MCHUMI mahiri na Mshauri Mkuu wa Chama cha CUF, Prof. Ibrahim Lipumba amewaeleza wananchi wa mkoa wa Tanga masikitiko aliyonayo juu ya hatua ya wenyeji wengi wa mkoa huo kuipigia kura CCM katika uchaguzi uliopita hali iliyochangia kukirejesha chama hicho madarakani ambapo hivi sasa Watanzania wanaishi maisha ya dhiki kutokana na 'sera' zake.
Prof. Lipumba aliyasema hayo mwanzoni mwa ziara yake mjini Tanga katika mkutano ulioandaliwa na chama hicho uliofanyika kwenye viwanja vya Tangamano siku ya Jumamosi Aprili 17, mwaka huu.
Prof. Lipumba aliuambia umati mkubwa uliofurika katika mkutano huo kuwa uchumi wa nchi umekuwa ukishuka kila mwaka kinyume na ahadi zilizotolewa na Rais Benjamin William Mkapa wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka 1995.
Alisema pamoja na kwamba kura za wananchi wa Tanga zilichangia kwa kiasi kikubwa kuiweka CCM madarakani lakini mkoa huo umewekwa chini kiuchumi.
Alitoa mfano wa kuuliwa kwa viwanda na kuwakosesha ajira hali iliyopelekea waendelee kuishi maisha ya dhiki jambo ambalo alisema kila mwananchi wa mkoa huo analishuhudia kwa macho yake.
Alipoulizwa na wananchi hao ni jinsi gani angeweza kuwasaidia hasa katika uvuvi, Prof. Lipumba alisema ambacho angeweza kama mtaalamu ni kuishauri serikali, lakini kiutendaji ni suala gumu kwake kwani inayofanya hivyo ni serikali waliyoiweka na yeye hayumo, hata hivyo aliahidi kulifikisha suala hilo katika kamati ya haki za binadamu.
Mwandishi wa habari hizi alipowahoji baadhi ya wananchi juu ya yale yaliyozungumzwa na Prof. Lipumba walikiri kuwa mkoa huo umeathirika sana kiuchumi hivi sasa kulinganisha na miaka ya nyuma.
Bwana Abdallah Saidi wa barabara ya 15 alisema viwanda vimeuzwa bila ya kuwafaidisha chochote wananchi.
Prof. Lipumba alitembelea
pia Pangani, Muheza na kumalizia ziara yake Korogwe.
|
|