SOMO lililopita tuliangalia maana ya siasa na tukachambua mifumo ya siasa tukaona umegawanyika katika sehemu mbili: Mifumo ya siasa iliyobuniwa na wanadamu na ule wa Kiislamu. Tulianza na kuliangalia kwa kina kidogo mifumo iliyobuniwa na wanadamu... Endelea
(ii) Mfumo wa siasa za utumwa
Mfumo wa sisa za kitumwa unafuatia baada ya ujima katika mlolongo wa siasa za kitwaghuti. Huu ni mfumo wa siasa za kitabaka huruhusu baadhi ya watu kuishi kwa jasho la watu wengine. Watu hao wenye fursa za mali au hadhi katika jamii huishi kwa kuwatumikisha wengine. Katika mfumo huu, utawala ulikuwa mikononi mwa matajiri ambao waliendesha siasa za kuwatumikisha wengine na wao kuishi maisha ya raha. Chini ya mfumo huu wa siasa, uzalishaji mali uliwekwa migongoni mwa watu wa tabaka la chini la watwana.
Inaelezwa na wachambuzi kuwa mfumo huu wa kitumwa ulianza kuyumba kwa migongano mbalimbali. Watumwa walianza kuamka na kujidhatiti kisha kuanza kupinga vikali sana hali hiyo ya utumwa. Nao Watu ambao awali walinyang'anywa mali zao na mabwana wenye watumwa waliungana na watumwa yakawa mapambano ya watwana na mabwana hatimaye kuufuta utumwa.
(iii) Mfumo wa siasa za Kimwinyi
Siasa za Kimwinyi ambazo inadaiwa zilifuatia baada ya siasa za kitumwa. nazo vile vile zilikuwa na minyororo yake. Katika mfumo huu tabaka la kimwinyi lilitawala njia zote za kijamii. Njia za uchumi zilitawaliwa kwa kukodisha mashamba halafu kutoa fungu kubwa kwa mwenye shamba wakati wa mavuno. Wazalishaji kwenye mashamba hayo chini ya mfumo huu, tofauti na utumwa, walilipwa posho ndogo kama malipo ya kazi nzito walizotumikishwa na mabwanyenye. Inadaiwa kuwa taasisi za dini pia zilitumika "kuhalalisha" ubwana na utwana! Mfumo wa siasa za kimwinyi ulisita kuendelea baada ya wanyonywaji kujiunga pamoja dhidi ya wanyonyaji.
(iv) Mfumo wa siasa za kibepari
Siasa za kibepari ni moja ya mifumo ya Kitwaghuti iliyokita mizizi katika jamii nyingi. Katika mfumo huu kila kitu kinachowezekana kufanywa ili "kuzalisha" pesa hufanywa. Wachache walio na fursa za mali na hadhi ndiyo huendesha masuala yote ya jamii na kundi kubwa la wanajamii huishi kwa kuuza nguvu, vipaji na taaluma zao kwa wachache hao, na wale wasio na chochote hulazimika kuishi maisha ya magumu na ya kubahatisha (kwa upande wa wanawake) kuuza miili yao, na wanaume kufanya vitendo vyovyote vile ili mradi wapate pesa.
(v) Mfumo wa siasa za Kijamaa (Kikomunisti)
Katika mfumo huu uliodhaniwa na waasisi wake kuwa ungelimkomboa mwanaadamu na kuleta "usawa wa sare", chama ndicho hushika hatamu zote na "kuwakilisha matakwa ya walio wengi" katika jamii. Aidha hudaiwa kuwa jamii chini ya mfumo huu wa siasa watu huwa huru kabisa na kuwa na "demokrasia" halisi. Hata hivyo historia inaonyesha kuwa chini ya mfumo huu wa siasa, jamii hupumbazwa na kudumazwa kwa njia mbalimbali. Kwa kuwa chama hushika hatamu za maongozi, ni kamati ya watu wachache tu ndani ya chama hicho ndio huendesha masuala yote ya utawala. Hudhibiti kila kitu kwa kuimarisha ulinzi wa siri ambao hupenyezwa kila eneo la jamii. Huendesha propaganda dhidi ya wale wote wenye fikra tofauti na zao ambazo huziita ni "sahihi na za kudumu". Njia zote za uchumi huwa chini ya kikundi hicho cha watu kwa sura ya "mali ya umma" Katika Tasnifu (thesis) yake ya shahada ya udaktari wa Falsafa mwaka 1946, Dr. Raufiddin, aliandika juu ya kuporomoka kwa siasa hii kama ifuatayo:
"Marxism (Communism), like every wrong ideal, contains the germs of its own dissolution and must break up sooner or later"
"Umaksi (Ukomunisti) kama ilivyo itikadi yoyote ile ya urongo, umebeba sumu ya kujimaliza wenyewe, hivyo lazima uporomoke hivi karibuni au baadae".
Hali ilizidi kuwa ngumu katika nchi viranja wa siasa hii, kufikia mwaka 1989 miaka 70 ya mapinduzi hayo ya Kikomunisti, Urusi ilisambaratika na huo ukawa ndio mwisho wa siasa hiyo.
(vi) Mfumo wa siasa za Kidemokrasia
Wataalamu wa mambo ya siasa wanaeleza kwamba Demokrasia (Democracy) ni neno la Kiyunani (Kigiriki); muungano wa maneno mawili; Demos - chombo cha raia (the citizen body) na cracy ni utawala. Hivyo kimaana Democracy ni chombo cha utawala wa raia.
Kiasili Demokrasia inarejea hadi uyunani ya kale ikiwa na maana finyu tu ambapo wanawake, watumwa, vijana waliokuwa chini ya umri wa miaka 30 na wale wote ambao hawakuweza kukamata silaha hawakujumuishwa katika chombo hicho kilichofahamika kama harakati za utawala wa Wanyonge.
Hata hivyo hivi leo Demokrasia
hufahamika kama ni utawala wa watu uliowekwa na watu kwa ajili ya watu
(the government of the people by the people for the people). Au
ni uhuru wa kujiamulia mambo ya mtu apendavyo! Kutokana na tafsiri hiyo,
kisiasa, kuna aina tofauti za miundo ya demokrasia, kwa mfano kuna demokrasia
ya chama kimoja, demokrasia ya vyama viwili, demokrasia ya vyama vingi;
demokrasia ya kiliberali ambao ina demokrasia ya moja kwa moja (direct
democracy) na demokrasia ya uwakilishi (representative democracy),
n.k.
|
|