Sheikh wa Mkoa Kigoma asema
Waislamu hawatavumilia dhulma

Na Ibrahimu Bakari

SHEIKH wa Mkoa wa Kigoma Alhaj Taufiq Ibrahim amesema Waislamu hawawezi kuendelea kuvumilia dhulma wanazofanyiwa na serikali.

Sheikh Taufiq alisema iweje serikali iwadhulumu Waislamu ilhali inafahamu kuwa wamefanya mengi kuleta uhuru wa nchi hii.

Sheikh Taufiq aliyasema hayo hivi karibuni katika moja ya hotuba zake kwa Waislamu wa Kigoma kufuatia hali inayodhaniwa kuwa ni ya madhila dhidi ya Waislamu hapa nchini.

Sheikh huyo amesema Waislamu wameuliwa kwa makusudi wakakaa kimya badala yake wameomba Tume huru iundwe kuchunguza kadhia hiyo hata hivyo amesema inavyoelekea jambo hilo limeshindikana.

Naye Sheikh Abas Idd Imamu Mkuu wa Msikiti wa Ijumaa Mwanga Legeza Mwendo, amewataka Waislamu kuendesha harakati za kujikomboa kwa mara nyingine bila ya kuogopa lawama za yeyote.

Sheikh Abas aliyasema hayo baada ya swala ya Ijumaa kufuatia propaganda zilizoenezwa mjini Kigoma kuwa sherehe za mwaka mpya wa Kiislamu zilikuwa na mrengo wa kisiasa ambapo zililenga zaidi kuihujumu CCM.

Sheikh huyo alifafanua kuwa walichokifanya Waislamu ni kueleza yale waliyotendewa na CCM.

"Waislamu wameuawa, akina mama wacha Mungu wamevuliwa nguo lakini mpaka leo CCM haijaomba radhi", alisema Imamu huyo maarufu mjini Mwanga.

Wakati huo huo, fukuto la maandamano mengine linaendelea kutanda mkoani Kigoma ambapo imeelezwa kuwa yamekusudiwa kuishia katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo.

Maandamano hayo yatafanyika kupinga madai ya serikali ya mkoa wa Dar es Salam kumsaka Katibu wa Kamati ya Kutetea haki za Waislamu Sheikh Ponda Issa Ponda.

Imeelezwa kuwa kufuatia joto hilo, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Bw. Ditopile akitoa nasaha katika mazishi ya mtu mmoja maarufu mkoani humo alisema kwamba haitakuwa vyema maandamano hayo yaishie kwake, kwa sababu wahusika wa suala hilo ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Makamba na Kamanda wake wa polisi Bw. Alfred Gewe.

Hata hivyo, Waislamu waliokuwepo katika msiba huo walisema kuishia kwake maandamano hayo hakuna maana ya kumuhusisha bali kwa kuwa yeye ni mwakilishi wa Rais mkoani humo wangependa kufikisha salaamu zao kupitia kwake.

Maandamano hayo yatatanguliwa na funga (swaumu) ya siku tatu na futari ya pamoja ambapo wale wa Mwanga watafuturu Msikiti wa Ijumaa Legeza Mwendo na wale wa Ujiji watafuturu Misikiti ya Buzebazeba na Muumin.


Wachangia Ujenzi wa Msikiti Babati
 

Na Mwandishi wetu, Babati

Waislamu wilayani Babati wakiongozwa na Mbunge wa babati Mashariki Bw. Omari Shabani Kwaang' hivi karibuni wameukabidhi uongozi wa msikiti mkuu wa Ijumaa wilayani hapa vifaa vya ujenzi wa Msikiti huo vyenye thamani ya Tshs, 640,000/- pamoja na fedha taslim shs. 160,000/-.

Akipokea michango hiyo kwa niaba ya Sheikh wa Wilaya hii, Sheikh Hashim Lema alisema michango yote iliyotolewa na waumini hao itasaidia ujenzi wa msikiti huo unaotarajiwa kukamilika hivi karibuni.

Alisema kuwa msikiti huo ambao upo katika hatua za mwisho katika ujenzi wake utakuwa na uwezo wa kuchukua waumini wapatao 400 na kugharimu zaidi ya shs. milioni 3 hadi utakapokamilika.

Pia Sheikh Hashim Aliwashukuru wote walionyesha moyo huo wa kujitolea mali na nguvu zao na kuwataka waumini wengine wafuate nyayo hizo ili kuwezesha kukamilika kwa msikiti huo.

Aidha aliwataka waumini kujiepusha na dhana mbaya ya migogoro ambayo ndiyo chanzo kikuu cha kudumaza maendeleo ya Waislamu.

Naye Mbunge Bw. Omari katika risala yake kwa waumini hao aliwataka kuwa na mshikamano wa dhati ili kulinda Dini hiyo na kuacha malumbano yasiyoisaidia Dini na Waislamu kwa jumla.

Katika kuchangia Msikiti huo Mbuge huyo alitoa Bati 50 wakati Bati 100 zilitolewa na Bw. Iddi Omari (Maziwa) na Mzee Juma Ibuva alitoa mifuko 10 ya saruji.


Wanafunzi Waislamu wanyanyaswa Mkwawa
 

Na Mwandishi Wetu

TAARIFA ya TAMPRO tawi la Iringa imedai kwamba inaelekea uongozi wa shule ya Sekondari Mkwawa haifurahishwi kuwepo kwa wanafunzi Waislamu shuleni hapo.

Wanafunzi Waislamu ambao ni wachache sana shuleni hapo imedaiwa kwamba wamekuwa wakikerwa na kunyanyaswa na uongozi wa shule kwa tuhuma kwamba wanataka kuiharibu shule kwa Uislamu wao.

Imeelezwa kwamba wanachodai wanafunzi hao ni uhuru wao wa kuswali, kuvaa Hijab na majukumu mengine ya dini yao wakiwa shuleni.

Taarifa ya TAMPRO iliyotolewa hivi karibuni imeeleza kwamba hivi sasa zipo juhudi za kulipiga marufuku vazi la Hijab ambapo kwa kushinikizwa na uongozi wa shule Kamati ya Wanafunzi ikiwa takriban ya Wakristo watupu imepiga kura kupitisha azimio la kumwandikia Mkuu wa Shule barua kumtaka apige marufuku vazi la Hijab shuleni hapo.

Kwa mujibu wa maelezo ya Naibu Katibu wa TAMPRO hivi karibuni wanafunzi Waislamu walikatazwa kuwashirikisha wanafunzi wa mashule mengine katika sherehe zao za kuwaaga wanafunzi wa kidato cha sita.

Mwalimu Mkuu alizuia sherehe hizo wakati akiruhusu shuleni hapo kufanyika kile kinachoitwa Joint Mass ya wanafunzi wa mashule yote ya mjini Iringa ikijumuisha Ifunda na Tosamaganga.

Mwalimu Mkuu huyo alidai kwamba asingeruhusu Waislamu wakutane hapo kwani watahatarisha amani.

Taarifa zaidi zimeeleza kwamba Mwenyekiti wa Bodi ya shule huenda akalazimishwa kujiuzulu kwa madai ya kuwa upande wa Waislamu wanaodaiwa kuleta udini Mkwawa.

Wakati huo huo, kumekuwa na tabia ya vijana wasiokuwa Waislamu kuwanyanyasa vijana wa Kiislamu katika shule ya Tosamaganga ambayo ina jumla ya wanafunzi wote takriban mia nane na hamsini (850). Vijana wa Kiislamu wakiwa 85 tu (asilimia 10%).

Kutokana na mazingira kama hayo kumezungukwa na watu wengi wasio Waislamu, ufugaji wa nguruwe umewekewa kipaumbele. Hata wafanyakazi walio wengi wamefuga nguruwe pamoja na shule yenyewe.

Nguruwe hawa wanapoliwa iwe ni nyumbani kwa mwalimu, mfanyakazi asiye mwalimu au shuleni, wanafunzi ndio wateja wakuu na ni wanunuzi wazuri.

Vijana hao wasio Waislamu huchukua nyama hiyo na kuingia nayo bwenini (Dining Hall) kitu ambacho kinawafanya vijana wa Kiislamu kuishi kwa shida.

Si hivyo tu, bali hata vyombo ambavyo hutumika huko wanapokula nyama hiyo huja navyo mabwenini na hatimaye vinaingia mesini bila kusafishwa kwa utaratibu unaotakiwa.

Zaidi wanafunzi wasio Waislamu wanachemsha mafuta hayo na wanachanganya na Blue Band pamoja na mafuta ya alizeti halafu wanaingia nayo mesini, hii imetokea baada ya kutangazwa mara kadhaa kuwa hairuhusiwi kuingia na nyama ya nguruwe au mafuta mesini.

Vijana hawa wanapoulizwa hutoa maelezo kuwa hayo ni mafuta ya kawaida, Blue Band au alizeti.

Serikali imeombwa itazame suala hili kiundani na hatimaye kuweka sheria ambayo italinda uhuru wa imani kwa wanafunzi wote.

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook