Wahimizwa kuienzi kalenda ya Kiislamu
 

Na Abeid Poyo
 

WAISLAMU kote duniani wametakiwa kujivunia na kuitangaza kwa hali zote kalenda yao ya Kiislamu.

Hayo yalisemwa hivi karibuni na Khatib wa Msikiti wa Qadiriya Ustadh Mohamed Komo alipokuwa akizungumza na Waislamu katika hafla ya maulid ya kuukaribisha mwaka mpya wa Kiislamu (1420 AH) ndani ya Msikiti Qadiriya wilayani Temeke.

Katika mazungumzo yake hayo, Ustadh Komo alieleza jinsi umma wa Waislamu hivi leo ulivyopuuza kalenda ya Kiislamu na kuiona kama kitu kilichopitwa na wakati.

"Kila mwezi katika kalenda ya Kiislamu una sababu zake za kimajira na kiibada, mfano mwezi wa Ramadhani na Dhulhijja ambapo mnapatikana ibada za Saumu ya Hijja", alisema alipokuwa akisisitiza juu ya mfumo mzuri wa kalenda ya Kiislamu.

Aliongeza kuwa haiyumkini kwa Waislamu kushindwa kuitangaza kalenda yao, wakati vitu vingi visivyo kuwa na maana kwa mwanadamu vimekuwa vikitangazwa.

Kalenda ya Kiislamu inaanzia pale Mtume Muhammad (s.a.w.) na masahaba zake walipohama kutoka Makka kwenda Madina.


Sheikh Jongo asema Uwawaru ni haramu
  Na Muhibu Saidi, Rufiji

"ALIYEINGIA UWAWARU na anayefikiria kufanya hivyo atoke mara moja kwani hiyo ni haramu".

Hayo yametamkwa na Imamu wa Msikiti wa Manyema Sheikh Hamid Jongo wakati akihutubia hadhara ya Waislamu wa wilaya ya Rufiji Jumamosi iliyopita.

Aidha, Waislamu wote wenyeji wa Rufiji wamelaani mbinu na hila zinazotumiwa na maadui wa Uislamu kuwahadaa ili kutaka kufufua umoja huo.

Waislamu hao wameazimia kwa pamoja kumshitaki yeyote atakayejaribu kutaka kufufua umoja huo kwa hila yoyote baada ya kuwa umekwishazikwa.

Wametoa kauli hiyo Jumamosi ya Aprili 17, mwaka huu katika kilele cha muhadhara mkubwa na wa aina yake uliofanyika eneo la Msikiti Mkubwa wa Ikwiriri (Masjid Jumuiyat) uliopo tarafa ya Ikwiriri, wilaya ya Rufiji mkoa wa Pwani.

Muhadhara huo uliojumuisha Masheikh maarufu na kufanyika kwa muda wa siku mbili mfululizo eneo hilo, uliandaliwa na Umoja wa Vijana wa Kiislamu nchini (TAYMA) na kuhudhuriwa pia na Sheikh wa Bakwata wa Wilaya ya Rufiji.

Akihutubia maelfu ya waumini wenyeji wa wilaya hiyo waliofurika katika muhadhara huo, Sheikh Hamid Jongo aliwataka wale wote waliokwishajiunga na umoja huo na wanaofikiria kufanya hivyo kwa vishawishi vya Sheikh huyo wa Bakwata watoke mara moja na washuhudie upya kwani uamuzi wao huo alisema tayari ulikuwa umekwishawatoa katika Uislamu na kuwaingiza katika ukafiri.

Alisema, Uislamu umewaruhusu Waislamu kuishi kwa wema na ihsani na wasiokuwa Waislamu iwapo tu hawaupigi vita Uislamu, lakini alisema wamekatazwa kushirikiana nao katika jambo lolote linalohusu imani ya dini maadamu watakuwa nje ya Uislamu.

"Tunasema Wakristo wakitukorofisha hatutokubali wala kuvumilia... maadui wanapotaka ugomvi lazima kwanza wauchezee Uislamu. Tunasema hivyo na hatujali hata kama tutaondoka na kuitwa siasa kali. Tuiteni jina lolote, lakini hatuwezi kuacha kuutetea Uislamu", alisema kwa hasira Sheikh Jongo huku akiungwa mkono kwa Takbira.

Sheikh Jongo alitoa fat'wa hiyo kufuatia uvumi ulioenea wilayani hapa kwamba Sheikh wa Bakwata wa Wilaya hiyo, Sheikh Kassim Saidi Lwambo kwa kushirikiana na viongozi wa Kanisa na baadhi ya watu ameamua kuufufua umoja huo.

Katika kuhalalisha umoja huo, Sheikh huyo anadaiwa kujaribu kuwahadaa waumini kwa kutumia hila mbalimbali akidai kwamba umoja huo hauingilii imani ya dini yoyote bali unalenga tu kuondoa tofauti zilizopo baina ya Waislamu na Wakristo na kwamba lengo lake kuu ni kuwaletea maendeleo wenyeji wa wilaya hiyo.

Aidha, ilidaiwa kuwa Sheikh huyo wa Bakwata pia amekuwa akiwaeleza waumini kuwa kujiunga na umoja huo ni katika mbinu za kutekeleza amri ya kuwalingania wasiokuwa Waislamu kwa hikma waingie katika Uislamu.

Umoja huo uliundwa na viongozi wa Kanisa moja nchini wakishirikiana na baadhi ya viongozi wa serikali wa wilaya hiyo.

Katika hotuba yake hiyo iliyokuwa ya kusisimua, Sheikh Jongo aliyapuuza madai yote ya kutaka kuwahadaa Waislamu ili wapate kuua Uislamu Rufiji kirahisi kupitia UWAWARU.

Alisema kila mwenye akili timamu anafahamu wazi kuwa vita dhidi ya Uislamu sasa ni vya wazi na kwamba siyo vya Rufiji wala vya kitaifa peke yake bali ni vya kimataifa.

"Hapa ninao ushahidi kwamba mbinu hizo zinasimamiwa na shirika moja la misaada la Kimarekani ili kuhakikisha wanautokomeza Uislamu duniani. Kama mlikuwa hamjui kuwa Uislamu una adui basi hivi sasa hilo mlijue, kwamba adui yetu yupo", alisema Sheikh Jongo huku akiuonyesha umati wa waumini nakala ya waraka wa shirika hilo.

Aliongeza kuwa maadui wameamua kuwaundia Warufiji umoja huo kama chambo baada ya kushindwa kuwapata kirahisi.

"Wameona Warufiji ni wagumu kuingia katika ukafiri kama Wakosovo ndio sasa wameamua kuwahadaa kwa hila", alisema.

Alisema Waislamu daima hawana ugomvi wowote na wazalendo wenzao Wakristo kwa kufuata kwao Ukristo. Na katika kudhihirisha hilo alisema Warufiji wamediriki kuwapatia ardhi Wakristo katika mashamba yao bila kujali utofauti wa kiitikadi.


Chuo Kikuu washuhudia mauaji ya Mwembechai
 

Na Mwandishi Wetu

MAMIA ya wanafunzi na baadhi ya Wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwanzoni mwa wiki hii walipata fursa ya kushuhudia unyama uliofanywa na polisi katika maeneo ya Mwembechai Februari mwaka jana.

Kupitia onesho la mkanda wa video ulionasa matukio ya kinyama, wanafunzi hao waliona jinsi raia wasio na hatia wakidunguliwa risasi huku maiti zao kukejeliwa na polisi waliokuwa katika operesheni hiyo.

Baadhi ya waliohudhuria onesho hilo lililofanyika mbele ya Msikiti wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam walionekana wakitiririkwa kwa machozi baada ya kushindwa kuvumilia vitendo hivyo vya kinyama vya jeshi la polisi la Tanzania huru.

"Siamini macho yangu, Tanzania imekuwa kama Soweto, watu wanalengwa risasi kama swala bila huruma", alisikika akisema kwa uchungu mwanafunzi mmoja wa mwaka wa pili.

Aidha, wasomi hao wamehoji nini kilichowasukuma polisi mpaka kufikia kuua raia waliokuwa na mawe.

Wamewashutumu viongozi wa serikali kwa jinsi walivyolichukulia suala hili kisiasa.

Wasomi hao wameonya kuwa Tanzania imefikia mahali pabaya ambapo hali ikiachwa iendelee hivi bila ya kuchukuliwa hatua zozote; nchi inaweza kufikia walipo Waserbia na Waalbania wa Kosovo hivi sasa.

Watu watachoka na wanaweza kufikia kujitoa muhanga ili waondokane na kunyanyaswa huko", alisema Bwana Alfonce Ndeki mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Kitivo cha Uandisi.

Wasomi hao wamependekeza kuwa mkanda huo wa mauaji ya Mwembechai upelekwe kila kona ya nchi na nje ya nchi ili ukweli juu ya tukio hilo ufahamike kutokana na vyombo vya habari kuupotosha kwa makusudi.


Waislamu Kigoma watakiwa kukamilisha ujenzi wa shule
 

Na Iddi Katimba, Kigoma

WAISLAMU mkoani Kigoma wametakiwa kukamilisha ujenzi wa shule ya sekondari ulioanza hivi karibuni mkoani humo.

Akielezea juu ya mradi huo, Sheikh wa Mkoa Tawfiq Ibrahim amesema shule hiyo ipo eneo la Mwanga na inatarajiwa kuandaa vijana wa Kiislamu kwa ajili ya maendeleo ya Waislamu wa mkoa huo na Tanzania kwa ujumla.

Alisema Waislamu hawana budi kuandaa wataalamu wao na kuwaandalia mazingira mazuri ya kujitegemea.

"Tusiwe watumishi wa wengine katika nchi yetu", alisema Sheikh Tawfiq.

Aidha, alitahadharisha kuwepo kwa maadui ambao alisema wameanza kupenyeza mikono yao ndani ya mradi huo wa shule ya sekondari.

Sheikh Tawfiq alitoa taarifa ya mradi huo wa shule mbele ya maelfu ya waumini wa dini ya Kiislamu katika maadhimisho ya mwaka mpya wa Kiislamu yaliyofanyika kitaifa mkoani humo Jumapili Aprili 18, mwaka huu.


Sheikh Bane awataka Waislamu watanabahi vita dhidi yao
 

Na Mwandishi Wetu, Rufiji

SHEIKH maarufu nchini, Sheikh Twaha Suleiman Bane amewatanabaisha wazazi na walezi wa Kiislamu kuchukua tahadhari juu ya mustakabali wa watoto wao dhidi ya vita vya kifikra vinavyoendeshwa hivi sasa kwa kasi ya kutisha na maadui wa Uislamu duniani.

Sheikh Bane alitoa tanbihi hiyo Ijumaa ya Aprili 16, mwaka huu wakati akihutubia maelfu ya waumini waliohudhuria katika muhadhara uliofanyika katika Msikiti mkubwa wa Ikwiriri (Masjid Jumuiyat) uliopo tarafa ya Ikwiriri, wilaya ya Rufiji mkoa wa Pwani.

Shekh Bane aliwakumbusha wazazi na walezi hao wajibu wao wa kuzipa familia zao malezi bora ya Kiislamu ili kupambana na maadili mabaya yanayopandikizwa kwa kasi na maadui wa Uislamu.

Alisema maadui wa Uislamu wameamua kubuni vita hivi kwa lengo la kuuenzi msalaba, alisema maadui hao hutumia mbinu mbalimbali kuhakikisha wanawatenga mbali Waislamu na dini yao (Uislamu) na kuwafanya kuwa wafuasi wa mila na tamaduni zao.

Alisema mbinu wanazotumia kuvutia katika mila zao wamezitaja katika sekta mbalimbali, ikiwemo elimu, vyombo vya habari, utamaduni na hata kwenye mabango mbalimbali ya matangazo, lengo ni kuuendeleza na kuuenzi msalaba.

Sheikh Bane aliongeza kuwa mbinu nyingine zinazotumiwa na maadui kufikia lengo lao ni pamoja na kukichafua kila kinachoheshimiwa na kuenziwa na Uislamu kama vile kuwaita "siasa kali" wale wote wanaopigania Uislamu na wanawake wa Kiislamu wanaojisitiri kwa vazi la hijabu kuwaita "maninja".

"Fujo zote kama zile za kuhamasisha kugawa na uvaaji wa kondomu, migogoro ya mirathi na mingineyo ni katika mbinu hizo hizo za maadui wa Uislamu dhidi ya Uislamu", alisema.

"Uadui dhidi ya Uislamu upo. Mbinu, hila, ujanja vinatumiwa ili kufikia lengo hilo. Vita hivi ndugu zangu si vidogo. Almuhimu tujitahidi kuwadhibiti wenetu kwa kuwalea vizuri malezi ya Kiislamu kwani hao ndio walengwa wanaokusudiwa. Tuboreshe madrasa zetu na tujitahidi kila kwenye Msikiti kuwepo na Madrasa", alimalizia Sheikh Bane.
 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook