherali Hussein Sherali kutangaza Msikitini kuwa taasisi ya kidini Afrika ya Kusini imetoa nafasi tano (5) kwa vijana wa Kiislamu kwenda kusoma kila mwaka kutoka mkoani Mwanza.

Sheikh Jabir aliwataka Waislamu kuacha tabia ya kudhania vibaya viongozi wao, ni muhimu wakafanya uchunguzi kwanza kabla ya kuwatuhumu.

Alisema kama kuna Muislamu anamjua kijana aliyepelekwa huko bila sifa amtaje hadharani; kwani nafasi zilizotolewa ni kwa ajili ya Mahafidhil-Qur'an tu ambao tayari wameshafahamishwa jambo hilo tayari kwa safari.

Mwanza kipo kituo cha kuhifadhisha Qur'an inasemekana kimeshahifadhisha Qur'an vijana wanne. Kwa maelezo ya viongozi zipo nafasi tano na atatakiwa kijana mwingine wa kujaza nafasi hiyo na labda ndiyo maana Sheikh Jabir alitoa wito kama kuna Muislamu anamfahamu kijana ambaye ni hafidhi ampeleke kwake.

Watu walioongea na gazeti hili baada ya maelezo ya Sheikh waliulaumu uongozi kwa kuwa wasiri na kujenga mazingira ya tuhuma kwani kama sifa za walengwa zingetajwa sambamba na kutangazwa kwa nafasi, mwanya wa tuhuma usingekuwepo kwani mahafidhi wa Qur'an ni wachache na wanajulikana.

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook