Kama nilivyoahidi katika toleo lililopita, endelea kufuatana nami katika sehemu ya tatu ya mada hii, uzidi kuona mtiririko wa sifa kuu nyingine zaidi zinazodhihirisha kwa uwazi zaidi ukweli kuhusu majina ya Allah na Yehova, kwamba ni majina yanayomhusu Mwenyezi Mungu yule yule mmoja aliyejitambulisha au kujifunua kwa Manabii wake mbalimbali kwa majina tofauti. Pia kutokana na uchambuzi huo, upate kuona kama kweli Yehova ndiye Mungu wa Wakristo?
Uweza (Hashindwi na chochote)
Kwa kuzingatia ukubwa wa uzito wa kazi ngumu ya kuumba na kuendesha kwake ulimwengu na vyote vilivyomo ndani yake, na pia kufanya kwake mambo mengi ya ajabu yaliyo nje ya upeo wa ufahamu, maarifa na ujuzi wa viumbe vyote, hapana shaka sifa kuu ya nne ya Mungu wa kweli ni lazima iwe ni Uweza wa kila kitu. Kwa mantiki hiyo, sifa hii pia ni kigezo kingine muhimu kinachoweza kuwa hoja ya msingi ya kutofautisha Allah na Yehova iwapo tu itabainika kuwa mmoja wao hana sifa hiyo. Hata hivyo, tusomapo maandiko ya Qur'an tukufu na Biblia takatifu tunaona mwenye sifa hiyo ni Mwenyezi Mungu mmoja peke yake. Ukweli huu tunaupata katika maandiko yafuatayo ya Qur'an tukufu na Biblia takatifu:
Biblia
"Yeye Mwenyezi Mungu hatuwezi kumwona; Yeye ni mkuu mwenye uweza". (Ayubu 37:23)
"Wewe ndiwe Mungu ufanyaye maajabu; Uliudhihirisha uweza wako kati ya mataifa". (Zaburi 77:14)
Qur'an
"Kinamtukuza Allah (Mwenyezi Mungu) kila kilichomo mbinguni na ardhini, na Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hikima. Ufalme wa mbingu na ardhi ni Wake, Anahuisha na Kufisha. Na Yeye ni mwenye uweza juu ya kila kitu". (Qur. 57:1-2)
"Na mali aliyoleta Allah (Mwenyezi Mungu) kwa Mtume wake kutoka kwao hamkuyaendeshea mbio farasi wala ngamia (hamkuyataabikia), lakini Allah (Mwenyezi Mungu) huwapa mamlaka Mitume yake juu ya wowote awatakao (kama alivyokupeni hivi); na Allah (Mwenyezi Mungu) ni mwenye uweza juu ya kila kitu". (Qur. 59:6).
Kulingana na shuhuda hizo, tunaona hapa kuwa Qur'an na Biblia vinafundisha kwamba sifa ya uweza ni ya Mwenyezi Mungu mmoja aliyejifunua kwa Manabii wake mbalimbali lakini kwa majina tofauti. Kwa shuhuda hizo, ni wazi kuwa sifa hii pia inadhihirisha kuwa Allah na Yehova ni Mungu yule yule mmoja aliyejifunua kwa Manabii wake mbalimbali kwa majina tofauti.
Kutokufanana na yeyote wala na chochote
Kwa kuzingatia udhaifu mkubwa uliopo kwa viumbe vyake kwa kila hali, sifa kuu ya tano inayomdhihirisha Mungu wa kweli, ni kutokufanana na kiumbe wake yeyote wala chochote. Kwa mantiki hiyo basi, sifa hii pia ni kigezo kingine muhimu kinachoweza kuwa hoja ya msingi ya kutofautisha Allah na Yehova. Hata hivyo, tusomapo maandiko ya Qur'an tukufu na Biblia takatifu tunaona ni Mwenyezi Mungu mmoja ndiye anayedai kuwa na sifa hiyo, kama aya za Qur'an tukufu na Biblia takatifu zinavyoeleza wazi hapa chini:
Biblia:
"BWANA akamwambia Musa, Ondoka asubuhi na mapema, ukasimame mbele ya Farao, umwambie, BWANA, Mungu wa Waebrania, asema, Wape watu wangu ruhusa waende ili wanitumikie. Kwani wakati huu nitaleta mapigo yangu yote juu ya moyo wako, na juu ya watumishi wako, na juu ya watu wako; ili upate kujua ya kuwa hapana mmoja mfano wa mimi ulimwenguni mwote". (Kutoka 9:13-14)
"Hapana aliyefanana na Mungu, Ee Yeshuruni, ajaye amepanda juu ya mbingu ili akusaidie". (Kumbukumbu la Torati 33:26).
"Mungu si mtu; aseme uongo; wala si mwanadamu, ajute". (Hesabu 23:19)
"Mtanifanisha na nani, na kunisawazisha naye, na kunilinganisha naye, ili tuwe sawa sawa?" (Isaya 46:5)
Qur'an
"Sema: Yeye Allah ni Mwenyezi Mungu mmoja (tu). Allah (tu) ndiye anayestahiki kukusudiwa (na viumbe vyake vyote kwa kumuabudu na kumuomba na kumtegemea). Hakuzaa wala hakuzaliwa. Wala hana anayefanana naye hata mmoja". (Qur. 112:1-4)
"(Yeye Allah ndiye) Muumba wa mbingu na ardhi. Amekuumbieni wake (zenu) katika jinsi yenu; na wanyama nao (akawaumbia) wake (zao katika jinsi moja na wao); anakuzidisheni kwa namna hii (ya kuchanganyika dume na jike). Hakuna chochote mfano wake; naye ni mwenye kusikia, mwenye kuona". (Qur. 42:11)
Kulingana na shuhuda hizo juu, tunaona hapa Biblia na Qur'an tukufu vyote vinamkariri Mwenyezi Mungu yule yule mmoja akibainisha wazi kuwa hafanani na yeyote wala na chochote katika viumbe wake wote ulimwenguni. Kwa shuhuda hizo basi, ni wazi kuwa sifa hii nayo, pia inadhihirisha kuwa Allah na Yehova ni Mungu yule yule mmoja mwenye sifa zote kamilifu, Muumba wa kila kitu.
Kutokuonekana
Kwa kuzingatia kuwa hana mfano wa kiumbe wake yoyote wala chochote,sifa kuu ya sita inayomdhihirisha Mungu wa kweli ni kutokuonekana na viumbe vyake hasa kwa vile binafsi yake (Mungu) hana umbo la kuonekana kutokana na Yeye kuepukana mbali na sifa dhaifu ya kuumbwa au kuzaliwa. Kwa mantiki hiyo, sifa hii pia ni kigezo kingine muhimu kinachoweza kuwa hoja ya msingi ya kutofautisha Allah na Yehova iwapo tu itabainika kuwa mmoja wao hana sifa hiyo. Hata hivyo, tusomapo maandiko ya Qur'an tukufu na Biblia takatifu tunaona pia kuwa ni Mwenyezi Mungu yule yule mmoja ndiye mwenye sifa hiyo. Ukweli huu unathibitishwa na maandiko ya Qur'an tukufu na Biblia takatifu yafuatayo:
Biblia:
"Yeye Mwenyezi hatuwezi kumwona; Yeye ni mkuu mwenye uweza; tena mwenye hukumu, na mwingi wa haki, hataonea". (Ayubu 37:23)
"BWANA akamwambia Musa, Nitafanya na neno hili ulilolinena, kwa maana umepata neema mbele zangu, nami nakujua jina lako. Akasema, Nakusihi unionyeshe utukufu wako. Akasema, Nitapitisha wema wangu wote mbele yako, nami nitalitangaza jina la BWANA mbele yako; nami nitamfadhili yeye nitakayemfadhili, nitamrehemu yeye nitakayemrehemu. Kisha akasema, Huwezi kuniona uso wangu, maana mwanadamu hataniona akaishi". (Kutoka 33:17-20)
"Na sasa, Ee Israeli... BWANA akasema nanyi kutoka kati ya moto; mkasikia sauti ya maneno, lakini hamkuona umbo lolote, sauti tu". (Kumbukumbu la Torati 4:12)
"Jihadharini nafsi zenu basi; maana hamkuona umbo la namna yoyote siku ile BWANA aliyosema nanyi kutoka kati ya moto; msije mkajiharibu nafsi zenu, mkajifanyia sanamu ya kuchonga, mfano wa sura yoyote, mfano wa mwanamume au mwanamke". (Kumbukumbu la Torati 4:15-16)
Qur'an:
"Huyo ndiye Allah (Mwenyezi Mungu), Mola wenu Hakuna anayeabudiwa kwa haki ila yeye, Mwumba wa kila kitu. Kwa hivyo, mwabuduni yeye (tu). Naye ni mlinzi wa kila kitu. Macho hayamfikii (kumwona), bali yeye anayafikia macho (kuyaona na kuwaona hao wenye macho). Naye ni mwenye kujua yaliyofichikana na yaliyo dhahiri". (Qur. 6:102-103)
Kulingana na shuhuda hizo, tunaona hapa kuwa Qur'an tukufu na Biblia takatifu vyote vinatufundisha pamoja kuwa sifa hiyo ya kutokuonekana na yoyote wala na chochote ni ya Mwenyezi Mungu yule yule mmoja hasa kwa vile yeye hana umbo la kuweza kuonekana. Aidha sababu nyingine ya kutokuonekana kwake kama maandiko yanavyoonyesha, inatokana na uwezo dhaifu wa mwanadamu wa kuweza kuhimili katika kumwona Mwenyezi Mungu mtukufu. Kwa shuhuda hizo, ni wazi kuwa sifa hii pia inadhihirisha kuwa Allah na Yehova ni Mungu yule yule mmoja asiyefanana na yeyote wala na chochote, Muumba wa kila kinachoonekana na kisichoonekana.
Upweke (hana mshirika)
Kwa kuzingatia Yeye ndiye aliyekuwepo kabla ya yeyote na kabla ya chochote na yeye ndiye mwanzilishi (Muumbaji) na mwendeshaji wa kila kitu na kwa kuzingatia pia udhaifu mkubwa uliopo kwa viumbe vyake katika kila hali, hapana shaka yoyote sifa kuu nyingine ya Mungu wa kweli ni upweke (yaani kutokuwa na mshirika katika Uungu wake). Kwa mantiki hiyo, sifa hii pia ni kigezo kingine muhimu kinachoweza kuwa hoja ya msingi ya kutofautisha Allah na Yehova iwapo tu itabainika kuwa mmoja wao hana sifa hiyo. Hata hivyo, tusomapo maandiko ya Qur'an tukufu na Biblia takatifu tunaona mwenye sifa hiyo ni Mwenyezi Mungu yule yule mmoja aliyejifunua au kujitambulisha kwa Manabii wake mbalimbali kwa majina tofauti. Ukweli huu tunaupata katika maandiko yafuatayo ya Qur'an tukufu na Biblia takatifu:
Biblia:
"BWANA, Mfalme wa Israeli, Mkombozi wako, BWANA wa Majeshi, asema hivi; Mimi ni wa kwanza, na mimi ni wa mwisho; zaidi yangu mimi hapana Mungu. Naye ni nani kama mimi atakayeita, na kuyahuburi haya, na kunitengenezea, tangu nilipowaweka watu wa kale? na mambo yanayokuja, na yatakayotokea, wayatangaze. Msiogope wala msifanye hofu, Je! Sikukuhubiri haya zamani na kuyaonyesha? Na ninyi ni mashahidi wangu. Je yuko Mungu zaidi yangu mimi? Hakika hapana Mwamba; mimi sijui mwingine". (Isaya 44:6-8)
"Hubirini, toeni habari, naam, na wafanye mashauri pamoja, na nani aliyeonyesha haya tangu zamani za kale? Ni nani aliyehubiri hapo zamani? Si mimi, BWANA? Wala hapana Mungu zaidi ya mimi; Mungu mwenye haki, mwokozi, hapana mwingine zaidi ya mimi". (Isaya 45:21)
"Ninyi ni mashahidi wangu, asema BWANA, na mtumishi niliyemchagua, mpate kujua, na kuniamini na kufahamu ya kuwa mimi ndiye; kabla yangu hakuumbwa Mungu awaye yote,wala baada yangu mimi hatakuwapo mwingine". (Isaya 43:10)
"Na uzima wa milele ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma". (Yohana 17:3)
Qur'an:
"Sema: Hakika sala zangu, na ibada zangu (zote nyingine) na uzima wangu, na kufa kwangu (zote) ni kwa Allah (Mwenyezi Mungu). Muumba wa walimwengu wote. (Likinisibu jambo limenisibu kwa kutaka Mwenyezi Mungu si kwa kutaka viumbe vyake. Na yote ninayoyafanya nayafanya kwa ajili yake".
"Hana mshirika wake. Na haya ndiyo niliyoamrishwa, na mimi ni wa kwanza wa waliojisalimisha (kwa Mwenyezi Mungu)". (Qur. 6:162-163)
"Allah (Mwenyezi Mungu) hakujipatishia mtoto wala hakuwa pamoja naye Mungu (mwingine). Ingekuwa hivyo basi kila Mungu angaliwachukua aliowaumba; na baadhi yao wangaliwashinda wengine (kwani lazima wangepigana kwani fahali wawili hawakai zizi moja). Allah (Mwenyezi Mungu) ameepukana na sifa wanazomsifu (nazo, zisizokuwa ndizo). Mjuzi wa siri na dhahiri na Ametukuka na hao wanaomshirikisha naye". (Qur. 23:91-92)
"Sema: Yeye Allah (Mwenyezi Mungu) ni mmoja tu". (Qur. 112:1)
Kulingana na shuhuda hizo juu, ni wazi kuwa Qur'an tukufu na Biblia takatifu vyote kwa pamoja vinamkariri Mwenyezi Mungu yule yule mmoja akijinadi kuwa yeye ni mmoja wa pekee, asiyekuwa na mshirika yoyote katika Uungu wake tangu milele na hata milele. Kwa shuhuda hizo, ni wazi kuwa sifa hii pia inadhihirisha kuwa Allah na Yehova ni Mungu yule yule mmoja aliyejifunua au kujitambulisha kwa Manabii wake mbalimbali kwa majina tofauti.
Itaendelea toleo lijalo
|
|