Hali ya Uislamu Seregete Moro mbaya
 

Na Rajab Rajab, Morogoro

HALI ya Uislamu katika vijiji vya Seregete 'A' na 'B' vilivyoko katika kata ya Kidugalo, tarafa ya Ngerengere mkoani hapa ni mbaya kufuatia eneo hilo kutokuwa na walimu wa dini licha ya kuwepo Waislamu wengi.

Vijiji hivyo vilivyoko mwishoni mwa mkoa wa Morogoro na Pwani kupakana na kijiji cha Lukenge mkoa wa Pwani havina Msikiti wala madrasa ambapo Waislamu wanalazimika kufanyia ibada zao chini ya mwembe.

"Hapa ndipo tunaposwalia baadhi ya Waislamu wengi waliokuwepo hapa kijijini", alisema Bw. Abdallah Saidi Dakawa akionyesha kiwanja kilichofagiliwa chini ya mwembe huku kukiwa na mkeka mmoja pamoja na birika iliyoning'nizwa katika tawi la mti huo, mara baada ya kuulizwa na mwandishi wa habari hizi ni wapi sehemu wanapofanyia ibada zao.

Akielezea hali ya Uislamu kijiji hapo, Bw. Dakawa aliendelea kusema "hali ya Uislamu hapa Seregete'B' ni mbaya kama unavyoona mwenyewe na isitoshe watu huzikwa kimila kwa kuombewa dua moja tu inayosema Kikukomile Genda Genda Nacho kwa lugha ya Kikutu".

Alipoulizwa nini maana ya dua hiyo alisema kuwa kitu kinachokuua uende nacho hicho kisha watu humfukia maiti na kuanza kutawanyika na kuendelea na shughuli zao kama kawaida.

Mwandishi wa habari hizi alipotaka kujua inakuwaje kwa mazishi ya baadhi ya watu ambao wanajaribu kufuata Uislamu kijijini hapo, alisema kuwa inawalazimikia kufunga safari mpaka mkoa wa Pwani kijiji cha Lukenge umbali wa masaa saba na kumtafuta Sheikh wa kuwazikia.

"Wakati mwingine kama kafa Muislamu tunakwenda kumfuata Sheikh Mamula Mamula anayeishi kijiji cha Matuli mwendo wa saa sita kwenda na kurudi", alisema Bw. Abdallah Saidi Dakawa ambaye nyumba yake inapakana na mwembe ambao waumini wa Kiislamu husalia hapo.

Alipoulizwa ni nani anayeongoza ibada pale chini ya mwembe, Bw. Dakawa aliwaita watoto wawili wadogo ambao mmoja anaitwa Mohamed Abdallah (11) na wa pili alijitambulisha kuwa ni Shaabani Saidi (12) "hawa ndio vijana wanao tuswalisha hapa siku zote na ndio nguzo yetu", alisisitiza Bw. Dakawa.

Watoto hao walipoulizwa ni wapi wamepata elimu ya dini, wamesema "Sisi huwa tunasomea jijini Dar es Salaam kila mwaka wakati shule zinapofungwa na huko Dar es Salaam tunafundishwa na Ustadh Salum Saidi".

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi umebaini kuwa watoto hao mpaka hivi sasa wameweza kuhifadhi sura mbili tu za Qur'an Surat Fatiha na Ikhlas na sura nyinginezo wamedai wamezisahau.

Aidha, uchunguzi umeendelea kuonyesha kuwa Uislamu wa Seregete 'B' wakati wa swala ya Iddi hulazimika kuziacha nyumba zao na kwenda kulala mkoa wa Pwani ambapo kuna Misikiti pamoja na Masheikh na kwa upande wa Swala ya Ijumaa hawana habari nayo. Nao Waislamu wa Seregete 'A' ambao wapo karibu na kijiji cha Lukenge mkoa wa Pwani nao hawana Msikiti na swala zao wanaziendesha chini ya miti ya miembe.

Wakati huo huo, Waislamu wa Vijiji vya Seregete 'A' na 'B' wametoa masikitiko yao makubwa kwa viongozi wa Uislamu mkoa wa Morogoro vikiwemo vikundi vya dini kwa kuwatelekeza kama watoto wasio na mama wala baba tofauti na wenzao wa mkoa wa Pwani ambao Masheikh wao wanawatembelea na kuona hali ya Uislamu vijijini kwao ikiwa ni pamoja na kuhamasisha ujenzi wa Misikti na Madrasa.

Wakiongea na mwandishi wa habari hizi kijijini hapo hivi karibuni, Waislamu hao wamesema kuwa mara nyingi wametuma ujumbe kwa Masheikh mjini ili kwenda kuwanusuru Waislamu wa huko, lakini hakuna mtu yeyote aliyefika kutoka mjini Morogoro.

"Tumetuma ujumbe mara mbili waende kuwaona viongozi wa dini Morogoro mjini ikiwa ni pamoja na umoja wa vijana wa Kiislamu (JUSHUMUDI), lakini taarifa zetu zimekuwa zikipuuzwa na viongozi hao", alisema muumini mmoja wa kijiji hicho Bw. Saidi Juma.

Masikitiko mengine yametolewa na bibi kizee mmoja aliyejitambulisha anaitwa Bibi Kido ambaye amesema; "Masheikh wetu pamoja na Waislamu wa mkoani kwetu Morogoro nadhani wameshamaliza kazi ya kuueneza Uislamu ndio maana wametuachia vitoto hivi kuongoza dini huku vijijini na wao wakibaki mjini kugombania uongozi Misikitini".

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook