Serikali yashutumiwa kwa uvunjaji wa amani
  Na Mwandishi Wetu

SERIKALI imeshutumiwa kuvuruga amani kwa vyombo vyake vya dola kuingilia masuala ya dini kinyume na Katiba na sheri za nchi.

Bw. Ndimbo ambaye ni Mkatoliki amemwambia Mkuu wa Wilaya ya Temeke kuwa serikali na vyombo vyake vinastahiki kubeba lawama zote za kuvunjika kwa amani nchini kwa vyombo vyake kuhusika kuanzisha vurugu katika mihadhara ya dini. 

Bw. Ndimbo wa kikundi cha mihadhara cha Kikristo alitoa shutuma hizo hivi karibuni wakati akichangia mapendekezo kadhaa ya serikali kuhusu

mihadhara ya dini katika mkutano baina ya mkuu wa Wilaya ya Temeke, kapteni John Chiligati na viongozi wa misikiti na makanisa wa Wilaya hiyo.

Mkutano huo ulifanyika ofisini kwa mkuu huyo wa wilaya kwa zaidi ya masaa matatu, Jumamosi ya Aprili 24, mwaka huu.

Alisema tabia ya serikali kung'ang'ania kukuza kashfa za kidini zisizokuwepo ni katika jumla ya sababu ambazo serikali imekuwa ikizitumia kuhalalisha vurugu hizo inapotaka kuwahujumu wahubiri wa dini na kuvuruga shughuli zao.

Aliongeza kuwa anashangaa kuona serikali imekuwa mstari wa mbele kushabikia kashfa hizo wakati wahusika wenyewe wa mihadhara hiyo hawana habari nazo wala ugomvi wowote.

"Sisi na Waislamu tuna ushairikiano mzuri tu katika mihadhara yetu, na hata baada ya kuhubiri tunaombana nauli, tunatembeleana na kukaribishana katika maofisi yetu vizuri tu", alisema Bw. Ndimbo.

Kwa hali hiyo, aliitaka serikali ieleze bayana mafunzo inayotoa sasa kwa polisi wake huko Moshi kama ni kukamata wahubiri wa dini badala ya vibaka na wezi.

Shutuma hizo za kiongozi huyo wa kikristo zimefuatia madai ya serikali yaliyotolewa na mkuu huyo wa wilaya katika mkutano huo kwamba serikali inazo habari za kuwepo katika mihadhara ya dini mahubiri ya kashfa yenye lengo la kuchukiza dini nyingine na kwamba kuna baadhi ya nyumba za ibada zinatumiwa kuhubiri mambo ya siasa jambo ambalo alidai linachochea chuki miongoni mwa waumini wa nyumba hizo wenye vyama tofauti vya kisiasa.

Mkuu huyo wa wilaya alidai kuwa serikali daima haifurahi kumkamata kiongozi yoyote wa dini kwa sababu ya kuhubiri dini lakini akasisitiza kwamba kuna watu wachache wanaotumia mihadhara hiyo kukashfiu dini nyingine na kuhubiri siasa misikitini na makanisani.

Pamoja na hayo, alisema kuwa sababu za kiusalama, serikali wilayani kwake imeamua kuweka saa 12:00 jioni kuwa muda wa mwisho wa kuhubiri dini katika viwanja vya wazi vya umma na kwamba kwa kuwa viwanja hivyo ni vya wananchi wote, mahubiri hayo yafanyike kwa muda wa siku mbili tu.

Hata hivyo, viongozi hao kwa pamoja walipinga suala zima la kupangiwa na seriali muda wa siku ya kuhubiri dini kwa hoja kwamba serikali haina haki hiyo kwa kuwa haina dini na kwa hiyo iwaachie wana dini wenyewe wajipangie mambo yao.

Akichangia maoni yake katika mkutano huo, mhadhiri maarufu jijini, Ustadhi Hussein Ismail alimwambia mkuu huyo wa Wilaya kuwa tofauti na siasa, mahubiri ya dini yanavipengele vingi vinavyohitaji kupata siku na muda mwingi wa kutosha.

"Inatakiwa upatikane muda wa kujiandaa na muhadhara, muda wa kuwasilisha mada na muda wa kukaribisha na kujibu maswali ya waumini ambapo ni tofauti na ilivyo kwenye mikutano ya siasa ambayo mzungumzaji anaweza akasimama na kuanza kusema nitawajengezeeni Hospitali, nitawajengeeni barabara n.k. kisha akafunga mkutano wake akaondoka zake bila kutoa nafasi ya maswali." alisema ustadhi Husein.

Aidha, alitaka serikali kutochukulia utofauti wa imani za msingi zilizopo baina ya Uislamu na Ukristo kuwa ni kashfa na badala yake imchukulie kuwa ni mchokozi wa kidini mtu yeyote atakayebainika akitoa mahuburi nje ya vitabu vya Mwenyezi Mungu na ambayo si sehemu ya dini yake.

Ustadhi Hussein aliongeza kuwa tofauti na kutangaza sera za vyama vya siasa msikitini, lakini waumini watakapoamua kuelezana misikitini juu ya dhulma na uonevu wanaofanyiwa na serikali, isichukuliwe pia kuwa ni kuhubiri siasa msikitini.

Akitoa msimamo wa kanisa lake la Tanzania Assemblies of God katika mkutano huo, Mchungaji Mfinanga alisema kulingana na programu ya mahubiri ya kanisa lake, siku mbili hazitoshi kabisa kwa maandalizi wala hakidhi mahitaji ya neno la Mungu kwa waumini. Kwa hali hiyo, alisema muda muafaka wa kufanya mikutano yake ni zaidi ya wiki moja.

Naye Mkurugenzi wa Elimu na Mafunzo wa ALMALLID, Sheikh Yusuf Omari aliitaka serikali badala ya kujengea hali ya hofu mihadhara ya dini vipembeni, ni wajibu wake kuipa ulinzi kama inavyotoa katika shughuli nyingine na bila kuwawekea siku na muda maalum wa kuhubiri.

Pamoja na kuahidi kuyafikisha mapendekezo hayo ya viongozi wa dini katika kikao cha viongozi wa ulinzi wa uslama, mkuu huyo wa Wilaya alihitimisha maelezo yake kwa kusema milangoya ofisi yake; iwazi kwa yeyote mwenye madai dhidi ya utendaji mbaya serikali na kuongeza kuwa hapendi kumsikia yeyote katika Wilaya yake akilalamika na kunung'nunika pembeni kwamba anaonewa au kudhulumiwa na mamlaka yoyote ya serikali.

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook