Huu mwaka wenye miezi ya Januari, Februari n.k. ingawa ndio uliozoeleka, na ndio unaosherehekewa kwa vifijo na hoihoi kila pale unapomalizika mwezi wa Disemba na kuingia Januari; lakini kwa kweli, huo ni mwaka wa kikristo. Mwaka huo unaitwa A.D., ambacho ni kifupi cha maneno mawili ya kilatini ANNO DOMINI, yakiwa na maana ya mwaka wa bwana; yaani mwaka aliozaliwa Yesu Kristo. Kwa kalenda ya kiristo huu ni mwaka 1999 A.D.
Inasikitisha sana kuona Waislamu wakiupapatikia sana kuusherehekea mwaka huo wa kikristo na huku wakiwa hawana habari kabisa ya kutoka na kuingia kwa mwaka wa Kiislamu! Kwa mujibu wa kalenda ya Kiislamu. juzi tarehe 1 Muharram, tuliuaga mwaka wa 1419 Hijiryya, na kuukaribisha mwaka 1420.
Hii haina maana kwamba kabla ya kuanzishwa kwa mwaka wa Kiislamu kulikuwa hakuna utaratibu wa kuhesabu miezi, na miaka. Hapana! Ulikuwapo utaratibu huo. Mwenyezi Mungu (s.w.) anasema: "Yeye ndiye aliyelifanya jua kuwa mwanga, na mwezi kuwa nuru, na akaupimia vituo (huo mwezi), ili mjue idadi ya miaka na hesabu nyinginezo." (Yunus 10:5).
Pili, baadhi ya masahaba walimwuliza Mtume (s.a.w.) juu ya mabadiliko ya mwezi; kwa nini mara nyingine uonekana mwembamba, mara uwe nusu, na mara nyingine uwe kamili? Mwenyezi Mungu (s.w.) akamwagiza Mtume (s.a.w.) awajibu, "Wanakuuliza juu ya miezi miandamo. Sema, 'Hiyo ni vipimo vya nyakati kwa ajili (ya mambo) ya watu na ya Hijja." (Al-Baqarah 2:189).
Tatu, Kur'ani Tukufu inaeleza kuwa tokea kuumbwa kwa ulimwengu Mwenyezi Mungu (s.w.) alikwisha panga kuwa mwaka mmoja uwe na miezi kumi na mbili. Mwenyezi Mungu (s.w) anasema, "Idadi ya miezi (ya mwaka mmoja) mbele ya Mwenyezi Mungu ni miezi kumi na mbili katika ilimu ya Mwenyezi Mungu (tokea) siku alipoumba mbingu na ardhi." (At-Tawba 9:36).
Aya hizi tatu tulizozitaja zinatosha kuwa dalili ya kwamba kweli Waislamu walikuwa wana utaratibu maalumu wa kupima nyakati za mambo yao kwa kutumia jua na mwezi. Walilitumia jua kuelewa siku inayoingia na kutoka pia kufahamu nyakati za kuingia na kutoka kwa vipindi vya sala, pamoja na kutambua muda wa kuanza kufunga na kufungua saumu zao. Na waliutumia mweizi kujua tarehe za siku mbalimbali, miezi na miaka, ili waelewe nyakati za kutekeleza ibada zao.
Labda swali la kujiuliza ni kuwa ikiwa tokea awali Waislamu walikuwa wana utaratibu maalumu wa kuhesabia nyakati za mambo yao, kwa nini tuseme kuwa kalenda au mwaka wa Kiislamu ulianzia baada ya Hijra? Naam, hiyo ni kwa sababu ingawa walikuwa na utaratibu kama huo; lakini walikuwa hawana mwaka maalumu wa kuanzia tarehe yao.
Katika uhai wa Mtume (s.a.w.) haikutokezea kuja ya kuwa na mwaka mahususi wa Kiislamu. Ilikuwa ni baada ya kufariki Mtume (s.a.w.) pamoja na khalifa wake wa kwanza, Sayyidna Abubakar Siddiq (r.a.), na baada ya kupita miaka 16 tokea Mtume (s.a.w.) afanye safari ya Hijra, katika zama za Khalifa wa Pili, Seyyidna Umar ibn Al-Khattab (r.a.) ndiyo ikatokea haja ya kuwa na mwaka wa Kiislamu.
Kwa kauli yenye nguvu, inasemekana watu wawili walishitakiana kwa Seyyidna Umar ibn Al-Khattab (r.a.) juu ya mmoja wao kumkopesha mwenziwe fedha na mdaiwa akashindwa kulipa deni hilo katika muda walioandikiana. Katika hati yao ya mapatano wakiandikiana mdaiwa alilipe deni hilo mwezi wa shaabani, bila ya kuainisha mwaka wenyewe.
Seyyidna Umar (r.a.) alipopewa hati hiyo na kuisoma aliiona kasoro hiyo. akawauliza wamekubaliana deni lilipwe katika Shaabani ya mwaka gani? Mbona hati haionyeshi mwaka wa kulipa?
Sayyidna Umar akashindwa kumchukulia hatua yule mdaiwa. akaona
, ili kuepusha isitokee mizozo mingine ya aina hiyo bora na Waislamu nao wawe na mwaka wao watakaoweza kuutumia rasmi katika mikataba na kumbukumbu zao. Basi alishauriana na masahaba wenziwe na wakakubaliana juu ya kuanzisha mwaka huo, Pia, walikubaliana mwaka huo uanzie wakati ule Mtume (s.a.w.) alipohama Makka na kwenda Madina. Na mwisho, wakachagua mwezi wa Muharram uwe ndio mwezi wa mwanzo wa mwaka wa Hijjriyya.
Ndiyo maana hivi sasa kila unapoingia mwezi wa Muharram tunasherehekea kuingia mwaka mpya wa Kiislamu. Katika hizi nchi zetu historia imetunyima fursa ya kusherehekea mwaka wa Kiislamu, kwa shangwe; na badalayake tunasherehekea mwaka wa Kikristo. Hii imetokana na utawala wa Kikoloni.
Wakoloni, ingawa walipoingia sehemu za pwani na ile miji iliyokuwa na wakaazi wa Kiislamu waliwakuta wenyeji tayari wana kalenda yao; wanaweka hesabu ya tarehe za siku kwa kutundika vipande vya vijiti misikitini kwa kutumia mwezi mwandamo, walifanya mbinu Waislamu waudharau utamaduni wao huo; ili wafuate utamaduni waliokuja nao wao.
Kwa vile wakoloni hao walikuwa ni Wakristo, basi mbali ya kutawala walijaribu, kila njia kuwarubuni wenyeji waache dini na mila zao ili wafuate dini na mila za Kikristo. Na ndiyo kwa njia hiyo hiyo wakafaulu kuwafanya Waislamu waache kutumia kalenda yao ya Kiislamu na kuifuata kalenda ya Kikristo. Baadhi ya mbinu walizoitumia ni kuipa umuhimu wa pekee kalenda ya Kikristo, kama vile kuifanya miezi ya Januari, Februari n.k. ndiyo miezi ya kulipia mishahara.
Lakini hivi sasa tumekwisha jikomboa, ukoloni haupo tena. Kwa nini basi hatuoni fahari ya kuusherehekea mwaka wa Kiislamu? Mbali ya kalenda za Kiislamu kuning'inizwa juu ya kuta za misikiti Mwislamu gani, anayeitumia kalenda hiyo katika mawasiliano yake na Waislamu wenziwe, au katika mikataba na kumbukumbu nyingine?
Hata hivyo, tukio hili la kuanzishwa kwa mwaka au kalenda ya Kiislamu, lina mazingatio muhimu kwetu. Kwanza, kitendo cha Sayyidna Umar ibn Al-Khattab (r.a.) cha kushauriana na masahaba wenziwe juu kuanzisha kalenda hiyo linatuonyesha vipi uongozi wa Kiislamu unavyotaka uwe. Ni wajibu wa kiongozi ye yote wa Kiislamui awashauri wale anaowaongoza juu ya yale anayokusudia kuyatenda. Mwenyezi Mungu (s.a.w) alimwambia Mtume Muhammad (s.a.w.), "... na ushauriane nao katika mambo." (Al Imran 3:159).
Ikiwa Mtume (s.a.w.) anatakiwa awashauri masahaba wake, vipi kiongozi wa Kiislamu
anayetakiwa afuate mwendo wa Mtume (s.a.w.) akatae kuwashauri hao anaowaongoza? Na kumbe mojawapo wa sifa kubwa ya Waislamu ni kushauriana wao kwa wao. Mwenyezi Mungu (s.w.) anasema, "... na wanashauriana katika mambo yao" (Ash.Shuura 42:38).
Laiti Waislamu tungalifuata mwongozo huo wa Kur'ani Tukufu wa kushauriana juu ya mamboyetu, bila ya shaka yo yote tungalifanikiwa. Lakini wapi. Jambo la kushauriana limekuwa geni miongoni mwa Waislamu na matokeo yake ni kuvurugika kwa mipango yetu yote.
Jambo la pili ni kwamba Hijra inatukumbusha vipi Mtume (s.a.w.) pamoja na wafuasi wake wachache na wanyonge walivyoonewa walivyodhulumiwa walivyoteswa, na walivyonyanyaswa, na wakafiri wa Makka, na hatimaye wakapanga kumwua Mtume (s.a.w.) ili waizime nuru ya Uislamu. Lakini vitimbi vyao hivyo vikashindwa na Mwenyezi Mungu akamnusuru Mtume wake kwa kumpa amri ya kuhama mji wa Makka na kukimbilia Madina.
Katika kuitaja nusura hiyo aliyompa Mtume wake, Mwenyezi Mungu (s.w.) anasema, "Kama hamtamnusuru (Mtume), basi Mwenyezi Mungu alimnusuru walipomtoa wale waliokufuru; alipokuwa (mmoja tu na mwenziwe) wa pili wake, (peke yao); walipokuwa wote wawili katika pango; (Mtume) alipomwambia sahibu yake: "Usihuzunike, kwa yakini Mwenyezi Mungu yu pamoja nasi.' Mwenyezi Mungu akamteremshia utulivu wake, na akamnusuru kwa majeshi msiyoyaona, na akafanya neno la wale waliokufuru kuwa chini; na neno la Mwenyezi Mungu ndilo la juu. Na Mwenyezi Mungu ndiye anayeshinda na ndiye Mwenye hekima." (At-Tawba 9:40).
Mazingatio makubwa yanayotokana na aya hiyo ni kuwa wale wote wanaosimama kidete kutaka kuusimamisha Uislamu watapigwa vita. Kuna watakaoonewa, watakaodhalilishwa, watakaodhulumiwa, watakaowekwa korokoroni na hata kuuawa; lakini kama ilivyokuwa kwa Mtume (s.a.w.) na masahaba wake, hatimaye ni nusura kutoka kwa Mwenyezi Mungu (s.w,) na kusimama kwa Uislamu.
Mwenyezi Mungu (s.w.) anasema, "Jee! Wanadhani watu wataachwa kwa kuwa wanasema: 'Tumeamini', nao wasijaribiwe?"
"Hakika tuliwajaribu waliokuwa kabla yao, na kwa yakini Mwenyezi Mungu atawatambulisha walio wakweli na atawatambulisha walio waongo." (Al-Ankabut 29:2-3).
Ni muhimu sana, katika wakati huu, Waislamu kuwa na umoja na mshikamano, na kushauriana juu ya mambo yetu. Kama Mtume (s.a.w.) alihama Makka kwenda Madina ndiyo aka;pata nusura ya Allah (s.w.); basi na sisi tuyahame yale maovu yote tuliyoyatenda huko nyuma, yakatusababishia tuwemo katika hali hii duni tuliyonayo hivi sasa.
Tusisahau kauli ya Mtume (s.a.w.), "Muumini haumwi mara mbili katika shimo moja!".
|
|