DODOSO LA KUTAFAKARI
 
Tutahadhari na Wachawi
 

Na Kipondo wa Changarawe

Mtu kuwa mchawi si lazima awe ni bingwa aliyebobea katika fani ya kupika mauzauza na umahiri wa kuwapiga watu ndumba au kuyatega majuju. Hivyo hivyo, mtu kutumika si jambo baya endapo kutumika kwake kutakuwa ni katika kuidhoofisha mizizi ya ukandamizaji ili haki na uadilifu viote na kustawi kwa manufaa ya wanadamu wote. Atakayeitetea dhulama kwa kauli na vitendo ni mchawi kadhalika na yule apigaye ukimya bila ya kuchukua hatua za kisheria.

Unaweza ukapatwa na mshangao wa inakuwaje dhalimu na mpambe wake, waipingao haki, na wanaonyamazia umwagaji wa damu za raia kuwa ni wachawi? Naam ni wachawi! Ni wachawi wanaoiroga amani itoweke kwenye jamii hali yakuwa wanafahamu kuwa gharama kuirudisha ni kubwa sana.

Dhulma, unyonyaji, unyanyasaji, uonezi, ukandamizaji, majungu, uchochezi, fitna, urongo, upendeleo, ubadhirifu, husuda, chuki, udini na undumila kuwili ndio uchawi wenyewe. Kwa nini? Kwa sababu vinaondoa upendo, Mshikamano, umoja na kujenga matabaka, dharau, kujiona faraka na hatma yake ni kuilipua jamii.

Kimsingi, huu ndiyo uchawi mkubwa wenye teketeza amani. Amani inapokosekana viumbe vyote vinakuwa katika dhiki na maisha yaliyokorogeka ya kimashaka mashaka.

Waislamu na Wakristo kama raia ni watu wanaofahamiana na wameridhika kuishi pamoja kama taifa katika msingi wa kukubaliana kutokubaliana kiimani lakini wenye kutendeana haki na kutokudhulumiana. Huu ndio msingi wa kuishi pamoja.

Kwa ujumla hakuna mristo wala Muislamu asiyejua miiko inayowaunganisha wao kuwa taifa moja. Ni kutokana na ukweli hu ndiyo maana ikaundwa katiba itakayotumika katika kumpa kila raia haki inayomstahiki bila ya kuzingatia dini au dhehebu analolifuata.

Kazi ya uchawi ni kupandikiza chuki baina ya watu walioaminiana na kushibana ili kutengeza ufa utakaoleta mfarakano ambao matokeo yake ni kuvurugika na kuchafuka kwa amani katika jamii. Kabla ya kuifikisha jamii kwenye kielele cha kuyaoga maji yenye damu, uchawi huwaandaa na kufanya tabaka la watu walio magwiji katika kupora haki za watu ambao kwa kupitia huo uchawi wamefanywa kuwa ni kundi linalodhalilika mikononi mwa wachawi.

Inapaswa kueleweka kuwa kila anayefanya jitihada za kuiharibu jamii ni mchawi. Ni mchawi kwa sababu kikomo cha jitihada zake ni kuporomoka kwa maadili mema na kutoweka kwa maisha ya kutendeana haki na uadilifu. Jamii ikishafikishwa hapo amani huwa ni kitu cha kufikirika tu.

Inasikitisha na kutia khofu inapodhihirika kuwa kuna watu wa naofanya jitihada za kutufikisha kwenye machungu. Kumruhusu mwanafunzi wa Kiislamu avae, na kuswali akiwa kwenye mazingira ya shule linakuwa ni jambo zito miongoni mwa walimu wakuu na wakuu wa Shule za Serikali. Si hivyo tu bali wakati mwingine mabinti wa Kiislamu walioamua kutekeleza mafundisho ya dini yao wanaandamwa kwa vitisho na kuwekewa ugumu ili waache kwa kuchelea kuhujumiwa katika masomo. Huu ni uchawi na hawa wanaofanya hivyo ndio wachawi wenyewe.

Usisahau kuwa wapo wale wafanyao makusudi, wale wenye azma na ghera ya kuyaeneza maguruwe kila mahali na kuyaacha yavinjari kwa wasaa mpaka misikitini na kwenye vyombo vya Waislamu. Kuweka mafuriko ya mabucha ya nguruwe katika maeneo ya mchanganyiko. Lengo nini?"

Wapo wachawi, wanaowanga kwa kupga matarumbeta na kupuliza vibuyu huku wakimba nyimbo za kiuchochezi. Kwa husuda na chuki wanashabikia dhulma na mauaji. Vinywa vyao vinamwaga petrol na kalamu zao zinawasha moto wa kuilipua amani. Inavyoonesha wanajisikia raha sana wanapotamka na kuandika. Waislamu wenye siasa kali" na kuzipamba kurasa kwa maandishi makuba bila ya kutafakari athari yake katika jamii.

Nataka kuipigia mstari nukta muhimu ya kuzingatiwa na kuiweka akilini. Kwamba mtu kuwa mchawi si lazima awe bingwa aliyezama katika taaluma ya kutengeneza majuju na kupiga ndumba. La hasha! Mchawi hasa ni yule anayeifisidi jamii. Mathalan, anapojitokeza mtu akachuna uso kuwahimiza watu wazini salama kwa kondom.

Ni mchawi kwa kuwa dhamira yake ni kutaka kujenga taifa la wahuni, wazinifu, machangudoa, wabakaji kwa kubomoa taasisi ya familia. Inaonekana kama hakuna maneno mengine ya kuwatahadharisha watu wajikinge na ukimwi isipokuwa ni kuwaamlia kuwa watumie kodom. Hakuna tafsiri nyingine yoyote itakayokuwa mnasibu ya kumtafasiri mfano wa mtu huyu ni mchawi anayekusudia kuwangamiza jamii kupitia ufusuka.

Mtu akiumwa malaria au taifodi, tu kisema kuwa ni magonjwa ya kawaida yanakubalika akilini, hata kama yawe ni magonjwa ya nayoongoza katika kuyachukua maisha ya watu bado huzuni yake inakuwa tofauti na ile ya ukimwi. Ukimwi si ugonjwa wakawaida kwa sababu hauna kinga wala dawa zaidi ya kuachana na tabia ya kiasharati, na wala haijathibitika kitaalamu kinga inayoitwa kondom. Ndiyo maana ya kusema kwamba yeyote atakayedai kuwa komdom ni kinga, anairoga jamii.

Upo msemo usemao kuwa "kiingiacho si najsi bali kitokacho". tukiyahusisha matumzi ya mdomo na hichi kipande cha mwisho cha msemo tutagundua ukweli uliomo. Ni kweli kwamba ulaghai, urongo udanganyifu pamoja na maneno ya uchai na uchochezi yanatoka kinywani. Imekwisha tangazwa na kujulikana kuwa hakuna kinga ya ukimwi inayoitwa kondom. Ni mtaalamu gani nchini aliyegundua kuwa kondom ni kinga.

Inatupasa tuyasikilize maneno kwa sikio la tatu kabla ya kuyatekeleza huku tukizingatia kuwa wachawi wapo wengi. Ni lazima tuchukue tahadhari na kutahadharishana kila wakati. Tukienenda namna hii tutakuwa miongoni mwa vipenzi vya Allah (s.w.), 'Ululul-albaab' ambao macho yao yanaona kwa undani kabisa kuliko waonavyo wanyama. Na tuyatafakari maneno kinyume nyume ili tufahamu undani wake. hebu tutafakari kwa pamoja!

Kuyaimarisha maadili mema ndiyo msingi wa kutengemaa kwa mtu binafsi, familia, jamii na taifa kwa jumla. Na ili ubindamu uwepo na kuyatawala maisha ya watu hapana budi kuwatanguliza mbele washika usukuni wenye heshima, wakweli, waadilifu, wanojali haki usawa kwa wote. Wachawi wanapotangulizwa mbele ni lazima jamii itanuka.

Jamii itanuka uvundo. Kiini chake ni wachawi ambao hawana lengo la maisha isipokuwa ni kujitahidi kuwa wanyama bora ambao mawazo na fikra zao zinalenga katika kushibisha matumbo pamoja na kuzima kiu za viungo vilivyopo baina ya miguu bila ya kuzingatia utu na ubindamu. Hii ndiyo nukusi inayozaa mabalaa yenye kuzaliana yanayovurga amani ya jamii.

Tusije tukashangaa tutakaposhuhudia watu wanaoandamana na kwa kutaka demokrasia ya kweli au kudai haki zao wakapelekewa jeshi liwatie mkong'oto; yakaruhusiwa maandamano ya kudai mipira ya zinaa ziongezwe kwa kisingizo cha ukimwi au kudai bei za pombe zipunguzwe. Kilele hiki kitakapofikiwa basi kizazi kitakuwa kimesharogeka.

Dodoso liliwahi kudokeza katika moja ya maudhui zake iliyowakilishwa kwa anuani ya "Kujinasua mtegoni" kuwa ni moja kati ya nyenzo muhimu wanazozitumia madhalimu ni kuwazamisha watu kwenye kina cha unyama ili dhulma itendeke bila ya pingamizi. Ili ifike mahala ambapohaitahofiwa kuwa mapesa ambayo serikali imefanikiwa kuyakusanya kutoka mifukoni mwa wananchi zimetumika katika shughuli gani zinazowanufaisha wananchi.

uchawi ukubwa ni kufanya mambo yote yanayopelekea kukosekana maisha ya upendo, furaha na amani miongoni mwa wana jamii. Kuyafumbia macho mauaji ya kinyama, kuyaangukia kwa uziwi na upofu madai ya kweli ya wanajamii wanaodhulumiwa, kuwatupia shutuma wanaoonewa kwa lengo la kuwanyamazisha wasidai haki zao, na mengine mengi yanayofanyika kwa madhumuni hayo yanaingia kwenye kundi la uchawi.

Wachawi wa firauni walitanabahi na kung'atuka baada ya kuwabainikia haki na ubaya wa kila walichokuwa wanakifanya katika kuendeleza dhulma na ukandamizaji dhidi ya wanajamii waliofanywa kuwa tabaka la chini; tabaka la watu waliofanyishwa kazi ngumu na kuambulia kuchinjiwa watoto wao wa kiume. Haki ilipowafikia wachawi wafirauni hawakupata kigugumizi. Pale pale wakampiga pande firauni na kumwambia lolote na liwe.'

Hakika Firauni alitakabari katika ardhi, na akawafanya watu kuwa matabaka. Akalidhoofisha kundi moja miongoni mwao, akiwachinya watoto wao wanaume na kuwaacha hai watoto wao wanawake. Hakika yeye alikuwa miongoni mwa waharibifu.

Wakaja wachawi kwa Firauni, wakasema: "Tutapata ujira ikiwa tutashinda." Akasema: "Naam, nanyi bila shaka mtakuwa miongoni mwa wasiocheza mbali na ikulu."

basi wachawi wakazozana kwa shauri yao baina yao na wakashauriana kwasiri. Wakasema: hakika watu hawa (Musa na Haruni) ni wachawi. Wanataka kukutoeni katika nchi yenu kwa uchawi wao, na wanataka kuondoa sera yenu iliyo bora kabisa". Kwa hiyo kusanyeni hila zenu kisha mfike kwa kujipanga safu, na kwa yakini atafuzu leo atakayeshinda.

Basi walipotupa waliyazuga macho ya watu na wakawaogopesha, na wakaleta uchawi mkubwa. Na tukampelekea Wahy Musa yakwamba, "tupa fimbo yako." Mara ikavimeza vyote vile walivyovibuni. Ukweli ukasimama na yakaharibika waliyokuwa wakiyatenda. kwahiyo walishindwa hapo na wakawa wenye kudhalilika. Hakika wao wametengeneza kila za uchawi tu, wala mchawi hatafaulu popote afikapo.

Basi wachawi wakaangushwa chini wanasujudu, na kusema; "Tumemwamini Mola wa Mussa na Haruni". (28:4, 7:113-119, 20:62-64, 69, 70).

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook