Na Mwandishi Wetu
WAISLAMU mkoani Singida wameitaka serikali imkamate na kumfikisha mahakamani Paroko Camillus Lwambano kwa uchochezi wake uliopelekea watu kuuliwa.
Wakizungumza mjini Singida hivi karibuni baada ya mkanda wa mauaji ya Mwembechai kuonyeshwa, wazee maarufu mjini hapa na waumini kutoka Misikiti ya Salafi na Majengo wamesema kuwa Paroko Lwambano ndiye aliyepandikiza fitna iliyoichochea serikali kutumia vyombo vyake vya mabavu dhidi ya Waislamu hadi kuua.
Wamesema leo wapo wajane na watoto yatima wakiteseka; chimbuko la masaibu yao likiwa uchochezi wake.
Mkanda wa mauaji bado unaangaliwa kwa wasiwasi katika eneo la mji wa Singida hasa kwa tuhuma zilizozagaa kuwa kuuangalia mkanda kutapandikiza chuki kati ya Waislamu na serikali.
Mama mmoja ambaye ni maarufu katika shughuli za Tabligh Bi Kyamani alisema haoni sababu ya kuogopa kuangalia mauaji hayo kwani yalifanyika pale Mwembechai hayakuwa ya siri; na TV binafsi walionyesha kadhia hiyo ingawa kwa kukatisha katisha.
"Hakuna mwananchi yeyote ambaye hakuyaona mauaji ya Waislamu Mwembechai kupitia TV," alisema.
Aidha mama huyo alisema yeye binafsi aliyaona mauaji kupitia TV binafsi alipokuwa Dodoma katika shughuli zake binafsi. Hivyo aliwataka Waislamu waache hofu isiyo ya msingi.
|
|