MAKALA
 
Kwanini tusisali Idd siku moja? (Jibu)
 

Na Bisura Waziri Nyello

MAKALA iliyoandikwa na Maalim Bassaleh katika ANNUUR No. 196 la Aprili 9-15, 1999 kuhusiana na hoja iliyotajwa hapo juu imejenga msingi mzuri wa majadiliano. Kumbe watu wengi wanakerwa na hali hii ya aibu ya kutofautiana katika kufunga na kuswali Idd. Dini yetu ni moja, Mtume wetu ni mmoja, kitabu chetu kimoja, Qibla chetu kimoja, na tunaswali namna moja. Kwanini tusisali Idd pamoja?

Kabla ya kuanza kuijadili hoja hii ya Maalim Bassaleh ningependa kutanguliza aya zifuatazo za Mwenyezi Mungu: "Kwa yakini huu ummah wenu ni ummah mmoja na mimi ni Mola wenu (mmoja), kwa hiyo niabuduni".

Mwenyezi Mungu anatuangalia Waislamu kama watu wa ummah mmoja. Uislamu hauna mipaka ya kijiografia, kitaifa wala kikabila. Ibada zote za Kiislamu zimelengwa kwa Waislamu wa ulimwengu mzima. Ndiyo maana Waislamu wote duniani wana lugha inayowaunganisha katika ibada zao. Hata ukiwa Uchina hutasikia adhana wala Fatiha ya Kichina!

Maalim Bassaleh anasema katika hoja yake kwamba: "Sala ya Idd ni sunna, lakini umoja wa Waislamu ni wajibu. Sisi tumeacha kulishughulikia lile jambo la wajibu, ambalo ni umoja wa Waislamu na kuamua kutoafikiana katika kusali sala ya Idd siku moja bila kuwa na sababu ya msingi".

Ni kweli sala ya Idd ni Sunna na umoja wa Waislamu ni faradhi. Na sunna inaweza kuvunjwa kwa ajili ya faradhi katika Uislamu lakini tatizo ni kwamba sababu gani inayotufanya tuivunje sunna? Kwa sababu sunna ili iwe sunna lazima itekelezwe kwa mujibu wa taratibu zake. Huwezi kuivunja sunna tu kienyeji kwa sababu inavunjika.

Kama Waislamu wameelekezwa kuswali Idd - El- Hajj siku ya pili baada ya Arafa kwanini sisi tuswali siku ya tatu? Huo umoja Maalim Bassaleh utakuwa ni wa Kiislamu au wa kitaifa?

Mwandishi amenukuu Hadith ya Mtume (s.a.w.) kutoka katika Bukhari na Muslim inayosema kwamba: "Akijitahidi mwanazuoni akasibu basi atapata malipo mara mbili. Na akijitahidi akakosea basi atapata ujira mara moja". Ametumia Hadith hii kuonyesha kwamba kila jambo Allah hutazama nia ya mtendaji na wala siyo jambo lililotendwa. Kama nia ni kumtii Allah basi jambo hilo hukubaliwa, la, kama nia nia ni nyingine basi hukataliwa. Kisha mwandishi akashauri: "Basi na sisi hata kama tutahitilafiana katika siku ya kwanza kufunga na kufungua Ramadhani, na pia katika siku ya kufunga Arafa, Mwenyezi Mungu atatulipa kwa mujibu wa nia zetu na ijitihada za wanazuoni wetu. Haidhuru huyu amefuata Saudi Arabia na mwingine amefuata mwezi ulioandama katika nchi yake".

Ibada zote za Kiislamu zina malengo maalumu. Ukamilifu wa malengo hayo ndiyo mafanikio ya mwenye kufanya ibada hizo (Waislamu). Lakini Waislamu tusipigane kupata thawabu bila ya kuzingatia lengo kuu la ibada zenyewe.

Mwenyezi Mungu anaposema: "Enyi mlioamini! Mmelazimishwa kufunga swaumu kama walivyolazimishwa waliopita kabla yenu ili mpate kumcha Mungu", anatufundisha kwamba lengo kuu la swaumu siyo kupata thawabu bali kutuandaa kuwa wacha Mungu. Mwenyezi Mungu atazikubali funga zetu baada ya kufikia lengo hili. Huku kutofautiana kwetu katika kufunga na kufungua, pamoja na Arafa kunatutoa nje ya lengo la ibada hizo.

Kwa Waislamu ni haramu kula mchana wa Ramadhani na kufunga siku ya Idd. Huku kupishana kwetu siku moja kunasababisha watu wale katika mchana wa Ramadhani na wafunge siku ya Idd!

Swala ya Idd El Hajja ni miongoni mwa sunna zilizokokotezwa. Swala hii kama ilivyo swala ya Idd El Fifri huswaliwa katika kipindi cha baada ya jua kuchomoza na kabla ya jua kuwa katikati. Mara nyingi huswaliwa kati ya saa moja na saa tatu asubuhi. Mtume (s.a.w) aliletewa habari mchana kwamba mwezi ulionekana jana yake. Kwa hiyo Mtume (s.a.w.) akaamrisha Waislamu wote wafungue ili kukwepa kufunga siku ya Idd, na kuwa muda ulikwishapita (asubuhi) akawaambia watasali Idd siku ya pili. Hiyo ni sababu nzito kabisa ya kuahirisha sala ya Idd.

Lakini sisi tunaahirisha swala ya Idd kwa lengo la kuvunja umoja na mshikamano wa Waislamu kimataifa. Hiyo ni sababu nzito? Maalim Bassaleh anasema: "Inavyopendeza Waislamu wote ulimwenguni wafunge na wafungue Ramadhani siku moja na pia wafunge Arafa siku moja".

Idd el Hajj ni ibada kubwa ya sunna inayoambatana na ibada ya Hijja kwa ulimwengu wote wa Waislamu. Katika siku hii Waislamu wote katika pembe zote za dunia hujiunga (kihisia na kiroho) na Waislamu wenzao walioitwa na kuitikia mwito wa Allah (s.w.) wa kwenda kutekeleza ibada ya Hijja. Moja ya lengo na mafunzo muhimu ya ibada ya Hijja ni kujenga udugu, umoja na mshikamano wa kweli wa Waislamu wote ulimwenguni. Ibada hii ni kielelezo cha umoja wa Kiislamu usiojali mipaka ya kijiografia, rangi, kabila, utaifa wala jinsia.

Ikumbukwe kuwa baada ya Waislamu kuporwa E.A.M.W.S. na kuundiwa Ma-Bakwata bila ya ridhaa yao, kazi iliyofuata ilikuwa kuwatenganisha Waislamu wa Tanzania na wenzao ulimwenguni kote. Bakwata ikapewa ukiritimba wa kusimamia shughuli zote za Waislamu nchini. Wanachosema wao basi huonekana kama ibada kwa Waislamu wa Tanzania. Ndiyo maana hutosikia hata siku moja Bakwata ikilaani mauaji ya Waislamu Kosovo, Bosnia au Algeria. Huko kote mbali, Mwembechai tu wanashindwa! Kwa hiyo namuomba Sheikh Basaleh asiutilie tashdidi umoja wa Kibakwata.
 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook