Kusema ukweli hali imekuwa mbaya mno kiasi kwamba inatia kinyaa! Majarida ya burudani yanayoitwa 'SPICE; kutoka nchi jirani yamechupa mno mipaka. Hutuwezi kukaa kimya kwa sababu inatishia; si, tu maadili yetu bali hata usalama wetu kama jamii.
Majarida haya katika matoleo yake ya nyuma, takriban, manne, yaliyoingizwa nchini yamepambwa na mrembo (cover girl) wa kiafrika aliye uchi kabisa! Ma a,elaa latola ,lap wa akani imapweza. Na amekaa mkao wa ajabu unaoweza kumtia wazimu mwanamume yeyote. Kilichoandikwa humo ndani ni uchafu mtupu! Kwa kuchunga maadili ya taaluma ya waandishi na taadhima ya gazeti hili, siwezi kuthubutu kueleza kilichomo ndani.
Kinachoumiza zaidi ni kwamba majarida yametapakaa mno na yanaweza kusomwa hata na watoto wa shule. Vipi mawakala wa majarida machafu kama hayo wanapewa vibali vya kuyaingiza nchini kwa wingi namna hii? Kuna manufaa gani tunayopata?
Mwanamke mnene, aliyeumbwa kiafrika kuwekwa wazi na mapambo yake ya siri katika jalada na kurasa za jarida la 'SPICE' Kunatia uchungu sana! Watanzania hatujaporomokewa na maadili kwa kiwango hiki. Kwanini serikali inaruhusu aibu hii kuwa jambo la kawaida?
Majanga mengi yanayoikumba jamii yetu yanatokana na kupuuzia mambo machafu yaliyopewa majina ya kupendeza. Leo wazinifu wanaitwa 'Wapenzi', ulevi unaitwa 'urithi wetu', kutembea uchui jukwaani Miss Tanzania', na zinaa imepewa jina la 'tendo la ndoa'. Kama tendo la ndoa; basi tuwaachie wenye ndoa - hawataki! Mtu ndoa hana lakini anang'ang'ania tendo la ndoa! Maajabu haya!
Wataalamu wa sayansi jamii, wanasheria, polisi, wanasiasa, na hata serikali kupitia wizara yake ya maendeleo ya jamii wanawake na watoto wanakiri kwamba tatizo la ubakaji na uhalifu mwingine wa ngono ulioikumba jamii yetu ni matokeo ya mmomonyoko wa maadili.
Tulidhani Serikali ingeweka nguvu za ziada katika kujenga upya na kulinda maadili yetu. Tunapoona majarida ya kihuni kama 'SPICE' yametapakaa mitaani kwa kweli tunakata tamaa kabisa! Kumbe Serikali inatumia nguvu nyingi kupambana na matokeo ya tatizo na kukwepa tatizo lenyewe.
Mbali na kumdhalilisha mwanamke wa kiafrika majarida kama haya ni kichocheo kikubwa cha zinaa na majanga yatokanayo na zinaa. Ni mwaka mmoja sasa umepita tangu sheria ya ubakaji ipitishwe na Bungue hapo Aprili 4, mwaka jana. Sheria hii imebeba adhabu kali inayoweza kumtia hofu hata mhaini wachilia mbali mbakaji. Lakini cha ajabu imeshindwa kabisa hata kupunguza kasi ya vitendo vya ubakaji usiseme kuviondoa kabisa. Kinyume chake vitendo hivi vimeongezeka kwa kasi kubwa zaidi kuliko ilivyokuwa mwanzo. Tatizo liko wapi? Maadili! Maadili! ... Maadili!
Haiwezekani kulishinda tatizo hili bila ya kujenga na kulinda maadili mema katika jamii. Sheria kali na matumizi ya vyombo vya dola peke yake havitafua dafu. Maadili mema utayajengaje iwapo majarida ya hovyo kama 'SPICE' yanaruhusiwa kuuzwa 'kuilaini' tu nchini.
Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoongoza katika Afrika kwa kasi ya kuenea kwa ugonjwa hatari wa ukimwi. Serikali imeendesha kampeni ya gharama kubwa ya kupambana na ukimwi. Kondomu zimetawanywa mpaka kwa wanafunzi, mabago ya tahadhari yamebandikwa kila pembe, 'T.shirts' na 'Capes' za ukimwi zimesambazwa nchi nzima. Lakini ukimwi bado uko pale pale.
Ni vipi ukimwi unaweza kutokomezwa wakati maadili yanazidi kubomolewa? Vijana wanashawishiwa kupenda uasherati na majarida ya kipuuzi na sisi hatujali. Ukimwi hauwezi kudhibitiwa kwa kutumia F.F.U.! Ni maadili mema peke yake.
Tuzingatie ukweli wa kimaumbile kwamba vijana wanapofikia baleghe miili yao inapitia mabadiliko makubwa ya kimaumbile na kibailojia. Mabadiliko haya yanaambatana na hamu kubwa ya kukutana na mwenzi wa jinsia tofauti. Vijana hawa wanapokutana na majarida ya jamii ya 'SPICE' ni vigumu sana kuwajenga kimaadili. Hawawezi kuyachukia mambo maovu kwa sababu jamii wanayoishi inayakumbatia. Matokeo yake ubakaji unazidi kushamiri, ukimwi unaongezeka, na majanga kama hayo.
Nadhani wakati umefika wa kupambana kwa dhati kabisa na vitendo vya ubakaji; na gonjwa la ukimwi; kwa kupambana na mmomonyoko wa maadili katika jamii yetu. Kila kinachotishia maadili yetu tukione ni adui mkubwa kuliko ukimwi au wabakaji.
Serikali lazima iwe na sera madhubuti ya kuchunguza majarida yote ya ndani na nje yanayouzwa nchini. Yale yanayochapisha uchafu yadhibitiwe mara moja! Hatuhitaji burudani zinazotufanya tufanane na wanyama. Nashangaa serikali imetangaza kuyafungia magazeti na majarida yaliyokwishakufa na kuyaacha yanayoangamiza maadili yetu. Kama kuna magazeti ya kufungia basi ni haya!
|
|