JIFUNZE SHERIA
 
Uendeshaji wa Mashitaka
 
Na Dkt. Abdallah J. Saffari
 

Mkurugenzi wa Mashitaka ya Jinai

UAMUZI wa kufungua, kuondoa au kufuta mashitaka umo mikononi mwa Mkurugenzi wa Mashitaka ya Jinai. (F.90, Sheria ya Mwenendo wa Jinai Na. 1, 1985). Lakini kutokana na aina ya wingi wa makosa ya jinai ni vigumu wajibu huo utekelezwe na Mkurugenzi wa Mashitaka ya Jinai pekee. Hata wale maofisa ambao wako moja kwa moja chini ya Mkurugenzi wa Mashitaka ya Jinai kama vile baadhi ya Mawakili wa serikali, kwa pamoja, hawawezi kushughulikia mashauri yote ya jinai.

Hivyo Mkurugenzi wa Mashitaka ya Jinai ameteua waendesha mashitaka ambao humsaidia katika moja ya shughuli zake muhimu - kuendesha kesi mahakamani. (G.92, Sheria ya Mwenendo wa Jinai i.h.j). Waendesha mashitaka wengi ni polisi na mawakili wa serikali. Lakini aghalabu uamuzi wenyewe wa kumshitaki mtu au haufanywi na waendesha mashitaka wenyewe. Uamuzi huo unaweza kufanywa na Mkuu wa Kituo cha Polisi, Mkuu wa Polisi wa Wilaya, Mkuu wa Upelelezi wa Jinai wa Mkoa au Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai kufuatana na mkondo wa utendaji wa Jeshi la Polisi. Kwa upande mwingine uamuzi huo unaweza kufanywa na mawakili wa serikali au Mkurugenzi wa Mashitaka ya jinai mwenyewe.

Kwa kawaida, mashauri madogo hughushulikiwa katika ngazi za chini ili kuwapa nafasi Wakuu wa Polisi waliotajwa kughuhulikia mashauri mazito. Na mashauri machache ambayo ni mazito zaidi ndiyo hufikishwa kwa mawakili wa serikali na Mkurugenzi wa Mashitaka ya Jinai mwenyewe.

Kuna baadhi ya mashitaka ambayo hayawezi kuendeshwa bila ya kibali cha Mkurugenzi wa Mashitaka ya Jinai. Nayo ni kama vile kusababisha hasara kwa vyombo vya umma kutokana na uzembe (F.59(2) pamoja na aya ya 11(1) ya jedwali la Kwanza ya sheria ya makosa ya Hujuma za Uchumi Na. 2, 1994) au kuwa na mali inayotuhumiwa imepatikana kwa rushwa (F.90 na 18, Sheria ya Kuzuia Rushwa Na. 16, 1971).

Karibuni mashauri yote katika mahakama ya wilaya huendeshwa na polisi isipokuwa yale mazito au yenye utata wa kisheria ambayo hushughulikiwa na mawakili wa serikali. Jambo hili limeleta matatizo makubwa mawili. Kwanza, kadiri siku zinavyoendelea ndivyo mbinu za utendaji wa makosa hukua na kufanya upelelezi kuwa mgumu zaidi. Aghalabu majalada mengi zaidi hupelekwa katika ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka ya Jinai kutaka maoni yake kama ushahidi unatosha kumfungulia mashitaka mtuhumiwa, na mashitaka yapi hayo. Kutokana na uhaba wa mawakili wa serikali maoni ya Mkurugenzi wa mashitaka ya jinai hupatikana baada ya muda mrefu. Sio hivyo tu; uendeshaji wa mashauri wenyewe mahakamani pia huwa mgumu kulingana na mbinu ziilzotumiwa katika kutenda makosa yanayohusika.

Hata hivyo, watu binafsi, kwa ruhusa ya mahakama, wanaweza kufungua na kuendesha mashtaka ya jinai wenyewe katika mahakama ya Wilaya au Hakimu Mkazi. (F.99(1), Sheria ya Mwenendo wa Jinai i.h.j. Shauri la R, v. Nyirenda, 1985, Mahakama ya Kisutu, Dar es Salaam ni mfano mzuri. Mshitakiwa alishitakiwa kwa kuvunja amri ya mahakama. Shauri liliendeshwa na Profesa Shivji kutoka Kamati ya Msaada wa Sheria, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam).

Katika Mahakama ya Mwanzo mawakili au waendesha mashitaka wa serikali hawaruhusiwi kuwakilisha upande wowote ule. (F.33(1), Sheria ya Mahakama ya Mahakimu Na. 2, 1994). Bali inastaajabisha kuwa mara nyingi askari polisi huendesha mashitaka dhidi ya washitakiwa badala ya walalamikaji wenye kufanya hivyo. Hakika kitendo hicho ni athari ya kimsingi inayoupa upande mmoja uwezo mzuri wa kutumia watu wenye ujuzi kuendesha mashitaka dhidi ya mtu ambaye anakatazwa na sheria kutetewa na wakili. Suala hili halijafikishwa kwenye mahakama kuu hivyo haieleweki kama hukumu ya kumtia hatiani mshitakiwa ambaye mashitaka dhidi yake yaliendeshwa na polisi ni batili au la. Hata hivyo tunafikiri itategemea tafsiri ambayo itapewa neno 'may appear' katika kifungu kinachokataza uwakilishi huo. ( K.h.j.).

Njia inayopasa kutumiwa kuendesha mashitaka ni kwa mlalamikaji kutoa malalamiko yake kwa Hakimu wa mahakama hayo ambaye atatayarisha hati ya mashitaka rasmi dhidi ya mshitakiwa ambaye, baada ya kuhudhuria shaurini, atasomewa hati hiyo ili atoe majibu yake. Ikiwa atakana mashitaka basi mashahidi wataitwa na mahakama kama wanavotajwa na mlalamikaji: (kwa kawaida mlalamikaji ndiye shahidi mkuu wa mashitaka). Sehemu kubwa ya kuhoji mashahidi hao hufanywa na Hakimu mwenyewe pamoja na wazee wa baraza. Halikadhalika mashahihidi wa mshitakiwa, kama wapo, huhojiwa na Hakimu pamoja na wazee wa baraza. Mshitakiwa atapewa fursa ya kumhoji kila shahidi wa mashitaka baada ya kuhojiwa na mahakama.

Hali ni tofauti katika Mahakama ya Wilaya na Mahakama Kuu ambako waendesha mashitaka wa serikali, yaani pamoja na polisi na mawakili, huweza kuwakilisha upande wa mashitaka, na ambako mshitakiwa huweza kutetewa na wakili.

Hati ya mashitaka mahakama ya wilaya huweza kutayarishwa na Hakimu baada ya kuridhika na malalamiko ya mlalamikaji dhidi ya mtuhumiwa kama vile ilivyo katika mahakama ya mwanzo. (F.128(5), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Mlalamikaji anaweza kutoa malalamiko yake kwa maneno au maandishi na, kinadharia, anaweza hata akatayarisha hati ya mashitaka mwenyewe ambayo itatiwa saini naye pamoja na Hakimu. (F.128(5), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Lakini kwa vile utayarishaji wa hati ya mashitaka, kama ambavyo itaelezwa punde tu, huhitaji utaalamu wa sheria, inabidi na ni vyema Hakimu atayarishe hati hiyo. Njia hiyo, hata hivyo, haitumiki sana siku hizi. Badala yake inatumika ya pili ambayo mlalamikaji hutoa malalamiko yake kwa polisi ambao baada ya kuridhika kuwa kuna ushahidi wa kutosha dhidi ya mshitakiwa, hutayarisha hati ya mashitaka dhidi ya mtuhumiwa.

Hati ya mashitaka rasmi katika Mahakama Kuu hutayarishwa na Mkurugenzi wa Mashitaka ya Jinai au mawakili wa serikali kwa niaba yake.

Mashitaka rasmi dhidi ya mshitakiwa huanza pale hati ya mashitaka inapofikishwa mahakamani.

Mamlaka na uwezo wa Mkurugenzi wa Mashitaka mintaarafu ya kuendesha mashauri ya jinai ni mkubwa mno. Katika utendaji wa kazi yake hiyo hawajibiki kukubali maoni au ushauri wa mtu yeyote yule ila Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (F.90, Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Anasimamia uendeshaji wa mashauri yote ya jinai kuanzia Mahakama ya Mwanzo hadi Mahakama ya Rufani ya Tanzania. Mathalan ingawa mlalamikaji huendesha kesi yake mwenyewe dhidi ya mashitakiwa katika mahakama ya mwanzo, Mkurugenzi wa Mashitaka anaweza kuingilia kati kama ni lazima. Na katika hatua yoyote ile ya shauri, iwapo ataona sawa kufanya hivyo, anaweza kulifuta au kuliondoa shitaka dhidi ya mshitakiwa, hata kama ni wakati wa hukumu inaandikwa. (F.91(1), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Anao pia uwezo wa kuyafufua mashitaka aliyoyafuta au kuyaondoa kwa kudiri sheria inavyoruhusu. Mamlaka ya kukata rufani zote za jinai yako chini yake. (F.379, Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j).

Hati ya Mashitaka

Hati ya Mashitaka ni msingi wa kunzisha mashitaka rasmi dhidi ya mshitakiwa. Kuna masharti kadhaa kuhusiana na uandishi wa hati za mashitaka ambayo ni muhimu mno kuzingatiwa. Masharti hayo yana madhumuni ya kumfanya mshitakiwa aelewe hasa kosa ambalo anadaiwa amelitenda japo kwa muhtasari ili aweze kujiandaa na utetezi wake.

Kabla ya kuangalia masharti ya kuzingatia katika uandishi wa hati za mashitaka ni vizuri kugusia kwamba sheria inazungumzia Hati ya Mashitaka na Taarifa ya Mashitaka.

Taarifa ya Mashitaka haina tofauti za kimsingi na Hati ya Mashitaka isipokuwa katika uandishi wake ambapo hueleza kuwa mahakama yanaarifiwa na Mkurugenzi wa Mashtaka kwamba mnamo tarehe kadha mshitakiwa kwa kosa kadha. Kama itakavyoonekana katika sehemu inayofuata huko mbele, kuna baadhi ya makosa ambayo huweza kusikilizwa na Mahakama Kuu ambayo ndiyo yenye uwezo wa kufanya hivyo, kwa mfano kuzinga na maharimu au mauaji.

Tofauti nyingine ni kuwa taarifa za mashitaka hutumika Mahakama Kuu tu. Vinginevyo masharti yote yanayotakiwa kuzingatiwa katika uandishi wa Hati za Mashitaka ni muhimu vile vile kwa utayarishaji wa Taarifa za Mashitaka.

Mfano ufuatao unaonyesha tofauti ya kimaandishi baina ya Hati ya Mashitaka na Taarifa ya Mashitaka mintaarafu ya kosa la kuzinga na maharimu. Tunaanza na Hati ya Mashitaka.

KATIKA MAHAKAMA YA WILAYA

KISUTU, DAR ES SALAAM

Mashitaka

Maelezo ya Kosa

Kuzinga na Maharimu dhidi ya fungu la 158 la Kanuni ya Adhabu

Muhtasari wa kosa

Ramadhani Masunga, kwamba mnamo tarehe 8 Mei, 1994, Temeke, Dar es Salaam alizinga na Maimuna Athumani akielewa kuwa ni dada yake.

Saini
Mwendesha Mashitaka
Dar es Salaam
Tarehe

Taarifa ya mashitaka hayo hayo, baadaye itakuwa na sura ifuatayo:

KATIKA MAHAKAMA KUU YA TANZANIA, DAR ES SALAAM

Taarifa ya Mashitaka

Katika kikao cha Mahakama kitakachofanyika tarehe 20 Julai, 1995 Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Mashitaka ya Jinai, kwa niaba ya Jamhuri ya Muungano, anayaarifu Mahakama kuwa Ramadhani Masunga atashitakiwa kwa kosa lifuatalo, yaani:

Maelezo ya Kosa

Kuzinga na Maharimu dhidi ya fungu la 158 la Kanuni ya Adhabu.

Muhtasari wa Kosa

Ramadhani Masunga, kwamba mnamo tarehe 8 Mei, 1995, Temeke, Dar es Salam alizinga na Maimuna Athumani akielewa ni dada yake.

Saini

Mkurugenzi wa Mashitaka
Dar es Salaam
Tarehe

Sharti moja muhimu katika uandishi wa Hati ya Mashitaka au Taarifa ya Mshitaka ni kuwa kwanza lazima kuwe na maelezo ya kosa linalodaiwa dhidi ya mshitakiwa. (F.132, Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Kama ni wizi basi maelezo yataeleza hivyo na kutaja fungu ambalo kosa hilo huadhibiwa. Wakati mwingine maelezo ya kosa hufafanuliwa na fungu jingine la adhabu kuelezwa na fungu mbali na hilo. Mfano ni wizi ambao hufafanuliwa katika fungu la 258 ambapo adhabu huelezwa katika fungu la 265. Hivyo ni makosa kwa hati ya mashitaka ya wizi kutoa maelezo ya kosa kwa mujibu wa fungu la 258 badala ya fungu la 265.

Kwa vile Hati na Taarifa za Mashitaka ni msingi wa kesi yenyewe ni muhimu maelezo ya kosa yataje fungu sahihi la sheria ambalo kweli huonyesha kosa linalodaiwa dhidi ya mshitakiwa. Katika shauri la Azone v. Uganda. (1969) E.A. 129) mrufani alishitakiwa na kupatikana na hatia ya makosa ya kuchukua mkopo kwa udanganyifu, kughushi maandishi na kujisingizia kuwa ni Naibu Waziri wa Afya wa Kenya. Maelezo ya makosa katika Hati ya Mashitaka dhidi yake yalitaja mafungu ya sheria ambayo hayakuwa sahihi. Kwa mfano kuhusiana na kosa la kughushi maandishi maelezo ya mashitaka yalitaja fungu la 326(1) la Kanuni la Adhabu badala ya fungu la 326. Kutokana na hali hiyo mahakama yaliona dhahiri kuwa fungu hilo la sheria ambalo mshitakiwa alishitakiwa nalo halikuwepo. Athari hiyo ilionekana kubwa lakini kwa kuwa kosa hilo lilikuwako chini ya fungu la 326 la Kanuni ya Adhabu na kwamba ushahidi ulionyesha haki ilitendeka licha ya athari hizo, hukumu ya mahakama ya awali iliachwa kama ilivyokuwa.

Itaendelea toleo lijalo
 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook