Kuweni macho na maadui - Mwinyi
 

Na Idd Katimba, Tabora

RAIS mstaafu Mh. Ali Hassan Mwinyi amewatahadharisha Waislamu wawe macho na wang'amue hatari iliyo mbele yao ambapo uadui na nguvu zote zilizo kuwa dhidi ya Ukomunisti zimeelekezwa katika Uislamu.

Amewaambia Waislamu kuwa kama ambavyo Ukomunisti umekufa; ni tamaa ya wapinzani wa Uislamu kuona nao unakufa au kusambaratika.

Alhaj Mwinyi aliyasema hayo akiwahutubia maelfu ya Waislamu waliohudhuria kuweka jiwe la msingi la Madrasa na Msikiti wa Mtendeni (TANESCO) eneo la Kiloleni.

Akiongea katika hafla mbalimbali za uzinduzi na uwekaji wa mawe ya msingi ya vituo vya elimu mjini Tabora, Alhaj Ali Hassan Mwinyi ametahadharisha juu ya ujinga uliowakuta watu ambapo watu wamekataa watoto kwa hofu ya njaa na umasikini.

Alisema ujahili huo ulikuwepo hata wakati wa Mtume (s.a.w.), lakini elimu ya Kiislamu ikauondoa. Aliwapongeza wakazi wa Tabora kwa kuamua kuufuta ujinga kwa kueneza vituo vya elimu.

Rais Mstaafu alikuwepo mkoani Tabora toka Aprili 18, kwa mwaliko wa Taasisi ya Nujumi ambapo pamoja na mambo mengine aliweka jiwe la msingi la shule ya sekondari ya Taasisi hiyo.

Baada ya shughuli hiyo Rais Mstaafu alikwenda kuuzindua upya Msikiti wa Ijumaa wa Isevya na Ipuli ambao ulijengwa kwa mara ya kwanza mwaka 1928, kwa hivi sasa umekarabatiwa upya na ndio unaosaliwa na wakazi wa Ipuli na Isevya kama Msikiti wa Ijumaa.

Wakazi hao walimuomba Rais Mstaafu kuwashawishi viongozi mbalimbali wa Kiislamu kuwatembelea, si kutembelewa wao tu bali watembelee nchi nzima ili kuhimizana na kushauriana ili kuleta maendeleo.

Siku ya Jumatatu alitarajiwa kwenda Lalangulu, Tumbi na baadaye kuweka jiwe la msingi la Msikiti wa Sheikh Kurwa Shauri mjini Tabora, baadaye kuondoka kuelekea Nzega hadi Shinyanga ambako angelala kusubiri ndege ya kumrudisha Dar es Salaam.

Kutokana na kuchelewa kuanza ziara hiyo kwa siku mbili, Alhaj Mwinyi hakuwahi kutembelea Sikonge, Nzega na Igunga.

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook