Harakati za kudai haki za Waislamu nchini:

Maandamano makubwa yafanyika Kigoma

Na Mwandishi Wetu, Kigoma

MAELFU ya waumini mkoani Kigoma Jumapili iliyopita waliandamana kuzunguka maeneo mbalimbali ya mji huo kumuunga mkono Katibu wa Kamati ya Kutetea Haki za Waislamu Bwana Ponda Issa Ponda kwa kuitaka serikali iwachukulie hatua waliohusika na mauaji ya Mwembechai.

Aidha, wananchi hao wamelishutumu jeshi la polisi kwa madai yake ya kumsaka Sheikh Ponda huku likiwafumbia macho wauaji.Maandamano hayo ambayo yalianza saa 12 asubuhi yalifanyika sambamba na maadhimisho ya Mwaka Mpya wa Kiislamu (1420 H) yalitokea vitongoji tofauti vya mji huo na kukusanyika katika shule ya msingi ya Wazaire ambapo kufikia saa 3:00 asubuhi umati ambao haujapata kuonekana katika historia ya mji huu  uliandamana kwa pamoja hadi viwanja vya Mwanga Centre.

Mwandishi wa habari hizi alishuhudia makundi ya wananchi walioshiriki maandamano hayo yakiwasili shule ya Wazaire kutoka kona tofauti ambapo wale wa Gungu na Mwandinga walitokea eneo la Sabasaba, wakati wale wa Mwanga walianzia Msikiti wa Legeza Mwendo, huku wa Kibirizi, Bungwe na Kigoma wakitokea Stesheni ya gari Moshi na kwa Ujiji, Mwanga, Majengo na Katibuka walianzia Ujiji kufika mahali hapo.

Tukio jingine lililosisimua wengi ni lile la kujumuika katika hafla hiyo wakazi wa Mwamgongo ambao waliwasili kwa njia ya boti siku tatu kabla.

Mwamgongo ni mwendo wa masaa yasiyopungua matatu kukatiza ziwa Tanganyika kwa usafiri wa boti.

Masheikh maarufu waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na Sheikh wa Mkoa Sheikh Tawfiq Ibrahim Malilo, Sheikh wa wilaya Sheikh Abubakar Idrisa Abdul Muhsin wa Ujiji, Sheikh Abdulwahid na Sheikh Hilali Mahuba.

Wengine ni Sheikh Hassan Iddi Kiburwa, Shekh Hassani Iddi, Sheikh Omari Buru, Sheikh Ibrahim Kabege, Sheikh Jafari Kasisiko, Alhaj Sheikh Shaaban Guoguo na Ustadh Tabrani.

Masheikh na waumini hao waliazimia mambo kadhaa katika maadhimisho hayo ikiwe ni pamoja na kuwataka wasomi wa Kiislamu wakutane na kuunda chama cha siasa kitakacholeta usawa na maendeleo kwa raia wote.

Wakati huo huo, Masheikh na waumini wa dini ya Kiislamu mkoa wa Kigoma wameitaka serikali iache mara moja kumuandama na kumsaka Ponda Issa Ponda na wameahidi kufanya maandamano hadi kwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma ili wampe ujumbe awafikishie kwa Rais.

Aidha, waumini hao wamesema wapo pamoja na Ponda kwa hali na mali na wamesisitiza serikali iache hadaa iwafikishe wauaji mahakamani na impeleke mtoto Chuki akatibiwe nje ya nchi.

Wamesema Ponda ni mtoto wao, ndugu yao, rafiki yao, Muislamu mwenzao na mzaliwa mwenzao wa mkoa huo hivyo polisi Jijini Dar es Salaam kutangaza kumsaka bila ya yeye kuwa na kosa lolote ni kuwachokoza wenyeji wa mkoa huo na Waislamu kwa ujumla.

Polisi jijini Dar es Salaam mwanzoni mwa mwaka jana ilitangaza kumsaka Sheikh Ponda kufuatia hatua ya kamati yake kuandika waraka ulioelezea dhulma wanazofanyiwa Waislamu hapa nchini na kuusambaza kwa Wabunge, vyama vya siasa, wanataaluma wa Chuo Kikuu, Idara ya Usalama na wanasheria.

Aidha, katika hatua nyingine iliyoonekana kuwakera baadhi ya viongozi, kamati ya Sheikh Ponda iliitisha mkutano wa waandishi wa habari na kueleza ukweli juu ya huzuni ya Mwembechai kinyume na propaganda zilizokuwa zikienezwa na viongozi hao.

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook