BAADHI ya wenyeji wa wilaya ya Handeni mkoani Tanga wameunga mkono kauli ya Prof. Lipumba aliyoitoa katika mkutano uliofanyika kwenye viwanja vya Tangamano mjini Tanga hivi karibuni.
Katika mkutano huo, Prof. Lipumba aliwakumbusha wale walioipigia kura CCM kwamba walifanya makosa ambayo hivi sasa wanastahiki kujilaumu wenyewe.
Mkoa wa Tanga na wilaya zake hasa wilaya ya Handeni ni miongoni mwa sehemu ambazo CCM ilizoa kura katika uchaguzi wa mwaka 1995.
Akizungumza na mwandishi wa habri hizi, mmoja wa wenyeji wa wilaya ya Handeni Bwana Zuberi Gumbo aliunga mkono kauli hiyo kwa kusema kwamba matatizo ya njaa na dhiki pasipo msaada wa serikali ni "ni zawadi" kwa wananchi wa wilaya hiyo kufuatia hatua yao ya kuipigia kura CCM huku wakijua haijafanya chochote cha maendeleo wilayani humo.
Aliwaomba wakazi wa wilaya hiyo na mkoa mzima wa Tanga wapime uzito wa kauli hiyo ya Prof. Lipumba kwa kulinganisha na hali mbaya inayowakumba hivi sasa.
Aidha Bwana Zuberi aliwataka wenyeji wa wilaya hiyo waamke na waazimie la kufanya katika uchaguzi ujao.
Wakati huo huo, Prof. Lipumba alizungumza na akina mama wa mkoa wa Dar es Salaam katika ukumbi wa Starlight Jumamosi iliyopita.
Katika mazungumzo hayo wanawake wa Dar es Salaam walimueleza matatizo mbalimbali yanayowakabili ikiwa ni pamoja na huduma mbovu za hospitali hasa kwa wazazi, kunyanyaswa kwa akinamama wanaofanya biashara ya mama ntilie na hali nzima ya maisha kuwa ngumu.
Baadhi ya akinamama hao waliahidi kupita nyumba kwa nyumba katika maeneo yao kujadili madhila ya serikali ya CCM na hatua za kuchukua ifikapo mwaka 2000.
Akizungumza mara baada ya mkutano huo wa Starlight Bi Zainab mkazi wa Manzese ameliambia gazeti hili kuwa tatizo kubwa walilonalo akinamama wengi ni hali duni ya maisha ambayo CCM imekuwa ikiitumia "kuwarubuni" kuwapa mikopo kila inapokaribia uchaguzi.
"Hali hii inaathiri sana maamuzi ya akinamama lakini sidhani kama kwa kibano cha awamu hii yupo mama atakayerubuniwa kuipa kura CCM", alisema mama Zainab ambaye ni mfanya biashara ndogo ndogo katika maeneo ya Mwembechai.
Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge utafanyika mwakani mwezi Oktoba ambapo Watanzania watapata fursa ya kuchagua serikali kupitia utaratibu kwa ajili ya kipindi kingine cha miaka mitano.
|
|