Uchambuzi/hoja binafsi
 
Je, Yehova na Allah ni miungu tofauti ? - 4
 
   

Na Muhibu Said

Kama tulivyoona katika matoleo yaliyopita, endelea kufuatana nami sehemu ya nne ya mada hii, uzidi kuona kwa uwazi zaidi kwamba Mungu yule aliyejifunua kwa Nabii wake wa mwisho, Mtume Muhammad (s.a.w.) kwa jina lake kuu la Allah, ndiye Mungu yule yule aliyejitambulisha kwa mara ya kwanza kwa Nabii Musa (a.s.) kwa jina la Yehova; na ndiye Mungu wa Nabii Ibrahimu, Ismail, Isaka, Yakobo na Mitume na Manabii wake (Mungu) wengine wote aliojitambulisha au kujifunua kwao (a.s.) kwa majina tofauti. Na pia upate kuona kama kweli Yehova ndiye Mungu wa Wakristo na amezaa mtoto?

Kutokuwa na nafsi zaidi ya moja

Kwa kuzingatia kuwa yeye ni Mmoja tu katika Uungu wake, ni dhahiri kuwa sifa kuu ya nane ya Mungu wa kweli ni kuwa Yeye ni Nafsi moja tu wa pekee asiyekuwa na mshirika na yeyote wala na chochote katika Uungu wake, sifa zake na katika kila hali yake kwa ujumla. Kwa mantiki hiyo basi, ni wazi kuwa sifa hii nayo pia ni kigezo kingine muhimu kinachoweza kuwa hoja ya msingi ya kutofautisha Allah na Yehova iwapo tu itabainika mmoja wao hana sifa hiyo. Hata hivyo, tusomapo maandiko ya Qur'ani Tukufu na Biblia Takatifu tunaona vyote vinamuelezea Mwenyezi Mungu yule yule Mmoja aliyejifunua au kujitambulisha kwa Manabii wake mbali mbali kwa majina tofauti akionyesha kuwa yeye ni Nafsi moja tu. Ukweli huu tunaupata katika maandiko yafuatayo ya Qur'ani Tukufu na Biblia Takatifu:

Biblia:

"Hubirini, toeni habari; naam, nawafanye mashauri pamoja; ni nani aliyeonyesha haya tangu zamani za kale? Ni nani aliyeyahubiri hapo zamani? Si mimi, BWANA? wala hapana Mungu zaidi ya mimi; Mungu mwenye haki, mwokozi; hapana mwingine zaidi ya mimi. Niangalieni mimi, mkaokolewe, enyi ncha zote za dunia; maana mimi ni Mungu; hapana mwingine. Kwa nafsi yangu nimeapa, neno hili limetoka kinywani mwangu katika haki, wala halitarudi, ya kwamba mbele zangu kila goti litapigwa, kila ulimi utaapa". (Isaya 45:21-23).

"Lakini kama hamtaki kusikia maneno haya, mimi naapa kwa nafsi yangu, asema BWANA, ya kuwa nyumba hii itakuwa ukiwa". (Yeremia 22:5).

"Kwa ajili ya nafsi yangu, kwa ajili ya nafsi yangu, nitatenda haya; Je! litiwe unajisi jina langu? wala sitampa mwingine utukufu wangu". (Isaya 48:11).

Qur'ani:

"Na (kumbukeni) Allah (Mwenyezi Mungu) atakaposema: Ewe Isa bin Maryam! Je, wewe uliwaambia watu: Nifanyeni mimi na mama yangu kuwa waungu badala ya Mwenyezi Mungu? Aseme (Nabii Isa): Wewe umetakasika na kuwa na mshirika. Hainijuzii mimi kusema ambayo si haki yangu (kuyasema, kwa kuwa ni ya uongo). Kama ningalisema bila shaka ungalijua; unayajua yaliyomo nafsini mwangu, lakini mimi siyajui yaliyo nafsini mwako; hakika wewe ndiye ujuaye mambo ya ghaibu." (Qur'an, 5:116).

"Na Mungu wenu ni Mungu mmoja tu, hakuna anayestahiki kuabduiwa ila Yeye ambaye ni Mwenye kuneemesha neema kubwa kubwa na Mwenye kuneemesha neema ndogo ndogo; (zote mneemeshaji ni Yeye. (Qur'ani, 2:163).

Kulingana na shuhuda hizo juu, tunaona wazi kuwa Qur'ani Tukufu na Biblia Takatifu vyote kwa pamoja vinafundisha kuwa Mwenyezi Mungu yule yule mmoja aliyejifunua kwa manabii wake mbali mbali kwa majina tofauti anajinadi kwa nafsi moja tu. kwa shuhuda hizo, ni wazi kuwa sifa hii nayo inadhihirisha kuwa Allah na Yehova ni Mwenyezi Mungu yule yule mmoja asiyekuwa na mshirika katika Uungu wake, Muumba wa kila kitu.

Kutobadilika - Badilika

Kwa kuzingatia udhaifu mkubwa wa sifa ya kubadilika-badilika inayowakabili viumbe vyake vyote katika kila hali, ni dhahiri kuwa sifa kuu nyingine ya Mungu wa kweli ni lazima iwe ni kutobadilika badilika hasa ukizingatia pia yeye (Mungu) hafanani na yeyote wala na chochote katika viumbe wake katika kila hali. Kwa mantiki hiyo basi, ni wazi kuwa sifa hii nayo pia ni kigezo kingine muhimu kinachoweza kuwa hoja ya msingi ya kutofautisha Allah na Yehova iwapo tu itabainika mmoja wao hana sifa hiyo. Hata hivyo, tusomapo maandiko ya Qur'ani Tukufu na Biblia Takatifu tunaona vitabu vyote hivyo vinafundisha kwamba mwenye sifa hiyo ni Mwenyezi Mungu yule yule mmoja aliyejitambulisha kwa Manabii wake mbali mbali hadi kwa Nabii wake wa mwisho, Mtume Muhammad (s.a.w.) kwa majina tofauti. Maandiko yafuatayo ya Qur'ani Tukufu na Biblia Takatifu yanathibtisha ukweli huu:

Biblia:

"Nitasema, Ee Mungu wangu, usiniondoe katikati ya siku zangu; Miaka yako ni tangu kizazi hata kizazi. Hapo mwanzo uliutia msingi wa nchi, Na mbingu ni kazi ya mikono yako. Hizi zitaharibika, bali Wewe utadumu; Naam, hizi zitachakaa kama nguo; na kama mavazi utazibadilisha, Nazo zitabadilika. Lakini Wewe U Yeye yule; Na miaka yako haitokoma". (Zaburi 102:24-27).

"Kwa kuwa mimi, BWANA, sina kiguegueu' ndio maana ninyi hamkuangamizwa, enyi wana wa Yakobo". (MALAKI 3:6).

"Kila kutoa kuliko kwema, na kila kitolewacho kilicho kamili, hutoka juu, hushuka kwa Baba wa mianga; kwake hakuna kubadilika, wala kivuli cha kugeuka-geuka". (Yakobo 1:17).

Qur'an:

"Hii ni kawaida ya Allah (Mwenyezi Mungu) iliyokuwa kwa wale waliopita zamani; wala hutapata mabadiliko katika kawaida ya Allah (Mwenyezi Mungu)" (Qur'ani 33:62).

"Ndiyo desturi ya wale tuliowatuma (tuliowapa Utume) kabla yako katika Mitume wetu. Wala hutapata mabadiliko katika desturi Yetu". (Qur'ani, 17:77).

"Hiyo ndiyo kawaida ya Allah (Mwenyezi Mungu) iliyotangulia zamani; wala hutapata mabadiliko katika kawaida ya Allah (Mwenyezi Mungu): (Qur'ani, 48:23).

Kulingana na shuhuda hizo juu, tunaona Qur'an Tukufu na Biblia Takatifu vyote kwa pamoja vinamuelezea Mwenyezi Mungu yule yule mmoja aliyejifuma kwa Manabii wake mbali mbali kwa majina tofauti kwamba si desturi yake (hana sifa ya) ya kubadlika-badilika. Kwa shuhuda hizo basi, ni wazi kuwa sifa hii nayo pia inadhihirisha kuwa Yehova na Allah ni Mweyezi Mungu yule yule mmoja aliyejitambulisha kwa Manabii wake mbali mbali hadi Nabii wake wa mwisho, Mtume Muhammad (s.a.w.) kwa majina tofauti.

Kutokuchoka

Kwa kuzingatia udhaifu mkubwa uliomo katika sifa dhaifu ya kuchoka ambayo pia inawakabili viumbe vyake na kwa kuzingatia kuwa yeye hana mfano wa yeyote wala na chochote katika kila hali, ni wazi kuwa siifa kuu nyingine ya Mungu wa kweli ni kutokuchoka (Yaani Mwenyezi Mungu daima ameepukana mbali na sifa ya kuchoka). Kwa mantiki hiyo basi, ni wazi kuwa sifa hii nayo pia ni kigezo kingine muhimu kinachoweza kuwa hoja ya msingi ya kutofautisha Allah na Yehova iwapo tu itabainika 'mmoja wao' hana sifa hiyo. Hata hivyo, tusomapo maandiko ya Qur'ani Tukufu na Biblia takatifu tunaona vyote kwa pamoja vimuelezea Mweyezi Mungu yule yule mmoja aliyejitambulisha kwa Manabii wake mbali mbali kwa majina tofauti kwamba ndiye mwenye sifa hiyo. Uthibtisho wa hilo tunaupata katika maandikio yafuatayo ya Qur'ani Tukufu na Biblia Takatifu:

Biblia:

"Je! wewe hukujua? hukuskia? Yeye Mungu wa milele, Bwana Muumba miisho ya dunia, hazimii, wala hachoki; akili zake hazichunguziki". (Isaya 40:28).

"Na tumeziumba mbingu na ardhi na vilivyomo kati yao katika nyakati sita, wala hayakutugusa machofu" (Qur;an 50:38).

Kulingana na shuhuda hizo juu, tunaona wazi kuwa Qur'ani Tukufu na Biblia Takatifu vyote kwa pamoja vinafundisha kuwa Mwenyezi Mungu yule yule mmoja aliyejifunua kwa Manabii wake mbali mbali kwa majina tofauti ndiye pekee asiyekuwa na sifa hiyo dhaifu ya kuchoka. Kwa shuhuda hizo, ni wazi kuwa sifa hii nayo pia inadhihirisha kuwa Allah na Yehova ni Mwenyezi Mungu yule yule mmoja, Muumbaji wa kila kinachoonekana na kisichoonekana, mwenye sifa kamilifu.

Kutokufa (Yu Daima)

Kwa kuzingatia kuwa yeye hafanani na kiumbe wake yeyote wala chochote katika kila hali, ni dhahiri kuwa sifa kuu nyingine ya msingi ya Mungu wa kweli ni lazima iwe kutokufa, hasa kwa kuzingatia kuwa yeye pekee yake ndiye anayetegemewa na viumbe wake wote kwa kila haja, kwa vile yeye peke yake ndiye Mwendeshaji wa mambo yote katika kila sekunde.

Hakuna yeyote wala chochote kinachoweza kuendesha ulimwengu na kukidhi haja zote za viumbe wote katika muda wote ambao Mungu angekufa. Kwa mantiki hiyo basi, ni wazi kuwa sifa hii nayo pia ni kigezo muhimu na cha msingi kimachoweza, kuwa hoja ya msingi ya kutofautisha Allah na Yehova iwapo tu itabainika 'mmoja wao' hana sifa hiyo. Hata hivyo, tusomapo maandiko ya Qur'ani Tukufu na Biblia Takatifu tunaona vyote vinafundisha kwamba mwenye sifa hiyo (ya kutokufa) ni Mwenyezi Mungu peke yake aliyejifunua au kujitambulisha kwa Manabii wake mbali mbali kwa majina tofauti. Maandiko yafuatayo ya Qur'ani Tukufu na Biblia Takatifu yanathibitisha ukweli huu:

Biblia:

"Nitasema, Ee Mungu wangu, usiniondoe katikati ya siku zangu; Miaka yako nitangu kizazi hata kizazi. hapo mwanzo uliutia msingi wa nchi, Na mbingu ni kazi ya mikono yako. Hizi zitaharibika, bali Wewe utadumu; Naam, hizi zitachakaa kama nguo; Na kama mavazi utazibadilisha, Nazo zitabadilika. Lakini Wewe U yeye yule; Na miaka yako haitakoma". (Zaburi 102:24-27).

"Mungu akamwambia Musa, MIMI NIKO AMBAYE NIKO; akasema ndivyo utakavyowaambia wana wa Isreili; MIMI NIKO amenituma kwenu" (Kutoka 3:14).

"Ambaye yeye peke yake hapatikani na mauti, amekaa katika nuru isiyoweza kukaribiwa; wala hakuna mwanadamu aliyemwona, wala awezaye kumwona. Heshima na uweza una yeye hata milele. Amina". (1 Timotheo 6:16).

Qur'an:

"Wala usimuombe - pamoja na Allah (Mwenyezi Mungu) - Mungu mwingine; hakuna aabudiwaye kwa haki ila Yeye; kila kitu kitakufa isipokuwa yeye (Mwenyezi Mungu basi). Hukumu (Yahova mambo yote) iko kwake, na kwake mtarejezwa (nyote)". (Qur'ani 28:88).

Aidha, kwa sifa yake ya kutokuonekana ni wazi kuwa hakuna yeyote wala chochote (na chenye uwezo wa) kumwua.

"Allah (Mwenyezi Mungu) hakuna Mola ila yeye, (na) ndiye mwenye uhai wa maisha, Msimamia kila jambo..." (Qur'an, 2:255).

Kulingana na shuhdua hizo juu, tunaona wazi kuwa Qur'an Tukufu na Biblia Takatifu vyote kwa pamoja vinafundisha kwamba Mwenyezi Mungu yule yule mmoja aliyejifunua au kujitambulisha kwa Manabii wake mbali mbali kwa majina tofauti ndiye peke yake mwenye uhai wa milele (yu daima) - hafi-na kwa ujumla yeye peke yake ndiye mwenye sifa ya kutokufa. Kwa shuhuda hizo, ni wazi kuwa sifa hii nayo pia inadhihirisha wazi kuwa Allah anayefundishwa na Qur'ani Tukufu ndiye Yehova anayefundishwa na Biblia Takatifu kwa majina tofauti.

Ukweli huu tunaupata katika Qur'an, Torati, Zaburi, Injili na sio kwenye Hadithi dhaifu zinazopingana na vitabu hvyo anazosingiziwa ati kasema Mtume Muhammad (s.a.w.)

Itaendelea toleo lijalo.
 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook