Na Mwandishi Wetu, Mwanza
WAISLAMU Mkoani Mwanza wameelezwa kwamba umwagaji damu uliofanywa na Polisi Mwembechai hautasahaulika kama ambavyo yale ya Hitler na wauaji wengine yasivyosahaulika.
Aidha wameelezwa kwamba lililomuhimu kwao ni kuwatambua wabaya wao ili wasihadaiwe na propaganda za kisiasa wakamfanya adui rafiki.
Hayo yameelezwa na wahadhiri mbalimbali katika sherehe za Mwaka Mpya wa Kiislamu 1420H zilizofanyika Masjid Arafa Mabatini na akina mama wa Madrasat Arafa na kuhudhuriwa na mamia ya Waislamu.
Akizungumza katika hafla hiyo Sheikh Ally Kulindwa alisema kwamba kamwe Waislamu hawatakuwa radhi na serikali bila ya wauaji hao kuchukuliwa hatua za kisheria.
Naye mgeni rasmi Sheikh Athumani Kaporo katika hotuba yake aliwataka Waislamu kuwachunguza maadui ili kupata kuwaelewa vilivyo, hivyo itasaidia kupambana nao kwa hakika.
Alisema tatizo lililopo Waislamu wamejisahau kuwa wana maadui, kwa hali hiyo adui anafanya atakavyo.
"Ukishamjua adui ni nusu ya ushindi, adui huanza kupoteza historia ya kitu na historia ikishapotea basi maana halisi ya kitu hupotea", alisema.
Aliwataka Maimamu kulifundisha somo hili la kalenda ya Kiislamu Misitikini na alisisitiza kuhusu maadui.
"Ukishayajua mabaya yao, tayari itakuwa rahisi kujua uzuri wa Uislamu wako, na utapigana nao na kupigania Uislamu ipasavyo", alisema Sheikh Athumani Kaporo.
Amezitaka taasisi zote za
Kiislamu hapa nchini kukaa pamoja na kupanga mikakati ya kuutetea Uislamu
bila kujali itikadi zao na bila kufanya hivyo makafiri wataendelea kuwachezea
Waislamu.
|
|