Edita mwingi wajina, japo
pembeni niweke,
Kwangaya bure kununa, mambo
haya yaepuke,
Baruwa nilivyoona, cheo
wakipigateke,
Wakubwa tukusanyike, watoto
tuwaokowe.
Watoto tuwaokowe, wakubwa
tukusanyike,
Kutunga kwao mayowe, mnadi
jina waweke,
Kutunga kwao mayowe, mradi
jina waweke,
Wakubwa tukusanyike, watoto
tuwaokowe.
Kapiteni Wakangara, kwangaya
wachamakeke,
Ulikuwa jingabora, nguo
zako ujivike,
Waiacha hadi bora, yakike
ujipachike,
Wakubwa tukusanyike, watoto
tuwaokowe.
Wapopote wema wenu, mwisho
mje muumbuke,
Kulalia na uvungu, kwanza
ngoja niwacheke,
Kweli jama haki yenu, roho
ni za pekee,
Wakubwa tukusanyike, watoto
tuwaokowe.
Mzee Mkanyageni, hodari upekepeke,
Utaingia motoni, kupenda
taji uvike,
Jongoo ni Bininyani, mpango
kura uvike,
Wakubwa tukusanyike, watoto
tuwaokowe.
Beti saba nimefika, kalamu
budi niweke,
Kisondoka ninacheka, swala
kugeuzwa mate,
Mkwawa hana mashaka, miguu
akupachike,
Wakubwa tukusanyike, watoto
tuwaokowe.
Mohamed Juma A. Kisondoka
Kibindu-Kwamarungu -
Uziguwa - Box.
Wendapo kuoa mke, chungua
mambo matatu,
La kwanza wazazi wake, tabia
iwe ya utu,
Wasiwe wapeke peke, mwana
kumvunja utu,
Muoe mwana wa watu, ajue
sheria zake.
Ajue sheria zake, muoe mwana
wa watu,
Wazazi wapekepeke, hawana
sheria kitu,
Kaka utamwacha mke, japo
upende si kitu,
Muoe mwana wa watu, ajue
sheria zake.
Tizama wazazi wake, wajue
mambo ya utu,
Mkigombana na mke, wazazi
wafanye utu,
Wewe pamoja na mke, wawaiteni
watu,
Muoe mwana wa watu, ajue
sheria zake.
Tizama fadhila zake, nakwambia
mwanakwetu,
Kuvamia wanawake, viumbe
usithubutu,
Mtizame mwendo wake, kichwa
kisiwe kurutu,
Muoe mwana wa watu, ajue
sheria zake.
Ukioa mwanamke, Halima aitwe
Fatu,
Mjaribu mwenendo wake, tabia
kama ya watu,
Hata na wazazi wake, waseme
yaliyofitu,
Muoe mwana wa watu, ajue
sheria zake.
Tamati hapa niweke, kalamu
nijenge utu,
Waume na wanawake, tusiubague
utu,
Yule na wazazi wake, tuwaombee
balatu,
Muoe mwana wa watu, ajue
sheria zake.
R.A. Mwanahewa (Mzee Simba)
Box 223,
Mbeya.
Mwafrika, Jumatatu
Septemba 17, 1962
BWANA Kassanga Tumbo, Rais wa PDP alisema katika mkutano uliofanywa katika Jumba la Arnautoglu juzi kwa sheria ya Jamhuri inayomfanya Rais wa Tanganyika awe sawa na dikteta, ni sababu mojawapo iliyomfanya ajiuzulu Ubalozi.
Aliongeza kusema kuwa hakuweza kuvumilia kuwatendea raia mabo yasiyofaa. "Mimi sijasema uongo", alitamka, na nitaongoza chama changu kwa vitendo wala sio kwa methali.
Bwana Tumbo alisema kuwa yeye alipinga kwa nguvu zake zote ile sheria ya uraia. Lakini ilipitishwa kwa sababu alikosa kura za kutosha.
Alijitetea kwa nini ametumia jukwaa la TRAU katika mkutano alipotangaza kwamba anajiuzulu kutoka TANU na kuwa Rais wa PDP, Bw. Tumbo alisema alitumia jukwaa hilo ili kuwaaga watu wala hakuhutubia mambo ya siasa.
Mapema, Bw. Lifa Chipaka, mweka hazina wa chama hicho alisema kuwa serikali inalaumu chama chao kuwa kila wakati wanasahihisha tu baada ya kufanya vitendo.
"PDP iliishauri serikali isikope shilingi 12,000,000 za kujengea hoteli mjini Dar es Salaam, bali kila raia atoe shilingi 1 tu kwa sababu kukopakopa si kwema. Lakini serikali haikujibu".
Bw. Chipaka alisema kwamba serikali imeshindwa kutimiza ahadi zake aliposema hakutakuwa na ada za shule na kumbe hivi sasa ada zimepanda kufikia kipeo cha shilingi 960.
Bwana Chipaka alijigamba kwamba kila siku wanapata 100, na hivi sasa jumla yao ni zaidi ya 1,500.
Hotuba zikamalizika kwa kueleza
kwamba matawi 10 chama yatafunguliwa hivi karibuni katika Tanganyika na
tawi la kwanza likiwa Ilala mjini Dar es Salaam.
YULE mzungu ambaye alijitolea kwa polisi mjini Mombasa akisema waya umemkaba na hana mbele wala nyumba, halafu akapatiwa msaada wa shilingi 100 kutoka katika 'mfuko wa Maskini' na Hakimu wa Mombasa alirejeshwa tena kortini Ijumaa akishitakiwa kufanya fujo baada ya kuuchapa mma.
Mzungu huyo, Patrick King, alifikishwa mbele ya Hakimu Mkuu wa Mombasa, Bw. R.J. Quin, siku ya Ijumaa akashitakiwa kwamba alifanya fujo katika Palace Hotel ya Mombasa.
Kortini hapo Ijumaa ilielezwa kwamba mshitakiwa baada ya kujitolea polisi na kusema kwamba alikuwa hana kitu, alifikishwa kortini na Hakimu akatoa ruhusa kwamba apatiwe shilingi 100 kutoka katika 'mfuko wa maskini' ili aendeshee maisha yake mpaka Septemba 20, Alhamisi ijayo ili aeleze ameingiwaje na waya kadiri hiyo.
Atarudi kortini
Jamaa baada ya kupewa mapesa
hayo, baadaye akaja kukamatwa ameunyaka mma na kufanya rafu katika Palace
Hotel.
Mwafrika Juni 22, 1961
BWANA Thomas Marealle ambaye alikuwa Mangi Mkuu tangu mwaka 1952 mpaka alipoondolewa hivi mwaka jana baada ya Wachagga kujichagulia Rais, ameshatangazwa sana na uvumi ambao umeenea kila mahali mjini Moshi, Amerika na Tanganyika kwamba amechaguliwa kuwa Balozi wa Tanganyika.
"Kila mahali mjini pamejaa uvumi huu" amesema Bwana Marealle alipoonana na mwandishi wetu mjini Moshi "lakini sijui uvumi huu umetokana na nani, hali serikali ya Tanganyika haijanieleza lolote".
Bwana Marealle amesema kuwa amepata hata barua za pongezi kutoka kwa watu maarufu huko Amerika na Uingereza kuhusu jambo hilo. "Lakini naamini watu hao ni watu wenye uhakika, na wenye kuaminika, maana wengine wanafanya kazi karibu sana na ofisi ya makoloni, na hawawezi kusema uongo. Huenda uvumi huo umetokana na maofisa wa ofisi ya makoloni, akanena.
Vidokezi Moshi
Hapo mjini Moshi kila mtu alikuwa akisema kuwa Thomas Marealle amechaguliwa kuwa Balozi wa Tanganyika katika nchi ya Uingereza. Wengine wakasema kuwa amechaguliwa kuwa Mkurugenzi katika idara ya Uhamiaji.
Lakini yeye mwenyewe amekanusha kuwa hajapewa taarifa na serikali juu ya kuwa Mkurugenzi, wala kuwa Balozi, isipokuwa anashangaa sana kupata pongezi kabla ya kupata taarifa kutoka serikali ya Tanganyika akiambiwa kama ameajiriwa kuwa Balozi.
Mwenyewe hana habari
Bwana Marealle alikataa kusema
kama ni kweli alipata kuomba kazi katika serikali kuwa Balozi au Mkurugenzi
katika Idara ya Uhamiaji. Lakini akanena kuwa yeye yuko tayari ikiwa ataitwa
kushika nafasi kama hiyo.
Sheikh Karume ambaye alikuwa anahutubia mkutano wa hadhara, ailsema kuwa serikali italinda haki ya kila mtu ili watu wapate uhuru wa kufanya kazi kuleta ustawi.
Akaeleza juu ya mali iliyochukuliwa na serikali: Nyote mwafahamu, alisema Karume, kwamba nyumba, ardhi, zimechukuliwa. Basi hoteli, mikahawa na mejengo ya namna nyingine nyingine yataanza kujengwa hivi punde.
Sheikh Karume akaendelea
kusema, kulikuwa na watu wapatao elfu tisa hapa nchini ambao hawakuwa na
kazi kabla ya kumpindua Sultani. Sasa? Akahoji, wapo watu 26 tu ambao hawana
kazi. Akatangaza kuwa kati ya Juni mosi mwaka huu, mtu wa taifa lolote
ambaye hana kazi atapata alawensi.
Mwalimu ambaye alikuwa akizungumza na Maofisa wakuu wa Jeshi la polisi wanaokutana mjini Tabora, alisema kwa kuwa hata imani za dini ambazo zililetwa kwa njia ya Mitume badi zinaendelezwa kila Ijumaa na Jumapili, ni dhahiri kwamba Azimio la Arusha ambalo lilipitishwa miezi michache iliyopita, bado linahitaji kuelezwa zaidi.
Mwalimu alisema kutokana na kutawaliwa kwa muda mrefu, watu walianza kutia hofu za kuweza kujitawala, na wale waliotawala walizoea tabia ya kutawala na kuifanya kuwa ni haki yao. Kutokana na hayo, wale waliotawaliwa walijipendekeza kwa watawala na kutaka watambuliwe kama watu. Hata waliopata elimu wengine waliitumia elimu yao ili waweze kukubaliwa na kujionyesha kwamba wao walikuwa tofauti na wenzao. Mwalimu alisema huo ulikuwa ni uogonjwa nakwamba bado upo.
Vile vile Rais alisema wengine waliopata elimu waliitumia kuwapa matumaini wenzao na kuonyesha kwamba hata wao wanaweza kuwa na hali kama za watu wengine.
Mwalimu alisema usawa wa binadamu ni wa maumbile na haupatikani kwa kuombwa. Usawa wa binadamu huonekana tu na kukubalika bila mtihani wowote.
Alisema kwamba katika mataifa yaliyotawaliwa na kujipatia uhuru, yako mengine ambayo yanataka kupewa mtihani kupata haki ya usawa. Lakini pia, yapo mataifa ambayo hayahitaji mtihani, nayo huendelea kufanya shughuli zao na kujiona ni sawa na mataifa mengine.
Akizungumza juu ya maonevu katika Afrika, alisemaz; "hatuwezi kuitoa Afrika Mashariki hali ya kuonewa na kunyanyaswa kwa kupata Waafrika wachache wanaofanana na makabaila. Kontinenti letu litaheshimiwa kutokana na hali ya wananchi wote kwa jumla kwa kushirikiana katika kufanya kazi ya kuleta heshima hiyo", alisema Rais.
Akijibu maswali, Mwalimu alisema kwamba tamu ya kutawala ni uchumi. Na kwamba ugomvi kati ya nchi zinazojitawala na zile zilizokuwa zikitawala huzuka wakati nchi zile changa zinaposema kwamba kujitawala bila kushika uchumi, utawala huwa si kamili.
Habari hizi zimeelezwa na taarifa kutoka Youth ya chama cha Frelimo ambayo imetiwa saini na makamu wa Katibu Mkuu wa Youth League.
Taarifa hiyo inaeleza kwamba maandamano hayo yatafanyiwa viongozi wote wa Frelimo kwa jumla.
Inaendelea. "Vijana wote wa Msumbiji, wake kwa waume, mnaombwa kuhudhuria katika ofisi yenu... ili kutayarisha maandamano... Tunamwomba Bw. Mmole atoe maelezo kamili ya kutia kwake saini ile taarifa iliyotoka Cairo na huku anajidai hajui chochote".
Taarifa hiyo inaendelea kueleza kwamba inasikitisha kwamba Halmashauri Kuu ya Frelimo haijatoa matamshi yoyote kuhusu kitendo cha Bw. Mmole mpaka hivi sasa.
Pia inaendelea kueleza kwamba wanatumaini kuwa shabaha ya Bw. Mmole ilikuwa kudumisha ukoloni katika Msumbiji - "jambo ambalo tunalipinga", yaeleza taarifa hiyo.
|
|