Tunaendelea na maelezo yetu juu ya mambo ya kuyaangalia unapotaka kununua kompyuta sasa hivi. Katika sehemu zilizopita tumezungumzia CPU, Motherboard na RAM. Kwenye sehemu hii tutaviangalia baadhi ya viungo muhimu ambavyo bado hatujavielezea.
Monita
Monita ni kitu muhimu sana kwani ndiyo unayoiangalia wakati wote unapotumia kompyuta yako. Kila monita ikiwa kubwa ndio barabara. Kwa siku hizi usinunue monita iliyo na ukubwa wa chini ya inchi 15, lakini ni vyema zaidi kununua ya inchi 17.
Vitu muhimu vinavyotafautisha monita moja na monita nyengine ni pamoja na:
Viewable image size (v.i.s)
Dot-pitch (dp)
Maximum resolution
Refresh rate
Ingawa unaweza kuona monita imesemwa kuwa ni ya inchi 17, sehemu ya kioo chake ambayo picha inaweza kuonekana ni ndogo zaidi ya hapo, pengine inchi 16 tu. Hiyo ndio huitwa viewable image size, kwa ufupi v.i.s, ambayo huwa tafauti kati ya monita na monita hata kama zinasemwa kuwa zote ni za ukubwa mmoja. Viewable image size hupimwa kimshazari (diagonally), na kila ikiwa kubwa ndio bara bara.
Kila monita imepakwa vidoto au mistari ya maadini ya phosphor yenye sifa ya kung'ara yanapogongwa na mionzi ya electrons. Monita za rangi huwa na phosphor za rangi nyekundu, kijani na buluu. Urefu kati ya vidoto au mistari ya phosphor ya rangi moja huitwa dot-pitch, kwa ufupi dp. Dot-pitch hupimwa kwa millimetre (mm) na kila dot-pitch ikiwa ndogo ndio picha inavyoonekana safi zaidi.
Tatizo ni kuwa baadhi ya watengenezaji wa monita hutumia udanganyifu wanapotoa ukubwa wa dot-pitch, na hii inasababishwa zaidi na njia mbali mbali zinazotumiwa kupima dot-pitch. Ikipimwa kimshazari (diagonal) dot-pitch huwa kubwa zaidi kuliko ikipimwa kwenye mstari uliolala (horizontal). Kwa mfano 0.28mm dp (diagonal) ni sawa na .25mm dp (horizontal). Kwa ujumla, hata hivyo, monita nyingi za siku hizi zinakuja na dot-pitch ya udogo wa kutosha kutoa picha nzuri. Dot-pitch ya kuanzia .28mm kujia chini inatosheleza haja. Na kwa kweli huwezi kuona tafauti kubwa kati ya monita ya .28dp na ya .25dp ingawa bei inaongezeka kila dot-pitch inapokuwa ndogo.
Resolution ya monita hupimwa kwa idadi ya pixels (picture elements) inazoweza kuzionesha kiupana na kwendea chini. Kila resolution inapokuwa kubwa ndivyo picha inavyoonekana safi zaidi. Kwa uzoefu wangu, resolution ya juu (maximum resolution) ya 1280x1024 inatosheleza kabisa.
Kawaida ya phosphor inapogongwa na mionzi ya electrons huwaka lakini baada ya muda mfupi huzimika. Inabidi ipitishiwe tena mionzi ya electrons ili iendelee kuwaka. Kama inachukua muda mrefu kupelekewa mionzi ya electrons monita inaweza kuonekana kama inapepesa. Refresh rate ni kipimo cha kuonesha ni mara ngapi kwa kila sekunde picha inachorwa upya kwenye kioo cha monita. Kila refresh rate ikiwa kubwa basi picha inaonekana safi zaidi. Refresh rate ya kuanzia 72Hz (non-interlaced) na kuendelea, inatosheleza kabisa.
Baadhi ya monita haiviwashi vidoto vyote vya phosphor kila mara bali huviwasha kwa kupishana. Yaani mkupuo mmoja inavichora vilivyo kwenye mstari wa kwanza, wa tatu, wa tano, n.k, na mkupuo wa pili inaviwasha vidoto vilivyo kwenye mstari wa pili, wa nne, wa sita, n.k. Mtindo huo unaitwa "interlacing". Monita zinazotumia "interlacing" si nzuri. Nzuri zaidi ni zile zinazoviwasha vidoto vyote kwa mkupuo mmoja, yaani non-interlaced. Refresh rate ya monita inategemea kama ni interlaced au non-interlaced. Kwa kutumia interlacing, vidoto vichache tu vinawashwa na kwa hivyo refresh rate inaweza kuonekana kubwa zaidi kuliko ile ya non-interlaced ambayo inawasha vidoto vingi zaidi, ingawa monita bora ni ile ya aina ya non-interlaced.
Mambo mengine ya kuangalia ni watengenezaji. KTX, AOC, Daytek, KDS, Goldstar, ni kati ya watengenezaji dhaifu wa monita. Monita madhubuti ni za Sony, NEC, Viewsonic, MAG, Hitachi, Digital, n.k. Watu wengi hupendelea monita zenye vioo bapa (flat screen) ambazo kwa bahati mbaya ni ghali zaidi. Na siku hizi pia monita zinazopendelewa ni zile zinazojuilikana kama short-depth monitors ambazo ni fupi na hazichukui nafasi kubwa kwa kwendea nyuma yaani huwa na CRT (Cathode Ray Tube) fupi.
Lakini cha muhimu ni kununua monita ambayo ina sehemu za kurekebishia mambo mbali mbali ya picha inayoonekana kwenye kioo cha monita mambo kama mwangaza (brightness), usafi (contrast), upana na urefu wa picha, n.k. Na zaidi, ni vyema kuchagua monita ambayo ina uwezo wa kutumia umeme wowote kati ya 110V na 250V yaani free voltage. Monita za namna hiyo ni muhimu kwenye nchi ambazo umeme unaongezeka na kupungua mara kwa mara.
|
|