Na Kassim Bilo
BALKAN ni eneo ambalo wenyeji wake wamezongwa na mijeledi ya historia katika uhai wa roho zao, watu hawa wamevumilia udhalimu wa tawala za kidikteta na kikomunisti kwa takriban miaka sabini huku wakijaribu kuhifadhi mila na desturi za dini na utamaduni wao.
Waislamu wa Balkan ambao kwa wingi wanaishi katika maeneo ya Albania Montenegro, Kosovo, Bosnia na Herzegovina na Bihac hawajawahi kuwa na jukumu la kudhibiti hali au mwelekeo wa maisha yao.
Madikteta wa kikomunisti waliwanyang'anya aina zote za uhuru wa Kiislamu na kuwaweka chini ya shirikisho kuu ili kuwatenganisha na imani yao.
Nchini Albania kiongozi wa kikomunisti Anvar Khoje aliwatawala Waislamu zaidi ya miaka hamsini katika mfumo wa kikatili na unyonyaji na kutenda mambo mabaya ambayo hata mchungaji wa kondoo hangeweza kuwatendea kondoo.
Serikali dhalimu ya kikomunisti ya Yugoslavia ya zamani haikuwapa Waislamu wa Bosnia na Herzegovina na Kosovo nafasi ya kupumua. Wakomunisti walijaribu kuwanyang'anya Waislamu turathi zao za kitamaduni katika maisha yao na hata wakati mwingine kuharibu Misikiti na vyuo vya Qur'an.
Uchezaji wa kamari, ulevi na uzinifu vilikuwa huru kwa yeyote lakini kwa upande mwingine miradi mingine ya kidini iliangaliwa kwa woga na macho ya walinda doria wa kikomunisti.
Sera ya ukomunisti iliyotumika kwa kipindi cha miaka sabini haikuwa na lolote la manufaa kwa umma bali ililipua mlipuko huo ulioanzia katika makao makuu ya ukomonisti mjini Moscow na kuzagaa.
Serikali hizi za Ulaya Mashariki hazikuweza kuhimili misukosuko iliyofuatia na hatimae zikaangushwa na raia waliokuwa vifungoni kwa miaka mingi.
Matukio haya yalitokea kwa kasi na kwa muda mfupi hivi kwamba hakuna aliyeweza kuwaokoa na kuwaongoza wananchi katika pahala panapostahiki. Na katika kiwango cha juu viongozi wao hawakuwa na fikra kamilifu za mageuzi mapya.
Hivyo basi nchi hizi za Mashariki Uropa zilianguka katika vita vilivyokuwa na asili ya kikabila na kusababisha mgawanyiko wa nchi. Katika nchi zilizoanguka ni Yugoslavia ambayo iligawanyika maeneo madogo sita yakiwemo Croatia, Serbia, Bosnia, Herzegovina na Slovenia.
Baada ya muda usio mrefu maadui wa Uislamu katika bara la Ulaya walileta mizozo ya kikabila na kidini ili kuwaangamiza Waislamu wa Ulaya. Serbia ilipewa silaha ili kuwauwa kinyama Waislamu wa Bosnia na Herzegovina.
Mauaji haya ya kikatili yalikuwa mabaya zaidi dhidi ya Waislamu walikuwemo watoto na wanawake.
Jambo la kusitikisha ni kwamba kulikuwako na visa vya kuwanajisi wanawake.
Leo tunaendelea kushuhudia vitendo vya uhalifu katika eneo hilo katika jimbo la Kosovo ambalo asilimia sabini ya wakazi wa sehemu hiyo ni wa asili ya Waislamu wa Kialbania hawajawahi kuona amani na utangamano kwa miaka michache iliyopita. Misikiti yao, vyuo na nyumba zao zimeshambuliwa na kuharibiwa au kutishwa vikali.
Yale waliyoyatenda huko Bosnia na Herzegovina, wanataka kuyarudia huko Kosovo, Wakosovo wamelazimishwa kwenda kwenye milima na majangwa bila ya vifaa vyovyote vile vya kujimudu.
Sasa hivi ni Mwenyezi Mungu (s.w.) ambaye ni mjuzi wa yote ndiye ajuae baada ya Kosovo ni nchi gani itakayokumbwa na jinai la uhalifu. Vile vile ni kwamba suala tuliulizalo ni kuwa iwapo Umoja wa Mataifa utaweza kuleta suluhu la mzozo huu, hili ndilo swala ambalo nchi za Magharibi zinazodai kuleta Demokrasia lazima zijibu.
|
|