HABARI zilizoandikwa katika ANNUUR toleo Nam. 196, la Aprili 9-15, kwamba huenda tarehe 21 Aprili, 1999 F.F.U ikatumika kuwafukuza Waislamu katika Masjid Mwinyi, na kumkabidhi Msikiti huo Bw. Daniel Zakaria anayedai kuwa hiyo ni sehemu ya mirathi yake, zinastusha sana, siyo kwa Waislamu tu; bali kwa kila yule anayeshimu uhuru wa kuabudu, haki za binadamu na utawala wa sheria. Kwa Waislamu, Msikiti si nyumba ya kufanyia ibada tu bali ni nyumba ya Mungu. Hii ina maana kwamba Muislamu aliyeamua kuitoa nyumba yake igeuzwe Msikiti au alitoa kiwanja chake kijengwe Msikiti, basi tokea siku ya uamuzi wake huo, nyumba hiyo au kiwanja hicho vinakuwa si mali yake tena. Ni mali ya Mungu.
Kwa lugha nyingine Muislamu aliyeamua kuigeuza nyumba yake iwe Msikiti huwa ameiweka Wakfu, au kwa msamiati wa kileo ameitaifisha kwa maslahi ya Waislamu wote. Haki miliki hutoka mikononi mwa huyo mwenye nyumba na kwenda kwa wadhamini wa huo Msikiti. Kwa hivyo, baada ya hapo si yeye wala warithi wake wenye haki ya kimiliki jengo hilo.
Kuhusu Masjid Mwinyi, mbali ya ushahidi wa kimaandishi aliouacha marehemu Hajat Aziza pia kuna ushahidi wa kimazingira unaoonyesha waziwazi kuwa marehemu aliitoa nyumba hiyo iwe ni Msikiti na Wakfu. Akiwa hai alishiriki katika ujenzi wake, ufunguzi na hata katika kutoa jina la Msikiti huo. Umeitwa Masjid Mwinyi kwa maana ya kwamba Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi ndiye aliyealikwa kuufungua rasmi. Marehemu alipofariki dunia alisaliwa hapo na waumini wa Msikiti huo huo, kwa kufuata mila na desturi za Kiislamu.
Hakuna ushahidi wowote wenye kuonyesha kuwa marehemu katika uhai wake alikuwa akipokea kodi kutoka kwa waumini wa Msikiti huo. Kama katika dini nyingine nyumba za ibada hukodiwa au hukodishwa, katika Uislamu, Misikiti haikodiwi na wala haikodishwi. Haijawahi na wala haitawahi kutokea Muislamu ajenge Msikiti kwa nia ya kuukodisha kwa Waislamu wenziwe.
Kila Muislamu anayejenga Msikiti uwe ni mdogo au mkubwa, wa gharama kubwa au nafuu, hukusudia uwe ni wakfu. Na kwa mujibu wa sharia ya Kiislamu Wakfu haurithiwi wala hauuzwi. Kwa hivyo, ni wazi kuwa marehemu Hajat Aziza bint Omar ambaye mpaka wakati wa kifo chake alikuwa ni Muislamu. Wala hakuna sababu ya kuamini vinginevyo!
Mbali ya michango inayotolewa na waumini, mara nyingi, Misikiti huwa haina vyanzo vingine vya mapato isipokuwa labda Msikiti kama huo uwe una nyumba ya wakfu. Waislamu wengi wanaojenga Misikiti hutoa na nyumba zao nyingine ziwe ni wakfu wa Misikiti hiyo, zipangishwe, ili kodi inayopatikana itumike katika kulipia gharama za uendeshaji wa Misikiti hiyo.
Marehemu Hajat Aziza alitoa nyumba zake mbili Wakfu kwa ajili hiyo hiyo. Alifanya hivyo kwa maandishi mbele ya vyombo vinavyokubalika kisheria. Na upo ushahidi wa maandishi kuthibitisha hayo.
Huwaje basi baada ya kifo cha marehemu huyo watokeze watu kama Bw. Daniel Zakaria na kundi lake watumie ujanja wanaoufahamu wao wenyewe, kudai kuwa ati Msikiti huo pamoja na hizo nyumba za Wakfu ni mirathi yao; na kisha vyombo vya sheria vikubali kuwarithisha?
Kwa mujibu wa sheria mtu hawezi kugawa mali asiyoimiliki. Anayetaka kugawa kitu chochote kumpa mtu mwingine ni lazima kwanza ithibitike kuwa kitu hicho kinamilikiwa kihalali na huyo mwenye kutaka kukigawa.
Kwa mfano, mtu alikuwa akimiliki gari, kisha akaliuza na kuna ushahidi wa maandishi kuthibitisha uuzaji huo. Baadaye mtu huyo akamwandikia mtu mwingine kuwa amemzawadia gari lile lile. Je! Gari hilo litakuwa ni mali ya nani; yule aliyeuziwa au huyu wa pili aliyezawadiwa? Bila shaka yoyote kwa mujibu wa sheria, gari hilo litakuwa ni mali ya yule mtu wa mwanzo aliyeuziwa.
Hiyo ni kwa sababu wakati wa kuuza gari hilo lilikuwamo kihalali katika milki ya muuzaji lakini alipotoa zawadi hakuwa akilimiliki kihalali. Kwa vile alikuwa amekwisha liuza, alikuwa hana haki ya kuligawa.
Na hivyo ndivyo ilivyo kwa nyumba za Wakfu. Kama tulivyotangulia kuona kuwa Muislamu anapotoa nyumba yake iwe ni wakfu kwa Msikiti fulani; basi hapo hapo milki ya nyumba hiyo hutoka katika milki yake na kuingia katika mikono ya wadhamini wa Msikiti unaohusika. Kwa ajili hiyo, mwenye hiyo nyumba huwa hana tena haki ya kuiuza au kuigawa nyumba hiyo kwa mtu mwingine yeyote. Na anapofariki warithi wake wanakuwa hawana haki yoyote ya kuirithi. Hii ndiyo maana ya wakfu katika Uislamu. Vipi basi Bw. Daniel Zakaria na wenziwe wapewe haki ya kurithi kitu ambacho hata huyo marehemu wanayedai kuwa ndiye wanayetaka kumrithi hakuwa akikimiliki baada ya kwisha kukitoa kiwe ni wakfu?
Aidha, Bw. Daniel hajamhusu marehemu ndewe wala sikio. Hawakuwa na uhusiano wowote si wa damu wala wa ndoa. Vipi basi amrithi? Isitoshe kwa mujibu wa sharia ya Kiislamu watu wenye imani tofauti hawarithiani hata kama wana uhusiano wa damu. Marehemu alikuwa ni Muislamu na Bw. Daniel ni Mkristo; itakuwaje Mkristo amrithi Muislamu?
Hivi juzi nilisoma katika gazeti fulani kuwa Jaji Msumi alikataa kumrithisha Muislamu kwa sababu alikuwa ana dini tofauti na marehemu. Kumbe hata hizi mahakama zetu zinatambua kuwa Waislamu hawarithiani na watu wa dini nyingine? Mbona Bw. Daniel ambaye ni Mkristo anarithishwa mali ya Muislamu? Kulikoni!
Mimi si mjuzi wa mambo ya sheria, wala sielewi mahakama zinatumia vigezo gani katika kutoa maamuzi yake. Lakini naikumbuka kadhia moja iliyotokea Kenya katika miaka ya themanini. Wakili mmoja maarufu wa kesi za jinai aliyekuwa akiitwa Otieno, ambaye alikuwa ni Mjaluo alioa mwanamke wa Kikuyu, akazaa naye. Alipofariki ulitokezea ubishi juu ya nani mwenye haki ya kumzika.
Mke wa marehemu pamoa na wanawe walitaka wapewe wao haki ya kumzika, kwa vile alikuwa ndiye mkuu wa familia yao. Na upande wa ndugu zake marehemu walitaka wapewe wao maiti hiyo kuizika, kwa sababu marehemu alikuwa ni ndugu yao wa damu katika ukoo, na pia ni Mjaluo kwa hivyo waliona lazima azikwe kwa desturi na mila za kabila lao.
Jopo la Majaji watatu likaamua kuwa kwa mujibu wa sheria za kienyeji (Customay Law); kwa vile marehemu alikuwa ni Mjaluo, na katika uhai wake alikuwa akishiriki katika mila na desturi za kabila hilo, basi azikwe na ndugu zake kwa kufuata desturi na mila za Kijaluo.
Swali la kujiuliza ni kwamba ikiwa mahakama zinaweza kukubali mila na desturi za watu wa kabila fulani, kwa nini mahakama hizo hizo zikatae kukubali mila na desturi za Kiislamu? Katiba ya nchi inamhakikishia kila raia kuwa na uhuru wa kuabudu, maadamu havunji sheria. Katika dini ya Uislamu mirathi ni sehemu ya sheria ya dini hiyo. Kwanini basi vyombo vya sheria viingilie taratibu za mirathi ya Kiislamu? Kufanya hivyo si kuwaingilia Waislamu katika uhuru wao wa kuabudu?
Pili, katika misingi ya haki za binadamu, ni mtu kumiliki mali alizozichuma kihalali, pamoja na kuzitumia mali hizo jinsi ya vile apendavyo.
Marehemu Hajat Aziza alimiliki nyumba tatu, katika uhai wake. Alipenda nyumba moja aigeuze kuwa Msikiti na mbili zilizobaki ziwe wakfu kwa ajili ya kugharamia uendeshaji wa Msikiti huo. Amebainisha azma yake hiyo kwa maandishi mbele ya vyombo vya sheria. Kwa nini vyombo hivyo vya sheria haviheshimu haki ya marehemu ya kuitumia mali yake vile alivyoagiza mwenyewe? Je! Huo si uvunjaji wa haki za binadamu?
Mimi ni katika wale wanaothamini uhuru wa vyombo vya sheria na ninaviheshimu sana. Sipendi viingiliwe na chombo kingine chochote katika utendaji wake. Lakini inapotokezea vyombo hivyo kutoa maamuzi yenye kutatanisha kiasi cha kwamba jamii ihisi kuwa haki haikutendeka, nini cha kufanya?
Hivi karibuni Jaji Mkuu Mheshimiwa Nyalali aliingilia kati maamuzi yaliyotolewa na Hakimu wa Mahakama moja aliyemhukumu kifo mbwa kwa kuitwa Immigration. Baada ya vyombo vya habari kutoa taarifa za kulaani hukumu hiyo ilimbidi Jaji Mkuu aingilie. Je, kama kweli kuna mahakama iliyompa kibali Bw. Daniel auchukue Masjid Mwinyi na nyumba za Wakfu kwa kuwa ni sehemu ya urithi wake hakuna haja hapo ya Jaji Mkuu kuingilia kati hukumu hiyo?
Je, serikali haioni kuwa
kuna haja ya kutumia taratibu za kisiasa kutatua mgogoro huo; ili kuiokoa
amani ambayo inaonekana iko katika njia panda?
|
|