JIFUNZE SHERIA
 
Uendeshaji wa Mashitaka - 3
 
Na Dkt. Abdallah J. Saffari
 
Hati ya Mashitaka
 

LAKINI hali ilikuwa tofauti katika kesi ya Uganda v. Keneri Opindi (1965 EA. 614) ambapo mrufaniwa awali alipatikana na hatia ya makosa mawili ya usalama wa barabarani: Kwanza kushindwa kuweka alama ya 'L' kwenye gari lake; pili kuendesha gari bila ya kuambatana na dereva mwenye ujuzi. Shitaka la kwanza lilikuwa chini ya fungu la 9(b) la sheria ya usalama barabarani ambapo lile la pili lilikuwa chini ya fungu la 9 na 12 la sheria hiyo hiyo. Mahakama ya Rufani ya Afrika Mashariki yalikubali kwamba mshitakiwa alikuwa ameshitakiwa na kutiwa hatiani kwa kosa ambalo halikuwepo katika sheria ya usalama wa barabarani. Fungu la 9(b) halikuwepo. Badala yake kulikuwa na fungu la 9 ambalo, hata hivyo, halikuonyesha kosa ambalo mshitakiwa alishitakiwa nalo.

Wakili wa serikali alidai katika hotuba yake mbele ya mahakama hayo kwamba kosa hilo lilikuwepo chini ya kanuni ya 9(b) ya Kanuni za Usalama Barabarani na kwamba bila ya shaka hati ya mashitaka hayo ilikusudiwa kusomeka hivyo. Mahakama yalikataa kabisa hoja hiyo na kusema ilikuwa ni ya kubuni tu. Mahakama yaliangalia hoja ya waendesha mashitaka kutokana na hati ya mashitaka yenyewe na mwenendo wa shauri tu, basi. Japo muhtasari wa kosa ulikuwa bayana kabisa usingetosha kufanya kosa ambalo kwalo mshitakiwa alikabiliwa nalo.

Mahakama ya Rufani yalizingatia hukumu iliyotolewa katika shauri la Abdul Sabur v. R., (1958 E.A. 126) na kulitofautisha na mazingira ya shauri hili la sasa. Katika kesi hiyo mahakama yaliona kuwa ingawa hati ya mashitaka dhidi ya mshitakiwa ilionyesha kosa chini ya fungu la 39(1) badala ya fungu la 40 la sheria ya usalama barabarani, mrufani alikuwa hakuonewa, bali bado alitendewa haki. Kuwepo kwa kosa ambalo mshitakiwa alishitakiwa nalo chini ya fungu la 40 badala ya 39(1) bado kulionyesha kuwa kosa hilo lilikuwepo. Lakini sio katika kesi ya Uganda v. Kaneri Opindi (i.h.j) ambapo kanuni za usalama na sheria ya usalama barabarani vilikuwa sio kitu kimoja. Rufani ya Opindi ilikubaliwa mintaarafu ya makosa yote matatu.

Sharti la pili ni kila Hati ya Taarifa ya Mashitaka lazima ionyeshe muhtasari wa kosa linalodaiwa. Swali ni je, muhtasari gani unatosha kukidhi haja ya sheria? Ni ule ufafanuzi unaofaa kumpa mshitakiwa taarifa ya kutosha mintaarafu ya kosa analoshitakiwa nalo. Aghalabu ufafanuzi huu unakuwa wa aina mbili: wa kosa linalodaiwa kisheria na ule wa uainishaji wa vitu au watu wanaohusika. Mahakama yamesisitiza umuhimu wa yote hayo mawili kama inavyoonekana katika mashauri machache yafuatayo.

Shauri la kwanza la Terrah Mukindia v. R. (1966 E.A. 425) Mrufani alipatikana na hatia ya kujipatia fedha kwa udanganyifu baada ya kushitakiwa kwa makosa hayo matano. Kosa la kujipatia kitu kwa njia ya udanganyifu huwa kamili tu pale ambapo mtu huyo amefanya udanganyifu huo kwa nia ya kuiba mali au kitu kinachohusika. Sasa, mashitaka ya nne na ya tano katika Hati ya Mashitaka dhidi ya mrufani hayakueleza kuwa mrufani alifanya udanganyifu na kujipatia fedha hizo kwa nia ya kumwibia mwenyewe. Kutokana na sababu hizo, iliruhusu rufani dhidi ya mashitaka mawili ya kujipatia fedha kwa udanganyifu.

Lakini katika shauri la Sosipeter Opale Idiawo v. R., (1962 E.A. 661) Mahakama ya rufani ya Afrika Mashariki yalikuwa na msimamo tofauti na ule ulioelezwa katika kesi iliyotajwa punde tu hapo juu. Sosipeter Idiawo alipatikana na hatia ya kuichoma nyumba ya Bwana Ojulong kinyume cha fungu la 307, Kanuni ya Adhabu, Kenya. Muhtasari wa kosa hilo haukuelezwa kuwa mshitakiwa alifanya hivyo 'makusudi' au 'kinyume cha sheria'. Mahakama hayo yalikiri kwamba dhahiri Hati ya Mashitaka yale ilikuwa na athari ya kutokueleza iwapo mrufani aliichoma nyumba ya Ojulong makusudi au kinyume cha sheria.

Hata hivyo yalisema kwamba hiyo ilikuwa ni athari tu ambayo haikuifanya Hati ya Mashitaka hiyo iwe potofu kisheria kiasi cha kubatilisha hukumu iliyotolewa. Zaidi ya yote hayo mahakama yalisisitiza kuwa athari kwenye Hati ya Mashitaka yenyewe haikusababisha upotoshaji wa haki dhidi ya mshitakiwa kwa vile hakufazaika wala kubabaishwa na athari hiyo kiasi cha kutoelewa lile kosa ambalo alikabiliwa nalo.

Ni vigumu kuelewa kama Mahakama ya Rufani ya Afrika Mashariki katika Terrah Mukindia (i.h.j) ingeshikilia uamuzi wake ule mintaarafu ya kosa la nne na la tano kama makosa mengine yote matatu yaliyobakia yangekuwa na athari kama yale mawili. Inafikiriwa tu kuwa msimamo kama huo ungeikebehi sheria badala ya kuitekeleza kwa haki. Kipimo kizuri ni kuona ushahidi unasema hivi: kama unaonyesha mshitakiwa ametendewa haki, pamoja na athari kama hizo kuwepo, basi sio halali kubatilisha hukumu iliyopitishwa dhidi yake ili tu kukubaliana na kanuni zilizowekwa. Nia na madhumuni ya kanuni zenyewe ni kutekeleza, sio kubananga, haki.

Jambo hili linajitokeza wazi katika mashauri mawili yafuatayo. Kwanza ni R. v. Omari Ismaili. (1970 H.C.D. n341). Jaji Mkuu Georges (kama alivyokuwa) alibatilisha hukumu ya kumtia hatiani mshitakiwa kwa kosa la kusababisha kifo kutokana na kuendesha gari kwa njia ya hatari kinyume na fungu la 44A(1)(a) la Sheria la Usalama Barabarani. Hati ya mashitaka katika shauri hili ilieleza kuwa: "Mshitakiwa aliendesha gari kwa hatari, hakuzingatia hali na mazingira ya barabara yenyewe". Jaji Mkuu Georges alisisitiza kwamba muhtasari wa maelezo ya hati hiyo haukutosha kwa vile haueleza sababu za kuonyesha kwamba mshitakiwa aliendesha gari lake kwa njia ya hatari. Na licha ya athari hiyo ya ushahidi wenyewe katika mwenendo wa shauri hakudhihirisha vitendo vya uendeshaji wa hatari.

Lakini katika shauri la Joachim Gregory v. R., (1975 L.R.T. n44) Jaji Lugakingira aliikataa rufani ya mshitakiwa aliyetiwa hatiani kwa kosa la kusababisha kifo kutokana na uendeshaji wa hatari. Jaji huyo alikiri kuwa muhtasari wa kosa lililohusika haukufafanua aina ya uendeshaji wa hatari uliodaiwa, lakini aliona kwamba kulikuwa na ushahidi wa kutosha kuthibitisha uendeshaji wa hatari.

Mbali na ufafanuzi wa kosa linalodaiwa kisheria, uainishaji wa vitu au watu ni muhimu vile vile kuonyeshwa katika muhtasari wa kosa. Sio vigumu kuelewa na kuona haja ya mshitakiwa kufahamu vitu vinavyodaiwa kuwa ameviiba. Vitu hivyo, kama nguo, gari au chochote kile ni vizuri vitajwe kiasic ha kumpa taarifa ya kutosha mshitakiwa. (Saidi Abdallah v. R. (1970) H.C.D. n62). Kwa mfano kama ni shtaka la wizi wa gari inatosha kutaja aina ya gari. Sio lazima kuelezea rangi, nambari ya mashine yake wala ya kuandikishwa. Masuala hayo yatathibitishwa kwa ushahidi wakati wa mwenendo wa shtaka lenyewe. Isipokuwa inapasa, ingawa sio lazima, kuelezea mali hiyo ni ya nani.

Kutokuanisha vitu vinavyohusika na kosa lenyewe sio lazima kubatilishe hukumu iliyofikiwa; kipimo ni iwapo athari imesababisha kutotendeka kwa haki au la. Kwa mfano katika Saidi Abdallah v. R. (K.h.j) mrufani alishitakiwa na kutiwa hatiani kwa kosa la kuvunja duka na kuiba mali ya thamani ya shilingi 2,000/= dhidi ya fungu la 296 la Kanuni ya Adhabu. Muhtasari wa kosa hilo haukuainisha mali, yaani vitu vilivyoibiwa. Hata hivyo mahakama kuu yaliacha kubatilisha hukumu ya mahakama ya awali kwa vile mwenendo wa shauri ulidhihirisha mshitakiwa alielewa vitu ambavyo alidaiwa ameviiba kutoka kwenye duka lililovunjwa.

Sio vigumu kuelewa kama athari ya kutoainisha vitu imesababisha kutotendeka haki au la. Ushahidi ambao umenakiliwa kwa usahihi katika mwenendo wa shauri, kwa mfano, utaonyesha mashahidi ambao wamevitambua vitu vilivyoibiwa. Na pengine vitu hivyo vinaweza kuwa vilitolewa mahakamani kama vielelezo.

Katika makosa ya mashambulizi au mauaji na kadhalika inapasa kuelezea jina la mtu aliyeshambuliwa au kuuawa. Lakini kutofanya hivyo sio lazima kubatilishe hukumu ya kumtia mshitakiwa hatiani. Mara nyingi aliyeshambuliwa atataja jina lake wakati akitoa ushahidi mahakamani.

Tatizo liko katika mauaji ambapo marehemu aliyeuawa hawezi kutoa ushahidi mahakamani. Lakini sio lazima mshitakiwa alifahamu jina la marehemu iwapo ushahidi unathibitisha kuwa yeye ndiye aliyemwua marehemu huyo kwa kukusudia. Kila shauri lazima kuangaliwa kufuatana na mazingira yake.

Mashitaka kuhusiana na makosa zaidi ya moja yanaweza kuwekwa kwenye Hati au Taarifa ya Mashitaka moja kwa mashauri mawili makubwa. Kwanza makosa hayo yawe yametendwa pamoja. (F.133(1), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j) Au pili, makosa hayo yawe yanafanya au ni sehemu ya mfululizo wa makosa ya aina moja au yanayofanana. (K.H.J.).

Tuanze na makosa yanayotendwa kwa pamoja. Mfano: mtuhumiwa anaweza kuvunja nyumba na kuiba, wakati huo huo akampiga mwenye mali ili asiweze kumzuia kuiba. Hivyo kwa wakati mmoja yametendeka makosa mawili mbalimbali: kuvunja nyumba na kuiba, pia wizi wa kutumia nguvu. Itakuwa ni sahihi kumshitaki mtuhumiwa kwa makosa yote hayo mawili katika Hati ya Mashitaka moja. Shauri lake litasikilizwa na ushahidi utatolewa kuhusiana na makosa yote mawili kwa pamoja. Kwa kawaida ushahidi utatolewa kwa jumla ukitilia maanani vipengele ambavyo ni lazima vithibitishwe kisheria. Mwisho wa kesi mahakama huuchambua ushahidi huo na kuona iwapo kila kosa lililodaiwa limethibitishwa au vipi.

Katika shauri la Joseph Odoro v. R., mshitakiwa alipatikana na hatia ya makosa matatu: kujeruhi kwa nia ya kusababisha madhara makubwa, kuharibu mali makusudi na tatu, kumzuia polisi wakati akiwa kazini. Mahakama ya Rufani ya Afrika Mashariki yaliafiki kuwa kosa la kwanza na la pili yalitendwa wka pamoja na mrufani mnamo tarehe 17 Julai 1953, hivyo ilikuwa sahihi kuyaunganisha makosa hayo katika Hati ya Mashitaka moja. Lakini yaliona ni kosa kwa kosa la tatu kuunganishwa na makosa yale mengine kwa vile lilitendeka Julai 21, 1953. Hata hivyo mahakama yaliikataa rufani kwa vile mrufaniwa alitendewa haki licha ya athari zilizokuwepo.

Inaendelea toleo lijalo

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook