BARUA
 
 
Barua ya wazi kwa Mwenyekiti wa Tume ya Jiji
 

Tunapenda kuandika kutoa yetu maoni, juu ya sheria ndogo zinazotawala ama jiji ama serikali za mitaa.

Sheria hizo zinafanya kazi kwa Raia wa kawaida, na hususani wale wasio na mahusiano ya karibu na vigogo. Kuna ufugaji wa ng'ombe jijini, ulimaji wa migomba ambayo huwa maficho ya vibaka, wezi katika maeneo mengi ya wazi jijini hasa maeneo ya Hananasif, Sinza Manzese migombani na sehemu nyingine nyingi za jiji. Yote hayo yanafumbiwa macho.

Kibaya zaidi ni kuzuka kwa mtindo wa kufunguliwa ma-bar katika sehemu nyingi za wazi jijini hasa vilivyokuwa viwanja vya CCM. Sasa tunahoji hivi hakuna shughuli nyingine kama vile michezo kwa watoto, Police Post, kuwapa vyama vya upinzani maeneo ya kujenga ofisi ama taasisi za dini kujenga sehemu za kufanyia shughuli za dini kama vile madrasa, kanisa ndogo ama mihadhara?

Ufugaji mifugo inashindikana sababu ni tatizo linawagusa wakubwa kuwa miradi ya wake zao. Hivi kweli kama uwezo upo kama tuonavyo kuwa na magari, vipi yasitafutwe mashamba ya mifugo nje ya jiji? Leo Oyster-Bay, Upanga, Kurasini kote kunanuka vinyesi vya ng'ombe na nguruwe. Nani wa kulaumu? Kweli mtunga sheria ndie mvunja sheria. Aibu gani!

Mabalozi wetu wote wa nje wako maeneo hayo hayo ambayo yameenea mifugo. Je sio kero? Sijui katika kutembea kwenye viongozi wetu mmefika miji ya wenzetu mkaona hivyo na ndio ustaarabu mliona toka huko? Inashangaza sana kukuta kundi la ng'ombe makutano ya Kaunda na Zambia Roads Oyster-Bay yakiwa malishoni. Basi hata suala hili linahitaji wataalamu kutoka nje na fedha za kigeni kuja kulitatua? Ama hadi Bunge likae Dodoma kutunga mswada juu ya hili? Dhahiri vigogo mnafanya makusudi.

Huko Kimara, Mbezi zote, na Tabata kunakoitwa kwa wasomi ama watu wenye nafuu ya maisha ndio kuna adha kubwa. Kila baada ya nyumba fulani ni milio ya ng'ombe na nguruwe tu. Kwa kweli hali hii haipendezi, ila wenye nguvu wanafanya kutimiza ubinafsi wao. Imefikia mahali hata baadhi ya mitaa imefungwa ama kwa kuwepo Bar-Ama Danguro (Guest House) katikati ya barabara kwa mfano Mwananyamala B Eneo la sokoni Kati Avot Centre na mtaa wa Malanga ipo huest House katikati ya barabara, na mstahiki mwenyekiti wa jiji alishawahi kuitwa mara kadhaa na kutofika wala kutuma hata muwakilishi wako. Je hali hii tukueleweje? Hata kama aliye jenga ana hati miliki. Je kabla ya kutolewa kiwanja hicho, ramani haikutazamwa? Isitoshe, mbali na kufunga hiyo barabara limemezwa eneo la Shule ya Mwananyamala pamoja na soko. Je Mwenyekiti wa jiji hii ni haki?

Wananchi waliwahi kukuandikia wewe binafsi, na hadi leo hakuna hatua yoyote uliyochukua. Mbele ya barabara hiyo kuna eneo la wazi ambalo lilikuwa kiwanja cha CCM ambacho kiliuzwa kwa kinyemera, kuna mabaa kama ilivyo uwanja wa Sembuyagi kule Temeke.

Mbele yake ni mtaa wa Malanga, eneo la wazi lilikuwa jalala miaka mingi, leo ni Bar sasa endapo maeneo yote jijini yatakumbwa na hali hii, hawa watoto wetu watachezea wapi? Kila Eneo ni bar, garage, Grocery, hali hii itatufikisha wapi? Na kwa bahati mbaya zaidi uchunguzi wetu unabaini kuwa ama shughuli hizo zote zina baraka za vigogo ama ni shughuli za vigogo wenyewe. Sasa kila mtu akitaka afanye aonavyo tutafika wapi? Jiji bado chafu, Tume inashindwa kukabili na kudhibiti uchafuzi. Zoezi la uzoaji taka linadorora tokea lianze.

Mabucha mengi machafu hayana bomba za maji, mizani zote mbovu hazikaguliwi ndio maana ukinunua kilo 10 nyama utaondoka na kilo 9 tu halali. Mahoteli vyoo vichafu ama hamna kabisa. Hakuna chombo cha maji moto (Heater) kuoshea glass. Wahudumu hatuwajui afya zao hawapimwi.

Kwa hali hii, Afisa biashara, bwana Afya wa eneo, askari wote muda huo wanahakika ya kuishi bila hata kugusa mishara yao. Kila mmoja anahakika ya kubandikiwa chai baada ya nusu saa atafika nyumbani na mkate, nyama, mayai na fedha. Hebu tuondolee keo hizi kabla ya uchaguzi wa madiwani waige mfano, na wewe jukusifu kwamba umefanya kazi nzuri.

Ni sisi:
(1)Yunusu Mohamed
(2) Ally Maulidi
Kny:Wananchi wakereketwa
Mwananyamala B
S.L.P. 15405
Dar es Salaam.


Viongozi wetu mna agenda gani?
 

Ndugu Mhariri

NIMESHANGAZWA sana na hatua ya baadhi ya viongozi hapa Mwanza waliosimama kumtetea Bw. Msabaha. Kwanza nawashauri wasipitie upofu wajue Waislamu wapambanuzi hawawezi kupumbazwa.

Pili mlikuwa wapi muda wote kuhusu suala la Mwembechai. Tatu, hivi sasa mnaagenda gani au ndio tukielekea mwaka 2000. Au ndio mmeshaanza yale yale ya mwaka 1995?

M.M. Rubeya,
Mwanza.


Udini watokota Chuo Kikuu

Ndugu Mhariri

Februari 17 Jumatano 1999 Chuo kikuu sehemu ya Mlimai, ulifanyika uchaguzi kupata uongozi wa wanafunzi (DARUSO).

Historia inaonesha nafsi ya Urais ndio inayopewa nafasi kubwa katika chaguzi zote. Hata hivyo Waislamu huko nyuma walikata tamaa ya kugombea kutokana na sababu anuwai.

Lakini uchaguzi huu ninaousema hivi sasa, alijitokeza bwana Bashiru Ally (Mwislamu) na mpinzani wake B.G. Maimu (Mkristo). Basi ushindani ulikuwa mkubwa na hata ikafikia baadhi ya Waislamu kujeruhiwa.

Kwa sababu ya chuki yao hawa wapinzani wa Uislamu, walimchafulia jina bwana Bashiru kwamba yeye ni Siasa kali ana udini, yeye ni Osama bini Ladeni ili mradi tu kumweka katika mazingira mabaya; na hayo ndio yaliyapelekea Bashiru Ally kushindwa.

Vijana wa chuo Kikuu ndo viongozi watarajiwa wanajawa chuki ya dini kiasi hiki, je taifa litaelekea wapi hapo baadaye? Mbegu hii ya udini itazaa nini? Je Kosovo, Bosnia, Rwanda, Zaire Burundi ama yatakuwa maafa ya aina yake..

Natoa mifano hii kwa sababu kulikuwepo na ubaguzi na kupelekea kunyanyaswa kwa kundi moja. Lakini ilifika kipindi waonewa walichoka na kuunda jeshi la kuwakomboa. Wanatoa nafsi zao bila woga, kwani wameona vyote sawa kufa au kuishi:

"Hawana watakachopoteza maishani mwao isipokuwa minyororo yao" Karl Marx:

Waislamu ambao bado wamelala usingizi fofofo, amkeni acheni mambo ya kukalia kupewa kitu kidogo na kuuza thamani ya kura zenu. Hili ni funzo kwa Waislamu kwamba wenzenu wanaangalia dini kwanza halafu mambo mengine. Sio watu wanajidai wao wanadamu ya kijani ya CCM halafu wanakuja kuua Waislamu kwa bunduki halafu wanapongezana.

Kila ufanyalo, hata ile kura yako utalipwa.

Shankaula
Box 35152
Dar es Salaam


Mawe ya NCCR Mageuzi siyo ya Mwembe Chai?
 

Ndugu Mhariri

Maandamano ya Jumamosi Aprili 24, mwaka huu ya wafurukutwa wa NCCR-Mageuzi yamedhihirisha tena unafiki wa serikali hii.

Waheshimiwa wa ngazi za juu Serikalini walisema kuwa polisi wasingeweza kuwaacha Waislamu wawapige mawe wakati wao wana bunduki, kwani polisi sio mbwa. Polisi wa Serikali hiyo hiyo waliowauwa Waislamu Mwembechai kwa kujihami na mawe, wakashindwa kuwauwa wamasai wenye silaha na polisi ndiyo waliokimbia. Na sasa hivi jumamosi wamekamata gunia la mawe la wafurukutwa lakini hawajauwa. Mwembechai ni dini ndio iliyopelekea damu kumwagwa.

Hata suala la dhamana pale mahakamani Kisutu halikuwa la mizengwe kama ilivyokuwa wakati wa Mwembechai.

Watuhumiwa wa NCCR walipewa dhamana bila kikwazo wala madai kama yale yaliyokwamisha dhamana ya watuhumiwa wa Mwembechai.

Tumewaona kinamama walioandamana siku hiyo, lakini hawajadhalilishwa kama walivyo fanyiwa kina mama wa Mwembechai. Sasa kama sio dini tena ni nini. Tusidanganyie tena, serikali haitupendi.

Wanamsaka Sheikh Ponda kwa madai eti amehatarisha amani. Hivi mbona Mrema aliyeandaa maandamano ya NCCR hajakamatwa kwa kuhatarisha amani? Lazima kuna kitu zaidi, nacho ni udini.

Waislamu tunayaona kwa jicho pevu mambo hayo, udini huu na ubalakala huu! Wivisheni jungu lakini mjue tutakula wote!

Mama Hijra
Box 3001,
Mwanga-Kilimanjaro


Makafiri wasituandalie agenda
 
Ndugu Mhariri

NAPENDA kuwafahamisha na kuwafunua macho ndugu zangu Waislamu popote walipo kwamba, mbinu mojawapo ya makafiri ya kuturudisha nyuma ni kutuundia agenda ambazo zitatushughulisha na kutupotezea muda wetu mwingi kuzijadili na kuzitafutia ufumbuzi badala ya kushughulikia mambo yanayotuhusu na kuyatatua matatizo yetu yanayotukabili Waislamu nchini na duniani kote kwa ujumla.

Tafadhalini tudumu katika kupigania haki zetu, tudai wauaji ya Mwembechai wafikishwe mahakamani. Hayo ni sambamba na kuendeleza programu za kujiletea maendeleo.

Fatma Mussa,
Mikindani,
Masasi.


Mhariri tekeleza ahadi

Ndugu Mhariri

NAPENDA nichukue fursa hii ambayo amenijaalia Allah (s.w.) kwa kuipata niweze kutoa machache niliyonayo katika gazeti letu tukufu la ANNUUR.

Katika toleo nambari 12 na 195 ndugu Mhariri umejitahidi kutusisitiza wasomaji wa gazeti hili la ANNUUR kutuma barua zao kwa wingi na ukaahidi kuwa zitachapishwa bila upendeleo wowote.

Lakini kilichonifanya nishindwe kuelewa msisitizo huo kutokakwa Mhariri kama msomaji wa ANNUUR nilituma barua yangu mwezi wa pili yenye kichwa cha habari kinachosema "kutekeleza amri ya Allah (s.w.) Waislamu tusipewe majina". Cha kushangaza ni kwamba barua hiyo haikuchapishwa na kwa hiyo ujumbe ambao nilipenda uufikie jamii haukufika.

Kumbuka kwamba kuwaambia wasomaji wa gazeti hili watume barua zao kwa wingi na zitachapishwa bila upendeleo wowote ni kutoa ahadi kwa wasomaji. Na Mwenyezi Mungu anasemaje kuhusu ahadi? Mwenyezi Mungu anatutahadharisha kuhusu ahadi anasema: "Tekelezeni ahadi zenu hakika ahadi zitakuwa zenye kuulizwa". (17:34)

Kwa hiyo wasomaji wa ANNUUR wanapotuma barua zao halafu nyingine hazichapishwi ina maana unakwenda kinyume na ahadi yako uliyowaahidi wasomaji. Natumaini kuwa kutokana na aya hiyo hapo juu utazichapisha barua zote za wasomaji utakazozipokea ofisini kwako - inshaAllah.

Sharifa Yusuf,
Mudio Islamic Seminary,
P.O. Box 8387,
Moshi.
 

Andika barua fupi juu ya masuala muhimu katika jamii; jenga hoja madhubuti, hoji au elimisha itachapishwa. - Mhariri
 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook