MASHAIRI
 

Kubadili anuani

Salamu alaykumu, amani nawaombea,
Ndugu zangu Isilimu, ANNUUR nikipitia,
Nimeishika kalamu, habari kuwaletea,
Nimeona ni muhimu, watunzi kuwaambia,
Kubadili anuani, Mwadui nimeondoka.

Mwadui nimeondoka, nyumbani nimerejea,
Riziki imekatika, mgodi nawaachia,
Kazi yake mtukuka, yote amenipangia,
Wala sinayo mashaka, Mola atanijalia,
Kubadili anuani, Mwadui nimeondoka.

Namshukuru Rabuka, kweli amenijalia,
Kumi na nne miaka, Mwadui kujikalia,
Ualimu kuushika, wanafunzi kuwanoa,
Leo hii kuondoka, salama nafurahia,
Kubadili anuani, Mwadui nimeondoka.

Nimerejea nyumbani, ni hapa Mwanza mjini,
Sehemu ni Mabatini, ni karibu na sokoni,
Barua nitumieni, na nyumbani karibuni,
Anauani nawapeni, nitaiandika chini,
Kubadili anuani, Mwadui nimeondoka.

Samahani marafiki, habari kutowafika,
Kuhama kuna mikiki, muda ulinikatika,
Kwangu ilikuwa dhiki, barua kuziandika,
Naomba mniafiki, msiache kuandika,
Kubadili anuani, Mwadui nimeondoka.

Nawaaga kina mama, pale Shinyanga mjini,
Bi Zuhura nimehama, mtihani wa Manani,
Muhibu Daresalama, Bi Batuli wa Pangani,
Mtandika nimehama, Rufiji nieleweni,
Kubadili anuani, Mwadui nimeondoka.

Zuberi wa Mohamed, Singida kwako Mugoo,
Jumanne bin Undi, Shinyanga Jihad njoo,
Muifanye jitihadi, ANNUUR iwe kioo,
Kwaherini nnarudi, jikoni mboga jogoo,
Kubadili anuani, Mwadui nimeondoka.

Mwl. Zabibu Iddi Ng'onda,
Box 7165,
Mabatini,
Mwanza.


Akhera

Nikifikiri jamani, akhera najililia,
Moyo wangu watamani, nisiitoke dunia,
Nayo haiwezekani, Mola ameahidia,
Sijui nitafanyaje, akhera kuna mazito.

Akhera siitamani, kila nikikumbukia,
Akhera kuna huzuni, nikiwaza najutia,
Akhera ni mtihani, kuushinda nahofia,
Siku hiyo ya Qiyama, nzito inaogopesha.

Qiyama siyo utani, Mola ametuambia,
Qiyama chake Manani, mmiliki tunajua,
Qiyama nambari wani, swala kutuhesabia,
Qiyama ni siku nzito, Yarabi tishio kubwa.

Sina raha asilani, kila nikifikiria,
Hata nile biriani, ni kama najisumbua,
Mawazo yako motoni, Mungu kisha uchochea,
Qiyama kitakapofika, tabu tupu na mashaka.

Nikiwepo kitandani, usingizi unapaa,
Najiona wa motoni, sina kitakachonifaa,
Nimetanguliza nini, mwenyewe najikosoa,
Maisha yake akhera, hasara ni kubwa sana.

Najionea imani, mimi dhaifu najua,
Nitashika mti gani, huo wa kuniokoa,
Yarabi wangu Manani, nisamehe ya dunia,
Unipe chumba cha mwisho, kwa daraja za peponi.

Hakuna kujua mama, baba, shoga, wala mwana,
Roho zataka salama, hakuna saidiana,
Vitisho vyake Qiyama, wote ni kukimbiana,
Tuhurumie Maliki, adhabu hatuiwezi.

Utusamehe Karima, mimi na wangu wazazi,
Tuepushe jahanama, na changu hiki kizazi,
Utuonee huruma, Allahu, Rabbi, Azizi,
Kwetu itakuwa vipi, siku ya msukosuko.

Qiyama kikisimama, mambo yatakuwa wazi,
Kila kitu kitasema, kushitaki kwa Azizi,
Ushahidi kusimama, tutashikwa bumbuazi,
Akhera ni nzito sana, nitamlilia nani?

Mchana ukitokea, na usiku kuingia,
Hasara najipatia, kifo kukimbilia,
Kaburini kuingia, ardhi yaningojea,
Tusamehe ya Al-Jabar, waja wako ni dhaifu.

Askari watiifu, walinzi watasimama,
Malaika watukufu, kwa kumtii Karima,
Wajipange safusafu, ni wapi pa kuegama,
Akhera yakaribia, Al-Ghafuur tusamehe.

Mwl. Zabibu Iddi Ng'onda,
S.L.P. 7165,
Mabatini,
Mwanza.



Mkwezi (swali Na. 2)

Kwa jina la Subhana, ninaishika kalamu,
Niwajuze waungwana, wakae wakifahamu,
Mkwezi tuliyenena, ahadiye ilitimu,
Mkwezi wa sifa gani, mimi atayenifaa?

Mkwezi alipokwama, niliwajuza kaumu,
Zuberi akaja hima, pamoja na Kuluthumu,
Nasaha wakazisema, atawalipa Karimu,
Mkwezi wa sifa gani, mimi atayenifaa?

Mikidadi Burhana, hakusita kukalimu,
Mwinyikai akanena, pikelele kajihimu,
Sharifu aliungana, tawalipa Muadhamu,
Mkwezi wa sifa gani, mimi atayenifaa?

Si kama nilinyamaa, kwa hayo lonilazimu,
Watu niliwagutia, na kuomba kwa Rahimu,
Mkwezi kajiachia, kabla hawajatimu,
Mkwezi wa sifa gani, mimi atayenifaa?

Mkwezi tulimzika, kwa yote yanolazimu,
Hayo ndiyo yalotuka, hadi kimya kikadumu,
Tumuombee Rabbuka, ende Jannatu Naimu,
Mkwezi wa sifa gani, mimi atayenifaa?

Si ndwele yalotendeka, tugange yanolazimu,
Nazi zimeshakauka, kuzivuna yangu hamu,
Nyingine zapukutika, zawa mbata humuhumu,
Mkwezi wa sifa gani, mimi atayenifaa?

Ushauri nautaka, wafaida ya kudumu,
Kwa mkwezi wa hakika, awezaye kazi ngumu,
Ninaogopa hakika, mkwezi mwingine humu,
Mkwezi wa sifa gani, mimi atayenifaa?

Beti tisa zinatosha, majibu ninayo hamu,
Malenga nawaamsha, nyote shikeni kalamu,
Mkwezi gani atosha, kwa sifa zinolazimu?
Mkwezi wa sifa gani, mimi atayenifaa?

Juma M. Bwanakheri,
(Utaadh),
S.L.P. 45245,
Dar es Salaam.



Msikiti rudisheni

Awali amani kwenu, hali nataka kujua,
Kuhusu mimi mwenzenu, sijambo najizuwia,
Tatizo langu ni lenu, ndiyo ninaulizia,
Msikiti rudisheni, ni mali ya Muumba.

Mtume ameondoka, dini ni ya waumini,
Sembuse wewe Mloka, mwenye tamaa moyoni,
Bagamoyo unatoka, unadai udhamini,
Msikiti rudisheni, ni mali ya Muumba.

Walidai Msikiti, Mwembechai Magomeni,
Wakaleta tofauti, vurugu kwa waumini,
Sasa chini wameketi, wakusali hawamwoni,
Msikiti rudisheni, ni mali ya Muumba.

Misikiti ni majumba, ya Mola wetu Manani,
Vipi wewe unatamba, kwa makeke mitaani,
Unapita na jalamba, asubuhi na jioni,
Msikiti rudisheni, ni mali ya Muumba.

Madhambi yenu makubwa, ukifanya tathimini,
Wamekufa waloumbwa, hawakuwa hatiani,
Dhuluma ni jambo kubwa, wacheni ushindani,
Msikiti rudisheni, ni mali ya Muumba.

Watu wengi walilani, mauaji balozini,
Vipi ya Msikitini, mlichokifanya nini?
Chuki kakaa wodini, serikali ni ya nani,
Msikiti rudisheni, ni mali ya Muumba.

Kalamu ninaiwacha, nawahi Msikitini,
Endapo mtauwacha, Mungu tawaghufirini,
Ombeni usiku kucha, Msikiti rudisheni,
Msikiti rudisheni, ni mali ya Muumba.

Zuberi M. Mwinyi (Amir),
P.P. Box 614228,
Dar es Salaam.


Dini tunaiharibu

Dini ni utaratibu, wa maisha yetu sisi,
Dini siyo madhehebu, na wala si taasisi,
Dini si ya Waarabu, na si wa watu weusi,
Kutukanana matusi, dini tunaiharibu.

Dini tunaiharibu, Mola tunapomuasi,
Na kufanya taasubu, kubaguana kwa jinsi,
Sisi tunacho kitabu, ndiyo yetu silabasi,
Kutukanana matusi, dini tunaiharibu.

Pengine ni maaribu, yatuzingayo nafusi,
Shida zinapotuswibu, imani huwa nyepesi,
Ndipo twatia irabu, zitupazo kujihisi,
Kutukanana matusi, dini tunaiharibu.

Nyingi hazina hesabu, mahakamani zetu kesi,
Za kututia aibu, kwa nguvu za ibilisi,
Ambae atughilibu, na kutupa wasiwasi,
Kutukanana matusi, dini tunaiharibu.

Ni wakati wa kutubu, na kufanya majlisi,
Qiyama kiko karibu, kuhukumiwa unasi,
Ni lipi tutalojibu, kwa Rabbi Muumba insi,
Kutukanana matusi, dini tunaiharibu.

Beti sita matulubu, nimezitunga kwa kasi,
Ninahofu Wahhabu, khofu yenye ikhlasi,
Anepushiye adhabu, kubwa na ndogo kiasi,
Kutukanana matusi, dini tunaiharibu.

Beti saba mansubu, hapa ninasema basi,
Washairi mawhubu, nawaachia nafasi,
Mimi bado ni naibu, nyinyi ndio maraisi,
Kutukanana matusi, dini tunaiharibu.

Khamisi Juma Sibura,
S.L.P. 164,
Majengo - Shinyanga



Aprili Moja si yetu

Bismillahi naanza, kwa jina la Mola wetu,
Islamu kuwaasa, uwongo si mila yetu,
Sikukuu kuiacha, ni yao wala si yetu,
Aprili moja siku, Islamu si ya kwetu.

Wajinga walianza, kuwaongopea watu,
Sikukuu kuanzisha, eti nini ya wapumbavu,
Siku huadhimishwa, kuwadanganya watu,
Aprili moja siku, Islamu si ya kwetu.

Matukio huanzishwa, uongo si kweli katu,
Gazetini huandikwa, ili kuwapasha watu,
Habari zisohakika, ili kupumbaza watu,
Aprili moja siku, Islamu si ya kwetu.

Mtume amekataza, uwongo kila mtu,
Isipokuwa ameacha, katika sehemu tatu,
Na hizo hakuzitaja, ziazimishwe na watu,
Aprili moja siku, Islamu si ya kwetu.

Kwanza ameutaja, kwa kupatanisha watu,
Uwongo waweza kuja, ili kuvuruga watu,
Mfarakano si tija, haitaki dini yetu,
Aprili moja siku, Islamu si ya kwetu.

Pili amesisitiza, kwa mume na mke mtu,
Mume apataliwaza, mke uwongo mtupu,
Apate kufarijika, kwa yake masumbufu,
Aprili moja siku, Islamu si ya kwetu.

Tatu, imekubalika, kwenye vita vya mtutu,
Ili waje salimika, wasipungue wenzetu,
Waweze kuendeleza, mapambano dini yetu,
Aprili moja siku, Islamu si ya kwetu.

Hapa mwisho nimefika, endelea sithubutu,
Ujumbe kufikisha, Islamu ndugu zangu,
Sikubali kuitika, furahia sikukuu,
Aprili moja siku, Islamu si ya kwetu.

Ramadhani H. Bakari,
Kisiju - Pwani.
 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook