TAHARIRI
Madhumuni ya Shahada
 
MAANA ya shahada ni kuwa hapana Mola ila Allah na Muhammad (s.a.w.) ni Mjumbe wa Allah. Neno 'Allah' katika Shahada linamaanisha Mungu, Ambaye ni Bwana, Muumba, Mlishaji, Mruzuku, ambaye husikiliza maombi yetu na huyajibu, na ambaye anastahiki ibada yetu. Pale usemapo, La ilaha illallah, inamaanisha kwanza, kwamba umetambua na kukiri kuwa ulimwengu haukutokea bila ya uwezo wa kuumba wa Mwenyezi Mungu, na wala si kweli kuwa una miungu wengi. Hakika una Mungu mmoja tu, naye ni Muadilifu, na hamna yeyote mwenye uwezo wa kiungu isipokuwa Yeye tu. Pili, lingine unalokiri katika Shahada ni kwamba Mungu Huyu Huyu ambaye ndiye Mungu wako pia ndiye Mungu wa ulimwengu wote. Vyote unavyovimiliki na vyote vilivyomo ulimwenguni ni Vyake Yeye. Yeye ndiye Muumba, Naye ndiye Mruzuku. Uhai na umauti vyote vimo chini ya mamlaka yake. Dhiki na faraja vinatokea kwa tawfiq Yake. Chochote akipatacho mtu amepewa na Yeye. Chochote kinachomtoka mtu, kwa hakika humtoka kwa amri Yake. Yeye Peke Yake ndiye wa kuogopwa. Yeye Peke yake ndiye wa kuombwa na kutegemewa kukidhi mahitaji yetu. Yeye Pekee ndiye wa kuabudiwa. Sisi sote si watumwa wala watumishi wa yeyote isipokuwa Yeye, Naye Ndiye Pekee Bwana na Mtawala wetu. Jukumu letu halisi ni kukubali amri Zake na kikamilifu kufuata na kutii Sharia Yake.

Hii ndio ahadi unayofunga na Allah mara tu baada ya kutamka La ilaha illallah, na kwa kufanya hivyo unaufanya ulimwengu mzima shahidi juu yako. Ukiivunja ahadi hii, mikono na miguu yako, kila unywele wako, na kila chembe ya ardhi na mbingu ambavyo mbele zao uliweka ahadi, vitatoa ushahidi dhidi yako katika mahakama ya Allah ambako utakuwa kizimbani katika hali ya udhalili mno kiasi ambacho hutakuwa na hata mmoja wa kukutetea. Hutakuwa na wakili wala mwanasheria wa kukusaidia katika kesi yako.

Kwa hakika mawakili na wanasheria ambao katika mahakama za ulimwengu huu wanaifanyia istihzai na kuipotosha sharia kwa ajili ya maslahi ya kilimwengu, wao wenyewe katika mahakama ya Allah watasimama katika dhila kama wewe. Mahakama hiyo si ya kukuachia kwa ajili ya mbinu, udanganyifu au hila. Unaweza kuwaficha hatia zako polisi wa dunia, lakini katu huwezi kuwaficha chochote polisi wa Allah. Polisi wa dunia hupokea hongo na rushwa kinyume na polisi wa Allah. Mashahidi wa duniani wanaweza kutoa ushahidi wa uongo, lakini sio mashahidi wa Allah, kwani ni waaminifu sana mno kabisa. Watawala wa ulimwengu wanaweza kufanya dhulma, lakini Allah ni Mtawala Muadilifu Asiyefanya dhulma. Na tena hamna kuepa wala kutoroka katika jela ya Allah ambapo huwafunga wahalifu. Ni ujinga mkubwa na kwa hakika ni upumbavu mkubwa kuliko wote kumfanyia Allah ahadi ya uongo. Unapoweka ahadi hii, kwanza fikiri vizuri sana, kisha itekeleze kikamilifu, kwani hukulazimishwa shingo upande utamke shahada. Kwani maneno matupu hayana manufaa yoyote.

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook