Maoni yetu
 
Serikali imeitia doa nchi yetu
 
Yashindwa kuthamini maisha ya raia wake
 
TAARIFA za vyombo vya habari za hivi karibuni zimeeleza kukiri kuwepo kwa njaa Mahenge iliyoua watu wasiopungua arobaini na watano (45). Baadhi ya vyombo hivyo vya habari vilitoa hata orodha ya waliokufa.

Awali vyombo vya habari viliporipoti kutoweka kwa uhai wa baadhi ya watu kutokana na njaa, serikali ilipinga kwa nguvu zake zote. Haikuishia hapo bali

ikatoa maelezo kwamba hata kama wapo watu waliokufa basi wamekufa kwa kipindupindu.

Hayupo mtu mwenye akili zake timamu anayefurahia watu kufa kwa kipindupindu wala haipo serikali yoyote ya watu makini inayoona fahari kutangaza kwamba raia wake kwa makumi wanakufa kwa kipindupindu. Hapo ndipo inapotuwia vigumu kuielewa ile mantiki ya serikali ya wilaya ya Mahenge kujigamba kwamba hakuna mtu aliyekufa kwa njaa ila kwa kipindupindu. Hivi kufa kwa kipindupindu ni fahari!

Suala la msingi hapa ni uhai na maisha ya watu, sio sababu ya vifo. Kama vimetokana na ajali, kuchomewa nyumba, kipindupindu, uti wa mgongo, njaa au vinginevyo bado ni uhai wa watu umepotea na ni lazima ionekane kwamba ni tatizo zito na wahusika waonekane kujali.

Suala la Mahenge lilivyoshughulikiwa haionyeshi kwamba ipo hisia miongoni mwa viongozi wetu ya kujali uhai wa watu. Kwa sababu tahadhari ingechukuliwa mapema watu wasingekufa. Nchi haipo vitani wala haijatangaza njaa nchi nzima kama wakati wa unga wa njano na maduka ya kaya. Hatukuhitaji tuagize chakula nje ili tunusuru maisha ya watu 45. Chakula kilichopo ndani ya nchi kingefanya kazi hiyo. Kilichohitajika ni watu wenye kujali na kuweka mipango muafaka. Lakini kwa kutojali matokeo yake ni kufariki zaidi ya watu 45 katika wilaya moja. Hatujui waliokufa katika wilaya nyingine nchini. Wala hatujui ni watu wangapi tena wamekufa baada ya hao wa awali.

Suala hili limetia doa kubwa kwa nchi yetu, kutokana na mazingira yaliyopelekea kutokea kwa vifo hivyo. Na Waziri Mkuu Mh. Frederick Sumaye alishuhudia mwenyewe hata katika hali hiyo ya watu kufa bado chakula cha msaada kilikuwa hakijasambazwa.

Doa hili limetokea wakati serikali yenyewe ilishatangaza toka na mapema kwamba kutakuwepo na upungufu wa chakula na ikaahidi kwamba itahakikisha kwamba hakuna anayekufa kwa njaa.

Heshima ya taifa lolote inafungamana na jinsi taifa hilo linavyothamini raia wake. Kilichotokea tumejidhalilisha ubinadamu wetu na utaifa wetu.

Chakusikitisha zaidi haieleweki kuwa kashfa hii ya taifa inapata uzito wake. Hakuna aliyewajibishwa wala hakuna dalili kuwa taifa lipo katika msiba.

Mdahalo wa maendeleo una tija gani kwa mwananchi iwapo mdahalo wenyewe hausaidii kuichagiza serikali ikawaona wenye njaa kwa jicho la huruma kabla ya kuwaongezea wenye nacho.

Matukio ya nyuma kama yale ya watu kuchomewa nyumba Nzasa, kipindupindu kudumu katika miji kwa kukosekana usafi wa mazingira, huduma safi za afya na maji salama kwa binadamu, mauaji ya raia wakiwa mikononi mwa polisi, mauaji ya Mwembechai n.k. yanajenga taswira ya kutisha kwa mustakabali wa nchi yetu.

Taifa la watu wanaoona kuwa ni jambo la kawaida kwa raia wao kuuliwa au kufa bila ya wao kufanya jitihada zozote, linaonyesha ishara ya hatari.

Si suala la chama gani cha siasa ni suala la uhai wa raia wa nchi hii ikilinganishwa na anasa za viongozi wetu.

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook