HUKU serikali ikiendelea kupiga kimya pamoja na kukiri kupokea malalamiko ya Waislamu, Sheikh wa Bakwata Mkoa wa Kigoma Sheikh Tawfiq Ibrahim Malilo amesisitiza madai kuwa waliohusika kuua wananchi wasio na hatia Mwembechai wachukuliwe hatua.
Akihutubia umati mkubwa wa Waislamu waliokusanyika katika viwanja vya Mwanga baada ya kuandamana maeneo mbalimbali ya mji huo Jumapili iliyopita, kiongozi huyo Mkuu wa Bakwata mkoa wa Kigoma alisema suala la Mwembechai haliwezi kwisha kwa hadaa za serikali.
Alisema ili kumaliza mgogoro huu serikali inapaswa kuchukua hatua za kiadilifu kwa kuruhusu sheria ichukue mkondo wake badala ya kuendesha propaganda na uonevu dhidi ya kundi kubwa la wananchi wake.
"Kumuua Muislamu mmoja ni sawa na kuwauwa Waislamu wote, kwani Waislamu ni sawa na mwili mmoja", alisema Sheikh Tawfiq akimaanisha kuwa suala la Mwembechai ni la Waislamu wote nchini.
Sheikh huyo maarufu nchini alionyesha kusikitishwa na hatua ya serikali ya Rais Benjamin Mkapa kuendelea kukalia kimya suala hilo na kuviacha vyombo vya dola vikiendelea kuwanyanyasa Waislamu kutokana na chuki za kidini za baadhi ya watendaji wake.
"Haiwezekani watu wakauawa kwa kulengwa kama wanyama porini na halafu kulizungumzia liwe suala nyeti", alisema kwa masikitiko Sheikh Tawfiq.
Aidha, alisema kuwa kuwashambulia Waislamu ndani ya Msikiti ni kosa kubwa lenye kustahiki kuchukuliwa hatua za haraka na serikali yenye kuheshimu haki za binadamu.
Akigusia kudhalilishwa kwa wanawake wa Kiislamu katika kadhia hiyo, alisema ni fedheha kubwa kuwavua nguo na kuwasachi akinamama sehemu za siri.
Alishangazwa na vyombo vinavyodai kupigania haki za wanawake kwa kuikalia kimya fedheha hiyo kwa kinamama.
Awali Sheikh Tawfiq alihimiza mshikamano miongoni mwa Waislamu na kusifu jitihada iliyofanywa mkoani humo kuondoa tofauti miongoni mwa Waislamu na kuwezesha kuwepo sala ya Ijumaa ya mshikamano wa Misikiti yote.
Sheikh Tawfiq alisema umoja kama huo ndiyo uliowawezesha wananchi wa Tanganyika kumng'oa mkoloni hivyo aliwataka Waislamu Kigoma na sehemu nyingine watumie umoja wa aina hiyo kukabili magumu yanayowafika.
Maandamano ya Jumapili Aprili 18, mwaka huu mkoani Kigoma yalienda sambamba na sherehe za Kitaifa za Mwaka Mpya wa Kiislamu 1420 Hijria.
Wageni kutoka mikoa mbalimbali
ikiwa ni pamoja na Jiji la Dar es Salaam walihudhuria hafla hiyo ya kihistoria
mkoani humo.
|
|