Na Kassim Billo, Tanga
BAADHI ya waumini wa Kiislamu wa Mkumbara wilayani Korogwe waliitwa kwenye kikao cha wazee wa mji wakishitakiwa kufanya kosa la kuvunja miko ya tambiko iliyokubaliwa na wanakijiji ya kutokwenda shambani kwa muda wa siku nne kama alivyoagiza mganga wa tambiko kuhusu wadugu wanaoharibu mimea waliozuka katika sehemu hiyo.
Kiongozi mmoja wa dini ambaye ni Imamu wa Msikiti sehemu za kijiji cha Mkumbara, wilayani Korogwe Maalim Mohammed Shekhe alieleza habari hizo kwa mwandishi wa habari hizi mjini Tanga hivi karibuni.
Mohammed Shekhe alieleza kwamba kutokana na kuzuka kwa wadudu wanaojulikana kwa jina la viwavi jeshi wanaoharibu mimea ya mahindi na mimea mingine, wazee wa mji wa Mkumbara wakishirikiana na viongozi wengine wa mji waliitisha kikao wakitaka kuitwe mganga wa kienyeji ili atengeneze madawa ya kienyeji ili wadudu hao wasiweko.
"Mganga aliitwa na akawabashiria watu wa mji wa Mkumbara kuwa wakitaka wadudu hao wasiwepo basi itawalazimu wasiende shambani kwa muda wa siku nne, na akasema atakayekwenda shambani kabla ya siku hizo kuisha basi atakuwa amevunja miko na wadudu hao watakuwepo na kuendelea kushambulia mimea", alieleza Imamu huyo.
Habari hizo zilipotangazwa mjini hapo baadhi ya Waislamu waliona jambo hilo ni moja ya shirki kubwa zinazomchukiza Mwenyezi Mungu na kwamba imani ya Kiislamu inakataza kukubali shirki kama hizo nao walizipuuza na hivyo kwenda mashambani kwao kulima na kupanda mimea yao.
Ilipojulikana kwa wazee wa mji waliitwa katika kikao cha wazee washitakiwe kuwa wamevunja amri za mganga na pia amri za kamati ya wazee wa kienyeji. Pamoja nao walikuwepo pia Walokole (Wakristo) ambao nao walikaidi amri ya mganga.
Kwa pamoja waliwaeleza wazee hao kwamba huo ulikuwa ni ushirikina na hivyo hawakuwa tayari kuufuata.
|
|