HABARI ZA NDANI
 
Wanawake wa Kiislamu Moshi:
Waazimia kuanzisha harakati za ukombozi
 

Na Ashraf Yussuf, Moshi
 
WANAWAKE wa Kiislamu mkoani Kilimanjaro na Arusha wameazimia kuanza upya harakati za kudai haki za Waislamu nchini kama ambavyo walivyoshiriki kupigania uhuru wa nchi hii.

Wamesema pamoja na kushiriki kwao katika kuupigania uhuru na kuwa chimbuko la Jumuiya ya kwanza ya kinamama katika siasa, bado haki za wanawake Waislamu na Waislamu kwa ujumla zinahujumiwa kinyume na Katiba ya nchi.

Aidha, wameungana na wenzao kuitaka serikali kuwafichua wale wote walioshiriki mauaji ya Waislamu na madhila mengine kwenye Msikiti wa Mwembechai mapema mwaka jana.

Hayo yalikuwemo kwenye tamko la wanawake hao mwishoni mwa kongamano la siku mbili lililofanyika hivi karibuni katika Msikiti wa Riadha Moshi mjini.

Katika tamko hilo wameshangazwa sana kuona idadi kubwa ya polisi ikimwagwa Ngorongoro kuwasaka majambazi waliomuua Ofisa wa Polisi wa Wilaya, huku polisi ikiahidi kuwapata wakiwa hai au wamekufa, lakini mauaji ya Mwembechai hayashughulikiwi.

Walisema hakuna subra katika hili na wakaitahadharisha serikali juu ya kupuuza madai yote ya Waislamu na wakaelezea hofu yao juu ya kupuuzwa huko.

Bi Amina wa Arusha akielezea malalamiko hayo ameikumbusha serikali mchango mkubwa wa wanawake wa Kiislamu kwa nchi hii katika kuleta uhuru na baada ya uhuru. Kutokana na kudhalilishwa kwa wanawake na mauaji hayo, ameonya uwezekano wa kusimama tena kidete kudai haki za Waislamu kama zilivyohakikishwa kwenye Katiba ya nchi pindi kupuuzwa kwa madai hayo kukiendelea.

Akinamama mbalimbali waliochangia mada katika kongamano hilo, walitoa mapendekeo na maazimio tofauti kwa serikali na akina mama wenzao wa Kiislamu.

Mchangiaji wa kwanza aliwataka wazazi wa Kiislamu kupunguza kasi ya kuenea kwa maovu kwa kuwashonea watoto wa kike mavazi ya stara (hijab), kwani kutembea uchi kwa watotow a kike kunachangia sana kueneza zinaa.

Bi Twaiba Shaaban aliwataka Waislamu wote kufuata na kusoma Qur'an kama inavyotakikana na kupiga vita matumizi mabaya ya Qur'an kama vile kuandikia kombe, hirizi na kutundika milangoni, jambo ambalo ni kinyume na mafundisho ya Qur'an.

Mtoa mada kutoka mkoa wa Arusha ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja alilitaka jeshi la polisi nchini kuacha mara moja tabia ya kuwakamatakamata viongozi wa Kiislamu na kuwapachika kesi za uchochezi, jambo ambalo alisema linazidisha chuki katika misingi ya imani baina ya Waislamu na wasiokuwa Waislamu.

Alisema chuki za kidini nchini zimefikia mahali pabaya kabisa, hivyo akaitaka serikali kulinda kwa nguvu zote uhai wa Sheikh Ponda Issa Ponda ili isije ikawa hadithi ya "alikuwa na shinikizo la damu au kisukari hivyo ametutoka ghafla", alisema kwa jazba dada huyo wa Arusha huku akipokewa na Takbir.

Tukio lililotia fora zaidi ni kanda ya video ya mauaji ya Mwembechai ilipoanza kuangaliwa na akinamama waliofurika kila pembe ya Msikiti wa Riadha, kwani walianguka vilio vya aina yake na huku wakipandwa na jazba, ndipo mmoja wao akasimama ghafla na kusema; "mauaji ya Mwembechai ni unyama, tuyaalani wanawake wote nchini".

Baada ya kufoka kwa dakika kadhaa na kuwaliza wenzake aliwaulizia kwa kusema "tuko tayari kwa lolote iwapo manyanyaso ya aina ile yatapuuzwa na serikali.

Katibu wa wanawake wa Kiislamu mkoa wa Kilimanjaro Mama Aslam Aloo alihitimisha tukio hilo la kongamano la kihistoria hapa mkoani Kilimanjaro na Arusha kwa kuwapongeza wanawake wote walioshiriki na kuwaeleza kuwa malipo yao yako kwa Allah (s.w.) kwani wameonyesha ushujaa kwa sababu hawakuchelea mtu bali Allah (s.w.) hivyo wazidishe ushirikiano na mshikamano ili kujenga umoja baina yao ili kuwashinda madhalimu.

Pamoja na mada mbalimbali pia palikuwa na maonyesho ya mauzo ya bidhaa mbalimbali. Kabla ya kufunga shuhguli, iliundwa Kamati ya kinamama kuwaunganisha wanawake wa Kiislamu kutoka Moshi, Arusha na wilaya ya Boma ng'ombe na Masama Mudio ili kuratibu mijumuiko ya aina hiyo mara kwa mara na kila itakapohusu jamii ya Kiislamu Kilimanjaro na Arusha na Tanzania kwa ujumla.


Ijue Madrasat Maarifat - Al-Islamiyah, Moshi
  Na Ashraf Yussuf, Moshi

MADRASAT Maarifat-L-Islamiyah ni moja kati ya Madrasa mpya hapa mjini Moshi ambayo ipo eneo la Njoro-Makaburuni. Ilianzishwa mwaka 1995, mwalimu muasisi akiwa Ustadh Abubakar Salim Rashid, akiwa na wanafunzi wasiopungua mia na ishirini.

Madrasat Maarifat L-Islamiyah ni moja ya madrasa inayofanya vizuri katika mashindano ya Qur'an katika sehemu mbalimbali hapa Moshi mjini na mkoa wa Kilimanjaro, masomo yanayofundishwa katika madrasa hii ni pamoja na Qur'an, Lugha, Fiqh, Hadith, Sira, Tawheed na Nahau.

Madrasa ina vitengo vitatu ambavyo ni kitengo cha wanafunzi kutoka mashuleni na sehemu mbalimbali ili kupata elimu ya dini, kitengo cha kinamama na kitengo kuhifadhi Qur'an tu kila siku isipokuwa siku ya Ijumaa. Malengo ya baadaye ya madrasa hii ni kujenga jengo kubwa zaidi katika eneo lililotolewa na mfadhili mmoja aitwaye Bw. Mruma ili kukidhi idadi kubwa ya wanafunzi waliopo katika madrasa hii kwa sasa.

Lengo jingine kubwa ni kuanzisha shule ya watoto wadogo (Nursery School) ya Kiislamu baada ya kukamilisha nyumba ya mwalimu wa madrasa ambaye ni mkombozi wa eneo hilo la Njoro Makaburini. Madrasat Maarifat L-Islamiyah imeanzishwa mwaka 1995 lakini imeshaanzisha tawi jingine eneo la Msaranga karibu na Kiborloni hapa Moshi Mjini.

Madrasa inakabiliwa na matatizo lukuki yakiwemo ajira isiyo ya uhakika kwa mwalimu ikiwa ni pamoja na wazazi kutojali ada na umuhimu wake kwa wanafunzi ambapo wengi huchelewesha au kutolipa kabisa.

Aidha, madrasa hi inafundishwa katika mazingira magumu kwani wanafunzi hawana madawati bali hukaa chini ukizingatia mvua nyingi za Moshi zilivyo kero kubwa kwa tope.

Pia Ustadh Abubakar ametoa wito kwa Waislamu ndani na nje ya nchi kuisadia madrasa hiyo madawati na kujenga madrasa ya kisasa ili kwenda sambamba na karne ya 21 Kiislamu kwa matendo na sio maneno tu.

Aidha, Ustadh Abubakar amerudia wito wa Sheikh wake mkuu, Sheikh Ramadhani Hamza Mzonge wa kuwataka waalimu wote wa Madrasa nchini kote kutopoteza nguvu nyingi kwa kuwahifadhisha wanafunzi kaswida na milango ya maulidi na badala yake wapoteze nguvu nyingi kuwahifadhisha Qur'an kwa manufaa ya Uislamu na Waislamu hapo baadaye.
 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook